TPA yaongoza mashirika yaliyotoa gawio, ikichangia Sh205 bilioni
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akipokea Gawio kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa (kulia) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPA, Balozi Ernest Mangu. Picha na Ikulu
Muktasari:
- Huu ni mwaka wa nne mfululizo kwa TPA kuendelea kuwa kinara katika utoaji wa gawio la asilimia 15 ya mapato ghafi.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imeendelea kuwa kinara wa kutoa gawio kati ya taasisi zinazochangia mfuko mkuu wa Serikali, ikichangia Sh205.5 bilioni kutoka Sh181 bilioni za mwaka jana.
Mamlaka hiyo, ilishika nafasi ya kwanza hata katika gawio la mwaka jana, baada ya kuchangia Sh181 bilioni, ikizidi taasisi na mashirika mengine yote ya Serikali.
Hayo yameelezwa leo, Jumanne Juni 30, 2026 na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu alipozungumza katika siku ya gawio.
Ametaja mashirika mengine ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) iliyochangia Sh61 bilioni, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Sh42.8 bilioni na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Sh27.9 bilioni.
Mengine ni Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) Sh20.4 bilioni, Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa kazi (Osha) Sh15 bilioni na Shirika la Viwango (TBS) Sh14.7 bilioni.
Yanayofuata, amesema ni Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) Sh11.4 bilioni, Shirika la Reli Tanzania (TRC) Sh11 bilioni, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) Sh10.6 bilioni na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) Sh10.1 bilioni.
Katika taarifa yake, TPA imesema mafanikio hayo yanaakisi kuimarika kwa shughuli za biashara ya bandari, ongezeko la mizigo inayopita katika bandari za Tanzania na juhudi zinazoendelea za kuboresha miundombinu na huduma.
Huu ni mwaka wa nne mfululizo kwa TPA kuendelea kuwa kinara katika utoaji wa gawio la asilimia 15 ya mapato ghafi, hatua inayodhihirisha mwenendo mzuri wa kifedha wa mamlaka hiyo na mchango wake katika kuimarisha mapato ya Serikali.