Prime
CAG abaini kasoro lukuki mashine za EFD

Muktasari:
- Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kwa mwaka wa fedha 2023/24 amebaini kasoro lukuki za matumizi ya mashine za kodi za kielektroniki (EFD).
Mwanza. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) haikusimamia ipasavyo matumizi ya mashine za kodi za kielektroniki (EFD), katika kufuatilia mauzo na bidhaa hivyo kushindwa kuhakikisha utii wa kodi na ukusanyaji wa mapato.
Katika Ripoti ya Ukaguzi wa Utendaji kuhusu Usimamizi wa Mashine za Kielektroniki za Kodi kwa mwaka wa fedha 2023/24 aliyoiwasilisha bungeni Aprili 16, 2025, Kichere amesema TRA haikutambua ipasavyo watumiaji wanaostahili kwa sababu ya ukosefu wa taarifa kamili za mapato ya wafanyabiashara, pamoja na kucheleweshwa kwa mikakati ya kupunguza gharama za EFD, ukosefu wa mikataba ya huduma kati ya wasambazaji na watumiaji na udhaifu katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa matumizi ya mashine hizo.
Amesema mapitio ya taarifa za watumiaji wa mashine hizo na namba ya mlipa kodi (TIN) kufikia Juni 2024 yalibaini kati ya wafanyabiashara milioni 2.057 ni 243,338 ndio waliokuwa wamesajiliwa kutumia mashine za EFD sawa na asilimia 12.
“TRA ilieleza si wafanyabiashara wote walio na TIN wanapaswa kutumia EFD, baadhi wameachwa kwa mujibu wa viwango vya mapato. Hata hivyo, mfumo wa sasa hauonyeshi kwa uwazi wafanyabiashara waliofaa kusajiliwa kwa EFD bila kuzingatia kiwango cha mapato,” amesema CAG Kichere.
Amesema asilimia 89 ya wafanyabiashara waliokuwa wamesajiliwa kiwango chao cha mapato hakikujulikana hali inayoashiria TRA haikuwa na taarifa sahihi za mapato ya wafanyabiashara, jambo linaloathiri tathmini ya uhalali wa kutumia EFD.
Taarifa hiyo imeendelea kusema mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2023/24 malengo ya usajili wa EFD yamepungua kutoka asilimia 101 hadi kufikia asilimia 46 kutokana na kupunguzwa kwa malengo ya upatikanaji wa mashine hizo hasa katika maeneo ya kikodi ya Kinondoni na Kariakoo, bila kuzingatia idadi ya wafanyabiashara waliosajiliwa na mzigo wa kazi kwa maofisa wa TRA.
CAG amesema ukaguzi ulibaini idadi ya malengo ya usajili wa EFD imekuwa ikiongezeka kutoka mashine 35,691 hadi 100,410 kwa mwaka ambapo mwaka wa fedha 2020/21 lengo la kusajili mashine 35,691 lilikamilishwa kwa mafanikio baada ya mashine 35,895 kusajiliwa sawa na asilimia 101 ya utendaji.
“Mwaka wa fedha 2021/22 lengo liliongezeka hadi mashine 45,641 lakini mashine 40,044 pekee ndizo zilizosajiliwa, sawa na asilimia 88 ya utekelezaji. Mwaka wa fedha 2022/23 mashine 51,353 zilisajiliwa dhidi ya lengo la 57,999 sawa na asilimia 89.
Hata hivyo, mwaka wa fedha 2023/24 licha ya ongezeko la lengo kufikia mashine 100,410, usajili halisi ulikuwa mashine 45,761 tu, sawa na kiwango cha chini kabisa cha utekelezaji cha asilimia 46,” amesema.
Baadhi ya sababu zilizosababisha kushuka kwa usajili huo zimeelezwa ni kutokuwepo kwa mifumo iliyounganishwa kati ya TRA na wadau wengine wa kibiashara, hivyo kukwamisha ufuatiliaji mzuri wa shughuli za walipa kodi.
“Hali hii imesababisha uongozi wa TRA kutumia mbinu za jadi kama operesheni za uwanjani (enforcement) ili kuongeza usajili wa EFD. Hata hivyo, kwa mujibu wa uongozi wa TRA, operesheni hizo zilisitishwa kufuatia mgogoro ulioibuka kati ya wafanyabiashara na TRA, jambo lililoathiri kwa kiasi kikubwa utendaji ukilinganishwa na miaka iliyopita,” amesema CAG Kichere.
Katika hatua nyingine, CAG amesema TRA ilibaini watumiaji 300 wa EFD kati ya 380 walizitumia mashine hizo vibaya kwa kutoa risiti bandia kwa wafanyabiashara 504 na kusababisha upotevu wa Sh249.4 bilioni huku, Sh12.8 bilioni haikurejeshwa sababu zikitajwa kuwa ni pamoja na kutosimamia kikamilifu taratibu za usajili na upungufu katika matumizi ya taarifa za EFDMS.
CAG kupitia taarifa hiyo amesema, wafanyabiashara 3,206 waliosajiliwa hawakutumia EFD na kufanya TRA iwapige faini ya Sh7.1 bilioni kutokana na kutotoa risiti kwa mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2023/24 na wafanyabiashara wengine waliendelea kufanya biashara bila kutumia EFD huku wakikwepa kulipa kodi inavyotakiwa.
Pia, Kichere amesema mashine za kielektroniki za kutolea stakabadhi (EFDMS) zimebainika kurekodi bidhaa za ndani pekee, zinazoagizwa kutoka nje haziwezi kuunganishwa moja kwa moja bila TRA kuingilia kati, jambo linalochukua muda na kuruhusu upotoshaji wa taarifa kuhusu kiwango cha hisa za wafanyabiashara.
Hata hivyo, CAG amesema asilimia 75 ya watumiaji wa EFD walisajiliwa kwa wakati
Katika kipindi hicho, maombi 152,139 kati ya 2,021,000 ya namba ya utambulisho wa mfanyabiashara anaposajili mashine ya EFD (Unique Identification Number -UIN) yalikamilishwa kwa wakati hata hivyo, mfumo hauonyeshi sababu au siku za kucheleweshwa kwa maombi yasiyoidhinishwa, jambo linalokwamisha ufuatiliaji wa haraka.
Katika taarifa hiyo, CAG ameishauri TRA kuweka malengo ya usajili wa EFD kwa kuzingatia utendaji wa awali, idadi ya wafanyabiashara waliosajiliwa na wanaostahili kutumia EFD, kuboresha mfumo wa EFDMS ili kurekodi mienendo ya hisa, manunuzi na mauzo kwa bidhaa zote zilizotengenezwa nchini na zilizoagizwa kutoka nje.