BoT yaelekeza mbinu kukwepa fedha bandia
Baadhi ya washiriki wa semina ya namna ya kutambua noti bandia na matumizi sahihi ya fedha, iliyoendeshwa na Benki kuu ya Tanzania BoT mkoani Geita. Picha na Geofrey Chubwa
Muktasari:
- Pamoja na kuimarisha usalama wa fedha za wananchi, matumizi ya miamala ya simu na benki yanasaidia fedha kubaki katika mfumo rasmi wa kifedha.
Geita. Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imewataka wananchi mkoani Geita kutumia mifumo ya miamala kidijitali kama njia salama ya kufanya malipo ili kujikinga dhidi ya matumizi ya fedha bandia na matukio ya utapeli yanayoweza kusababisha hasara.
Rai hiyo imetolewa leo Alhamisi, Julai 23, 2026 na Ofisa Uhusiano wa BoT, Saad Makomba wakati akitoa elimu kuhusu utunzaji sahihi wa noti na namna ya kutambua noti bandia kwa wachimbaji wadogo, washereheshaji (MC), wasanii wa muziki na wajasiriamali.
Mafunzo hayo yalifanyika katika Ukumbi wa Nyerere uliopo kwenye viwanja vya maonyesho vya Dk Samia Suluhu Hassan, Kata ya Bombambili, Manispaa ya Geita.
Makomba amesema BoT imeendelea kutoa elimu hiyo kwa makundi mbalimbali nchini, lakini imeona umuhimu wa kuifikisha tena mkoani Geita kutokana na ukuaji wa shughuli za uchumi, hususan sekta ya madini, ambayo imeongeza mzunguko wa fedha na hivyo kuongeza umuhimu wa wananchi kuwa na uelewa wa kutambua noti halali na kuzitunza ipasavyo.
Amesema pamoja na kuimarisha usalama wa fedha za wananchi, matumizi ya miamala ya simu na benki yanasaidia fedha kubaki katika mfumo rasmi wa kifedha, jambo linalochochea ukuaji wa uchumi na kupunguza gharama za Serikali za kuchapisha noti mpya kutokana na uchakavu wa zile zilizopo.
"Tunashauri wananchi watumie zaidi njia za kidijitali kulipana kwa sababu zinapunguza hatari ya kuingia hasara kutokana na fedha bandia. Pia zinasaidia fedha zisichakae haraka kwa kuwa miamala mingi inapita kwenye simu na benki," amesema Makomba.
Ofisa mahusiano kutoka BoT Sadi Makomba,akitoa elimu kwa wachimbaji wadogo,wasanii na washereheshaji iliyofanyika manispaa ya Geita.
Ameongeza kuwa utunzaji usiofaa wa noti unaigharimu nchi kwa kuwa uchapishaji wa fedha unategemea rasilimali za fedha za kigeni.
Akizungumza baada ya mafunzo hayo, mchimbaji mdogo, Teonestina Christopher amesema elimu hiyo ni muhimu kwa wachimbaji kwa kuwa shughuli zao zinahusisha mzunguko mkubwa wa fedha taslimu.
"Wachimbaji wanapata fedha katika mazingira magumu sana. Elimu hii itatusaidia kuzitambua fedha bandia na kujua namna sahihi ya kuzitunza ili tusipate hasara," amesema.
Kwa upande wake, msanii wa muziki wa kizazi kipya, Maria Faustine amesema mafunzo hayo yatawasaidia wasanii na washereheshaji kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya fedha, hasa katika sherehe ambako mara nyingi watu hupewa fedha kwa kuwekewa usoni wakati wa kutumbuiza.