Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Eneo lililotajwa halifai kwa maisha lawa somo Tanzania



Miaka takribani 30 iliyopita, sehemu kubwa ya eneo la Xihaigu katika Mkoa wa Ningxia, kaskazini magharibi mwa China, lilitajwa na wataalamu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kuwa miongoni mwa maeneo yasiyofaa kwa makazi ya binadamu kutokana na ukame mkali, uhaba wa maji na uzalishaji mdogo wa chakula.

Leo, eneo hilo limebadilika kiasi cha kushangaza. Miji imejengwa, mashamba yanazalisha mazao yenye thamani kubwa, viwanda vidogo vinaendelea kuchipua, mamilioni ya watu wameondolewa kwenye umaskini na sehemu kubwa ya jangwa sasa ni kijani kibichi.

Katika matembezi yangu yanayoendelea hivi sasa katika mkoa huo naona kwa nchi yangu (Tanzania), hadithi hii ni darasa muhimu kuhusu namna taifa linaweza kutumia rasilimali zake, ardhi yake na watu wake kugeuza maeneo yenye changamoto kuwa vyanzo vya ustawi.

Somo la kwanza ni kwamba ardhi ni rasilimali ya kiuchumi, si eneo la kusubiri maendeleo yatokee yenyewe. Katika maeneo mengi ya Tanzania bado kuna maelfu ya hekta za ardhi ambazo hazitumiki au zinatumika chini ya uwezo wake. Wakati mwingine tunajivunia ukubwa wa ardhi tuliyonayo, lakini ukweli ni kwamba thamani ya ardhi haipimwi kwa ukubwa wake bali kwa kiwango cha uzalishaji wake.

China ilitambua jambo hilo mapema. Hadithi ya Minning Town ina funzo. Lengo halikuwa kuwapa wananchi wa eneo hilo la Xihaigu mashamba makubwa pekee, bali kuhakikisha kila kipande cha ardhi kinaingizwa katika uzalishaji wenye tija. Kupitia umwagiliaji, teknolojia, mbegu bora na upatikanaji wa masoko, ardhi iliyokuwa ikionekana haina thamani iligeuzwa kuwa chanzo cha mapato.

Tanzania ina zaidi ya hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo, lakini sehemu ndogo tu ndiyo inayotumika kikamilifu. Ikiwa taifa litawekeza kwa nguvu katika umwagiliaji, teknolojia za kisasa na miundombinu ya masoko, ardhi yetu inaweza kuwa injini kubwa zaidi ya kupunguza umaskini kuliko ilivyo sasa.

Somo la pili ni kwamba kupunguza umaskini kunahitaji kuwapeleka watu kwenye fursa, si kusubiri fursa ziwafuate watu walipo.

Moja ya maamuzi magumu yenye mafanikio nchini China ilikuwa kuhamisha baadhi ya wananchi kutoka maeneo ambayo yalikuwa hayafai kwa uzalishaji kwenda maeneo yenye fursa zaidi za kiuchumi. Japo kuna waliogoma hadi leo.

Sehemu kubwa ya mambo yaliyofanyika miaka hiyo ya 1990 yanayosimuliwa katika tamthilia maarufu ya China ya Minning Town, inayotokana na matukio halisi ya kampeni ya kupunguza umaskini nchini humo.

Ni jambo ambalo mara nyingi huibua mjadala mkali, lakini ukweli ni kwamba si kila eneo lina uwezo sawa wa kuzalisha utajiri. Serikali ya China ilitambua hilo na kuunganisha uhamishaji wa watu na uwekezaji katika miundombinu, maji, elimu na shughuli za uzalishaji.

Tanzania pia ina maeneo yenye changamoto kubwa za mazingira, ukame wa mara kwa mara na uzalishaji mdogo. Badala ya kuangalia suala hili kwa mtazamo wa misaada pekee, kuna haja ya kufikiria kwa upana zaidi kuhusu namna ya kuwaunganisha wananchi wa maeneo hayo na fursa za uchumi wa kisasa.

Somo la tatu ni ushirikiano wa maendeleo.

Katika simulizi la Minning Town, moja ya siri kubwa ya mafanikio ilikuwa ushirikiano kati ya Ningxia na Mkoa wa Fujian, ambao ulikuwa umeendelea zaidi kiuchumi. Fujian ilitoa mtaji, teknolojia, utaalamu na masoko.

Kwa Tanzania, somo hapa ni umuhimu wa kuunganisha maeneo yaliyoendelea zaidi na yale yaliyo nyuma kiuchumi. Mkoa wenye nguvu za viwanda unaweza kusaidia kukuza mkoa wa kilimo. Miji mikubwa inaweza kufungua masoko kwa maeneo ya vijijini. Kampuni kubwa zinaweza kuwa sehemu ya suluhisho la kupunguza umaskini badala ya kuwa watazamaji.

Mathalani mkoa wa Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya ipewe jukumu la kuiendeleza mikoa kama Lindi, Katavi na Rukwa.

Somo la nne, ni kwamba vita dhidi ya umaskini vinahitaji nidhamu ya kitaifa.

China haikufanikiwa kwa sababu ya sera moja au mradi mmoja, bali mafanikio yalitokana na miongo kadhaa ya utekelezaji wa malengo yaliyokuwa yanafuatiliwa kwa karibu. Kila ngazi ya serikali ilikuwa na wajibu wa kuhakikisha wananchi wanatoka kwenye umaskini.

Katika nchi nyingi za Afrika, ikiwamo Tanzania, mara nyingi tunapenda kuanzisha miradi mipya kabla ya kukamilisha iliyopo. Tunabadilisha vipaumbele kabla ya kuona matokeo ya muda mrefu. Minning Town inatukumbusha kwamba maendeleo ni matokeo ya uvumilivu, uthabiti na utekelezaji endelevu.

Tanzania tayari imewekeza katika reli ya kisasa, uzalishaji wa umeme, barabara, bandari na miradi mingine mikubwa ya kimkakati. Hatua inayofuata ni kuhakikisha uwekezaji huo unatafsiriwa kuwa ajira, mapato na ongezeko la uzalishaji kwa wananchi.

Hadithi ya Minning Town inaonyesha kwamba hakuna eneo lililolaaniwa kuwa maskini milele. Eneo ambalo wataalamu waliwahi kusema halifai kwa makazi ya binadamu leo limekuwa mfano wa mafanikio ya maendeleo.