Elon Musk apoteza Sh300 trilioni ndani ya miezi miwili

Muktasari:
- Kuporomoka kwa utajiri wake kunahusishwa moja kwa moja na kushuka kwa thamani ya hisa za kampuni yake kuu ya Tesla inayozalisha magari ya umeme.
Marekani. Utajiri wa Elon Musk, ambaye ni tajiri namba moja duniani, umeendelea kushuka na safari hii zaidi dola bilioni 22.2 (Sh57 trilioni) zimepungua ndani ya siku moja.
Desemba 2024 utajiri wake ulifikia kiango cha juu cha Dola 480 bilioni, lakini sasa umepungua kwa takriban dola 116 bilioni hadi kufikia dola 364.3 bilioni Februari 2025, kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na jarida la Wealth kupitia mtandao wake wa Instagram.
Kuporomoka huku kunahusishwa moja kwa moja na kushuka kwa thamani ya hisa za kampuni yake kuu ya Tesla, ambayo hisa zake zimepungua kwa asilimia 30 tangu Desemba 2024.
Hisa hizo zimeendelea kudorora kwa asilimia 21 tangu Januari 2025, hali ambayo imesababisha msukosuko mkubwa kwa wawekezaji na kupunguza thamani ya soko la bidhaa za kampuni hiyo kwa kiasi kikubwa.
Tesla, ambayo inachangia zaidi ya nusu ya utajiri wa Musk, imekumbwa na changamoto kadhaa mwaka huu. Ripoti zinaonyesha kuwa mauzo ya Tesla yamepungua kwa kiwango kikubwa katika masoko muhimu, hasa barani Ulaya, ambako mauzo yalishuka kwa asilimia 50 Januari 2025.
Hii imeifanya jumla ya hisa za kampuni kushuka hadi chini ya Dola 1 trilioni kwa mara ya kwanza tangu Novemba 2024.
Pamoja na hayo, Tesla inakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa kampuni za magari ya umeme kama BYD ya China, ambayo iliuza magari milioni 1.76 mwaka 2024, huku ikivutia wateja kwa bei nafuu na teknolojia ya kisasa.
Kadhalika, siasa za Elon Musk zimeiathiri Tesla, kwani nafasi yake katika utawala wa Trump kama mkuu wa Idara ya Ufanisi wa Serikali (DOGE) imepunguza imani ya wawekezaji. Wengi wanaona kuwa shughuli zake za kisiasa zinapunguza muda wake wa kuongoza kampuni.
Mabadiliko ya sera pia yamechangia kuporomoka kwa hisa. Trump ametangaza kufuta ruzuku za magari ya umeme na kulegeza sheria za uchafuzi wa mazingira, jambo linaloweza kuathiri mapato ya Tesla.
Mahitaji ya magari ya umeme yamepungua huku ushindani ukiongezeka. Makampuni kama BYD ya China na Volkswagen ya Ujerumani yanatoa magari ya bei nafuu na teknolojia ya kisasa, hali inayoiweka Tesla kwenye shinikizo kubwa sokoni.
Pamoja na changamoto hizi, Musk amepanga kuanzisha majaribio ya teksi zinazojiendesha (robotaxi) jijini Austin, Texas, ifikapo Juni 2025. Hata hivyo, wawekezaji wanaendelea kuwa na mashaka kuhusu uwezo wa Tesla kushindana na makampuni mengine yanayoingia kwa kasi katika teknolojia hiyo.
Aidha pamoja na kupungua kwa utajiri wake, Musk bado anashikilia nafasi ya kwanza kama mtu tajiri zaidi duniani, ingawa hatima ya Tesla na utajiri wake kwa jumla, itategemea hatua atakazochukua kurejesha imani ya wawekezaji na wateja katika siku za usoni.