CAG akosoa uendeshaji kiwanda cha Keko, atoa mapendekezo

Muktasari:
- Abaini mauzo yaliyofanyika mwaka 2023 na 2024 ya Sh4.58 bilioni na Sh4.39 bilioni mtawalia, yalifanyika kwa wateja bila ya kuwa na mkataba. Hii ilitokana na kutofuata sheria za ndani zinazosimamia mauzo.
Moshi. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amekosoa mambo kadhaa katika uendeshaji wa kiwanda cha dawa cha Keko, ikiwamo kufanya mauzo kwa mkopo kwa wateja bila kuwa na mkataba wa kisheria baina yao.
Katika taarifa yake ya ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ulioishia Juni 30, 2024, CAG amebainisha pia kusuasua kwa uzalishaji wa dawa katika kiwanda hicho cha Serikali.
CAG, Charles Kichere amesema kipengele cha 5.1 na 5.2 cha taratibu za uendeshaji wa mauzo za kiwanda cha dawa Keko, za mwaka 2023, kinataka mauzo yote yanayofanyika kwa mkopo kwa wateja yafanyike kwa njia ya mkataba.
Hata hivyo, katika ukaguzi wa CAG katika kiwanda hicho, amebaini mauzo yaliyofanyika mwaka 2023 na 2024 ya Sh4.58 bilioni na Sh4.39 bilioni mtawalia, yalifanyika bila ya kuwa na mkataba.
Hii ilitokana na kutofuata sheria za ndani zinazosimamia mauzo. Mauzo yanayofanyika bila ya mkataba yanaweza kusababisha kiwanda hicho kushindwa kurejesha fedha za bidhaa zilizouzwa kwa mkopo kwa wateja.
Kutokana na changamoto hiyo, CAG amependekeza kiwanda hicho kihakikishe mauzo yote yanayofanyika kwa wateja yanakuwa na mkataba.
Kusuasua kwa uzalishaji
Kiwanda cha dawa Keko kina idara ya uzalishaji yenye maeneo mawili ambayo ni la uzalishaji dawa aina ya penicillin na eneo la uzalishaji wa dawa ambazo siyo penicillin ambayo huzalisha kapsuli na vidonge mtawalia.
CAG amebaini kuwa kiwanda kilifanya uzalishaji wa dawa chini ya kiwango kilichopangwa, kwa miaka mitatu mfululizo ambapo uzalishaji ulikuwa asilimia 40, 66 na 40 kwa mwaka 2021/22, 2022/23 na 2023/24 mtawalia.
“Uzalishaji wa kiwango cha chini ya lengo ulisababishwa na kutopatikana kwa malighafi kutokana na kutokuwa na mtaji wa kutosha wa kufanya kazi, kuharibika kwa mashine na kukatika kwa umeme,”ameeleza CAG katika taarifa yake.
Amesisitiza kuwa uzalishaji wa dawa chini ya kiwango unasababisha kutokukidhi mahitaji ya wateja na kukosa mapato, hivyo amependekeza kiwanda kiweke na kutekeleza mikakati thabiti ya kuimarisha mtaji utakaowezesha upatikanaji wa fedha za kununua malighafi na kuongeza uzalishaji.
Kutozingatia njia bora za uzalishaji
Katika ukaguzi huo, CAG amerejea Kanuni ya 7 (1) na (2) ya Vyakula, Dawa na Vipodozi Tanzania (Utaratibu Bora wa Utengenezaji) za mwaka 2018 kuelezea namna kiwanda kilivyoshindwa kuzingatia njia bora za uzalishaji.
Kanuni hizo zinaitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania kutoa cheti kwa kiwanda ambacho kimetimiza mahitaji yanayohitajika ya utaratibu bora wa utengenezaji na cheti kitakuwa halali kwa kipindi cha miaka mitatu.
Hata hivyo, CAG amesema katika mapitio yake ya ripoti ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania ya Mei 2023 yalibaini kuwa kiwanda hicho hakikuzingatia mahitaji ya chini ya mwongozo huo katika utaratibu bora wa utengenezaji dawa.
CAG ameeleza hali ya mapendekezo ya utaratibu bora wa utengenezaji yaliyotolewa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba kwenda kwa kiwanda cha Dawa Keko yalibaini kiwanda kifanyia kazi mapendekezo 29 sawa na asilimia 59 kati ya mapendekezo 49 ambayo yaligawanywa kwa umuhimu, ukubwa na udogo.
Hali hiyo imesababishwa na mambo mbalimbali, ikiwamo uwepo wa teknolojia ya zamani ya mashine na vifaa vinavyosababisha kutokuwepo kwa ufanisi wa uzalishaji na idadi ndogo ya wafanyakazi wa kiufundi katika kiwanda.
Aidha, ukosefu wa mtaji wa kufanya kazi kwa ajili ya kununua malighafi na kwamba hali hiyo ya kufuata utaratibu usioendana na utaratibu bora wa utengenezaji huweza kusababisha kushindwa kupenya katika soko pana.
CAG amependekeza kiwanda hicho kihakikishe kinaajiri idadi ya kutosha ya wafanyakazi wa kiufundi, ili kutekeleza majukumu ya uzalishaji kwa mujibu wa utaratibu bora wa utengenezaji.
Pia CAG amependekeza kiwanda kibadilishe mashine na vifaa vya zamani na kuwekwa mashine na vifaa vyenye teknolojia ya kisasa, ili kuhakikisha ufanisi wa uzalishaji kulingana na utaratibu bora wa utengenezaji.
Mbali na mapendekezo hayo, CAG amependekeza kiwanda hicho kishirikiane na Wizara ya Fedha juu ya kuboresha mtaji wa kiwanda, ili kuwezesha ununuzi wa malighafi na vifaa vya kisasa vya uzalishaji.