Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hii hapa sababu Chaumma kumkataa Mwalimu

Muktasari:

  • Vuguvugu la baadhi ya makada wa chama hicho kushinikiza kuondolewa madarakani kwa Mwalimu, lilianza jana baada ya wajumbe wa sekretarieti ya Chaumma, kuwasilisha kwa Kamati Kuu waraka wa kutokuwa na imani naye



Dar es Salaam. Baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), wametaja sababu za kutokuwa na  imani na katibu mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu ikiwamo kushindwa kueleza chanzo cha fedha zinazotumika katika shughuli za chama hicho.

Sababu nyingine zilizotajwa ni matumizi mabaya ya ofisi, ubadhirifu wa fedha, kuwadharau viongozi wenzake, kuifanya Chaumma kuitwa ‘CCM B’ na kupongeza ushindi wa chama tawala ilhali haukuwa msimamo wa chama hicho.

Vuguvugu la baadhi ya makada wa chama hicho kushinikiza kuondolewa madarakani kwa Mwalimu, lilianza jana baada ya wajumbe wa sekretarieti ya Chaumma, kuwasilisha kwa kamati kuu waraka wa kutokuwa na imani naye.

Hatua hiyo, ikamlazimu Mwalimu aandike barua ya kuomba uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili, hivyo amejiweka kando na wadhifa wake kuruhusu uchunguzi huru.

Licha ya hatua hiyo ya Mwalimu, baadhi ya wajumbe, wameiambia Mwananchi kuwa, uchunguzi na kujiweka kando kwa muda pekee hautoshi, wanahitaji aachie wadhifa huo ili apewe mwingine mwenye maadili.

Hata hivyo, Mwananchi ilimtafuta Mwalimu kuzungumzia madai hayo ya kukataliwa lakini simu yake ilikuwa haipatikani.

Leo Jumanne Juni 30, 2026, chama hicho kimefanya kikao cha halmashauri kuu ambacho ndicho kilichokuwa na uamuzi wa mwisho kuhusu hatima ya nafasi ya Mwalimu na hadi saa 11:00 jioni habari hii ilipoandikwa bado kikao kilikuwa kinaendelea.


Kwa nini hawamtaki

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa makatibu wa mikoa wa Chaumma, Basil Lema amesema malalamiko dhidi ya Mwalimu yamekuwa yakiwasilishwa katika vikao halali vya chama kwa muda mrefu, lakini hawakuwahi kupata majibu ya kuridhisha.

Moja ya malalamiko hayo, amesema ni kitendo cha Mwalimu kupongeza ushindi wa CCM bila kuwashirikisha viongozi wa Chaumma katika ngazi za mikoa ili kupata tathmini ya hali halisi ya uchaguzi.

"Nilimfuata binafsi kumuuliza kwanini alienda kupongeza ushindi wa chama tawala bila hata kuwasiliana na makatibu wa mikoa.

“Kwa mfano, hali ya Kilimanjaro ilikuwa mbaya, lakini hakutafuta taarifa kutoka kwa viongozi wa mikoa kabla ya kutoa tamko hilo," amesema.

Amesema Mwalimu pia alipaswa kushauriana na viongozi wa chama kuhusu mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kabla ya kwenda kutoa msimamo unaodaiwa kutowakilisha uamuzi wa chama.

Basil amekosoa kwa kushiriki katika tukio la kumuapisha Rais Samia Suluhu Hassan na kwa kuwasilisha maoni mbele ya Tume ya Jaji Mohamed Chande bila ridhaa ya vikao vya chama.

Kwa upande wa matumizi ya fedha, Basil amedai Mwalimu hajawahi kueleza wazi chanzo cha fedha zinazotumika katika shughuli za chama.

"Tunaona fedha zikitumika lakini hajawahi kutueleza zinatoka wapi. Wakati mwingine huzitoa mfukoni na kuzigawa bila utaratibu unaoeleweka, jambo linalozua maswali mengi," amesema.

Amesema mgawanyo wa fedha umekuwa ukifanyika bila uwazi na wakati mwingine kwa upendeleo, huku akidai pia kuwa, chama kimekuwa kikiendeshwa bila baraza kuu kufanya kazi ipasavyo.

"Makatibu wa mikoa tunaunga mkono msimamo wa kamati kuu. Hatumtaki Mwalimu; tunataka kukisafisha chama chetu, na asiyeunga mkono hilo atuachie nafasi," amesema Basil.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu, Eliya, amesema ingawa Mwalimu ameomba kuundwa kwa tume ya uchunguzi, hawezi kuelekeza namna wajumbe watakavyofanya uamuzi wao.

"Kinachoongoza ni katiba ya chama. Tume itafanya kazi yake, lakini msimamo wetu unabaki kuwa hatumtaki Mwalimu. Wakati wa kufanya uamuzi ukifika, jambo hilo litaamuliwa kwa mujibu wa taratibu za chama," amesema.

Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma Bara, Benson Kigaila amesema hatima ya Mwalimu kuhusu kukataliwa au kutokataliwa na wajumbe itafahamika baada ya mchakato wa ndani wa chama kukamilika.

Amesema hoja hiyo bado ipo kwenye vikao vya chama na wajumbe wa Halmashauri Kuu ndiyo wenye mamlaka ya kufanya uamuzi wa mwisho.

Kutokana na hali hiyo, amesema si busara kuzungumzia suala hilo kana kwamba tayari limehitimishwa.

"Baada ya kikao cha Halmashauri Kuu kitakachokamilika jioni ya leo, kila jambo litawekwa wazi kwa umma," amesema Kigaila.


Ilivyokuwa kwenye kamati kuu

Jana, wakati kikao cha kamati kuu, wajumbe walipiga kura ya kutokuwa na imani na Mwalimu wakimtuhumu kujiamulia mambo na kutumia vibaya ofisi yake.

Waraka uliosainiwa pamoja na orodha ya wajumbe waliopiga kura hiyo uliwasilishwa katika kikao hicho. Miongoni mwa wajumbe waliopiga kura ya kutokuwa na imani na Mwalimu ni Benson Kigaila.

Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani ya kikao hicho, sababu mojawapo ya kura hiyo ni madai kwamba, Mwalimu amekuwa akifanya uamuzi binafsi, ikiwamo kutoa maoni yake binafsi huku akiyawasilisha kama msimamo rasmi wa vikao vya chama.

Baadhi ya maoni yanayotajwa kutokuwa msimamo wa Chaumma ni pamoja na kuipongeza na kuisifia Tume ya Uchunguzi wa Ghasia za Oktoba 29, 2025.

Hoja nyingine iliyowasilishwa na Kigaila inahusu madai ya matumizi mabaya ya ofisi.

Inadaiwa kuwa, Mwalimu amejimilikisha magari mawili ya kifahari (mashangingi) yaliyotolewa na mmoja wa wadau kwa ajili ya kukisaidia chama.

Kwa mujibu wa madai hayo, magari hayo ni miongoni mwa yaliyotumika katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na inadaiwa moja alijimilikisha na jingine ameliuza.

Sababu nyingine iliyotajwa na vyanzo hivyo ni madai ya ubadhirifu wa fedha, hoja ambayo iliwahi kujadiliwa katika kikao kati ya Mwalimu na makatibu wa mikoa mapema mwaka huu.

Hata hivyo, katika kikao hicho Mwalimu alipewa nafasi ya kujitetea dhidi ya tuhuma hizo.

Akiwa bado anaendelea kutoa utetezi wake, alitoka ukumbini akidai wajumbe walikuwa wamemkosea heshima kwa kuvujisha taarifa za kikao hicho kwenye vyombo vya habari kabla hajamaliza kujieleza.

Hatua hiyo ilimkasirisha Mwalimu na kuondoka katika kikao hicho, huku akimuachia Mwenyekiti Hashimu Rungwe ujumbe wa kuundwa kwa chombo cha kuchunguza tuhuma zinazomkabili.