Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Biteko: Bei ya mafuta zitaendelea kushuka

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akizungumza wakati wizara yake  ilipokuwa ikiwasilisha taarifa kuhusu mwenendo wa biashara ya mafuta  nchini kwa kipindi cha Septemba hadi  Desemba 2023 kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Muktasari:

  • Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema jitihada za wizara yake na taasisi zilio chini ya wizara hiyo zimesababisha kushuka kwa gharama za mafuta nchini huku muda wa meli kushusha mafuta ukipungua.

Dodoma. Serikali imesema jitihada zilizofanyika zimesababisha kuendelea kushuka gharama za uingizaji wa mafuta ya dizeli na petroli nchini na hivyo kuchangia unafuu wa gharama za bidhaa hiyo.

Mbali na hilo imesema muda wa meli za mafuta kushusha mzigo bandarini umepungua kutoka siku tisa hadi nne badala ya siku tisa.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema hayo leo Ijumaa Januari 19, 2024; jijini Dodoma wakati wizara hiyo ilipowasilisha taarifa kuhusu mwenendo wa biashara ya mafuta nchini kwa kipindi cha Septemba hadi Desemba 2023, kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, Katibu Mkuu, Felchesmi Mramba, baadhi ya wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo na watendaji kadhaa wa wizara hiyo.

Amesema Wizara ya Nishati, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), zimefanya kazi kubwa iliyosababisha kushuka kwa gharama za uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi.

Amesema hapo awali gharama za mafuta zilikuwa zikiongezeka kila mwezi lakini hivi sasa zinashuka kutokana na jitihada za Serikali.

“Hivi karibuni mlisikia Waziri wa Kenya akisema bei za mafuta nchini humo zipo juu na za Tanzania zipo chini sababu ya gharama za uingiza, na wengine pia walio nje wanatoa ushuhuda kwamba walau sisi gharama zetu zina unafuu,” amesema.

Dk Biteko amesema Serikali itaendelea kusimamia kwa ukamilifu PBPA ili iendelee kufanya kazi kwa ufanisi kwa sababu tayari imekuwa ni mfano wa kuigwa kwa nchi zinazoizunguka Tanzania.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kuiboresha Kampuni ya Mafuta ya TANOIL ambayo ni kampuni tanzu ya TPDC kutokana na umuhimu wake katika biashara ya mafuta nchini.

Amesema TANOIL imekuwa ni kimbilio hasa nyakati zinapotokea changamoto za upatikanaji mafuta kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu.

Muda wa meli kupakua

Mkurugenzi Mkuu wa PBPA, Erasto Mulokozi amesema Serikali imechukua hatua za kuboresha mfumo wa upakuaji mafuta melini na kuhakikisha meli hazikai muda mrefu bandarini.

Amesema hatua hizi ni kuagiza matenki ya Kampuni ya Mafuta ya TIPER kutumika kupokea na kuhifadhi mafuta, hatua ambayo imewezesha meli za mafuta ya dizeli kutumia siku nne kushusha mafuta badala ya siku tisa.

Mulokozi amesema hatua hiyo imeleta unafuu kwa mlaji na kupunguza gharama ambazo Serikali ilikuwa ikilipa kutokana na muda wa meli kukaa bandarini.

Amesema Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ipo katika hatua za mwisho za kuanza ujenzi wa sehemu maalumu ya kupokea na kuhifadhi mafuta ijulikanayo kama ‘single receiving terminal’.

Mulokozi amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutafanya meli kuwa na uwezo wa kupakua mafuta kati ya saa 48 na 36 na hivyo kumaliza kabisa changamoto ya gharama za meli kukaa bandarini.

Pia amesema kabla ya kuwepo taasisi ya PBPA upotevu wa mafuta kutoka bandarini ulikuwa ni asilimia 0.5 lakini hali ya upotevu kwa sasa imedhibitiwa na upotevu umepungua hadi asilimia 0.1.

Amesema Serikali inaendelea na jitihada za kuondoa upotevu kabisa kwa kufunga mita za kupimia mafuta pamoja na mfumo wa uangalizi wa mita hizo (SCADA) ambao utakuwa chini ya PBPA.

Mkurugenzi huyo amesema mfumo huu utafanya kazi kwa muda wote, meli inaposhusha mafuta na hivyo kuondoa uwezekano wa upotevu wa mafuta kabisa wakati wa ushushaji wa mafuata.

Aidha Mulokozi, amesema mfumo huo wa SCADA utaweza kuona shughuli ya ushushaji wa mafuta kwa bandari za mikoa inayopokea bidhaa hizo za Tanga, Mtwara na Dar es Salaam.