Prime
Dhahabu na tumaini jipya la kulinda uchumi Tanzania
Muktasari:
- Ripoti ya Tathmini ya Hali ya Uchumi ya kila Mwezi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonesha kuwa mauzo ya dhahabu nje ya nchi yalizalisha Sh13.54 trilioni katika mwaka ulioishia Machi 2026, yakichangia kati ya asilimia 30 hadi 40 ya mapato yote ya fedha za kigeni ya Tanzania
Dar es Salaam. Ukuaji wa mauzo ya dhahabu nje ya nchi umetajwa kusaidia kulinda uchumi wa Tanzania dhidi ya mshtuko wa bei ya mafuta duniani, ripoti ya Tathmini ya Uchumi ya Kila Mwezi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza.
Ripoti hiyo ya Aprili, 2026, inaonesha kuwa, dhahabu imekuwa nguzo muhimu ya uthabiti kwa sekta ya nje ya Tanzania wakati mataifa mengi yanayotegemea bidhaa kutoka nje yanakabiliwa na ongezeko la gharama za mafuta, mbolea na usafirishaji kufuatia kufungwa kwa Mlango wa Hormuz Machi 2026.
Mauzo ya dhahabu nje ya nchi yalizalisha Sh13.54 trilioni katika mwaka ulioishia Machi 2026, yakichangia kati ya asilimia 30 hadi 40 ya mapato yote ya fedha za kigeni Tanzania.
Ripoti hii inaeleza kuwa, utendaji huo mzuri unasaidia kufidia ongezeko la gharama za uagizaji wa mafuta huku bei ya mafuta ghafi ikiongezeka katika soko la dunia.
“Kwa kawaida, vipindi vya mvutano wa kisiasa duniani husababisha bei za mafuta na dhahabu kupanda kwa pamoja,”inaeleza ripoti hiyo.
Mlango wa Hormuz hupitisha karibu asilimia 20 ya mafuta yote ya dunia huku mapigano yaliyoibuka Februari mwaka huu yakivuruga usafirishaji kupitia njia hiyo na kusababisha mishtuko katika masoko ya bidhaa duniani.
Ripoti hiyo inaonya kuwa kupanda kwa pamoja kwa gharama za mafuta, usafirishaji na pembejeo za kilimo kunasababisha mshtuko upande wa uzalishaji wenye athari kwa mfumuko wa bei, thamani ya sarafu na uwezo wa wananchi kununua bidhaa.
Kwa Tanzania, athari hizo tayari zimeanza kuonekana katika uchumi wa ndani kupitia kupanda kwa bei ya mafuta ambayo imeongeza gharama za usafirishaji na usambazaji katika mifumo yote ya ugavi nchini.
Kwa kuwa bidhaa nyingi nchini husafirishwa kwa njia ya barabara, ongezeko la gharama za usafirishaji linatarajiwa kuongeza bei za chakula, saruji, mbolea na bidhaa nyingine za matumizi ya kila siku.
Kaya za kipato cha chini zinatarajiwa kuathirika zaidi kwa sababu sehemu kubwa ya mapato yao hutumika kwenye usafiri, chakula na nishati.
Hata hivyo, ripoti ya BoT inaonyesha kuwa mapato ya dhahabu yanaendelea kuwa kinga muhimu kwa uchumi wa Taifa kwa kusaidia akiba ya fedha za kigeni na kupunguza shinikizo kwenye nakisi ya urari wa biashara ya nje.
Akizungumzia suala hilo, mchambuzi wa uchumi Profesa Abel Kinyondo amesema mfumuko wa bei Tanzania bado unaweza kudhibitika kwa kiasi kikubwa kutokana na mapato ya dhahabu na usimamizi makini wa uchumi.
Amesema Tanzania inanufaika na mauzo ya dhahabu tangu kipindi cha janga la Uviko -19, ikiizidi sekta nyingine zote kama chanzo kikuu cha mapato ya fedha za kigeni nchini.
“Baada ya Uviko-19 kulifuata vita vya Urusi na Ukraine, kisha mvutano wa kisiasa katika nchi za Mashariki. Migogoro hii ya dunia ilisababisha bei za dhahabu kupanda kwa kasi. Pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji kutoka kwa wazalishaji wakubwa wa dhahabu, hali hii imeongeza kwa kiasi kikubwa mapato ya mauzo ya nje,” amesema.
Hata hivyo, ameonya kutegemea sana sekta hiyo akisema, “hatupaswi kuridhika kupita kiasi kwa sababu kinachopanda kinaweza pia kushuka. Bei za dhahabu zinaweza kushuka baadaye, ndiyo maana Tanzania lazima iendelee kuupanua na kuutofautisha uchumi wake.”
Rais wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Tanzania (Femata), John Bina amesema kuendelea kupanda kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia kumepunguza makali ya bei ya dizeli wanayotumia katika shughuli zao za kila siku.
“Gharama za kupata madini ni kubwa sana, hivyo ukuaji wa bei ya dhahabu katika soko la dunia unatokana na mahitaji yake, kunasaidia kupunguza maumivu hata kwetu pia kwa sababu tunaona faida; ingekuwa mafuta yamepanda na bei ya dhahabu inashuka hali ingekuwa mbaya,” amesema.
“Hakuna mchimbaji aliyesitisha shughuli zake hadi sasa, kwa sababu haya ndiyo maisha yetu, tutaendelea kupambana kwa sababu hatujui kesho yetu, bei ikipanda ya mafuta zaidi na dhahabu kushuka hapo labda ndiyo unaweza kusema tusitishe huduma kwa muda.” Ametumia nafasi hiyo kuwataka wachimbaji kuwa na mbadala wa uwekezaji katika shughuli wanazofanya badala ya kutegemea uchimbaji pekee, ili mambo yanapokuwa si mazuri sehemu moja wawe na sehemu ya kuegama.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amesema mara zote bei ya dhahabu inapoongezeka inakuwa ni neema nchini.
“Bidhaa inapoongezeka, mauzo mapato yanaongezeka kwa nchi, fedha ulizopata jana zinakuwa tofauti na leo, mapato yanaongezeka,” amesema.
Amesema mbali na kuongezeka kwa fedha za kigeni hata mchango wake katika pato la Taia huongezeka licha ya kuwa ni vigumu kwa kipindi hiki kuupima bali hadi mwaka unapofikia tamati.
Kwa takwimu za mwaka 2024/2025 mchango wa madini ulikuwa asilimia 11 katika pato la Taifa. “Kwa sasa huwezi kupima kwani huwa ni mwaka mzima,” amesema.