Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bei ya kuku yapanda Mwanza, wanunuzi wageukia nyama ya ng'ombe

Wateja wa kuku wakiulizia bei katika soko la Buhongwa jijini Mwanza. Picha na Saada Amir

Muktasari:

  • Bei ya kuku imepanda kutoka Sh20,000 hadi Sh55,000 kulingana na ukubwa, huku baadhi ya wakazi wa jijini Mwanza wakigeukia nyama ya ng'ombe, ambayo bei yake imeshuka baadhi ya maeneo kutoka Sh10,000 hadi Sh9,000 kwa kilo.

Mwanza. Bei ya kuku jijini Mwanza imepanda kutoka Sh20,000 hadi Sh55,000 kulingana na ukubwa.

Uchunguzi wa Mwananchi katika soko la Buhongwa, Mkuyuni wilayani Nyamagana na soko la Mbogamboga lililopo wilayani Ilemela, umebaini kuwa jogoo aliyekuwa akiuzwa Sh30,000 sasa anauzwa kuanzia Sh45,000 hadi Sh55,000, huku kuku tetea akiuzwa kati ya Sh25,000 hadi Sh30,000 badala ya Sh20,000, bei ya kabla ya sikukuu.

Wanunuzi wa kitoweo hicho wamesema imekuwa tabia ya wafanyabiashara wa kuku kupandisha bei wakati wa sikukuu kwa kuwa wanajua walaji hawana namna nyingine na watanunua kwa bei yoyote.

"Wanajua sikukuu sisi watu wa maisha ya kawaida lazima tununue kuku, hivyo ndiyo maana wanapandisha bei. Nimenunua kuku Sh25,000 lakini juzi nilipita kuulizia nikaambiwa Sh20,000, hivyo Sh5,000 nzima imepandishwa," amesema Amina Shabani, mkazi wa Mkolani.

Mkazi wa Mkuyuni, Ashura Salehe amesema amenunua jogoo kwa Sh45,000 baada ya kuomba apunguziwe kwa kuwa bei ya kwanza aliyotajiwa ilikuwa Sh50,000.

"Sikuwa na namna, maana nimeondoka nyumbani watoto wanajua leo wanakula kuku. Nimezunguka vibanda vitatu vyote bei ileile, cha kwanza walianza kuniambia wanauza Sh55,000, mwisho Sh50,000 nikashindwa, wa pili hivyo hivyo, huyu watatu kanipunguzia hadi Sh45,000, imebidi nichukue kwa hiyo hela," amesema.

Muuzaji wa kuku aliyejitambulisha kwa jina moja la Kulwa katika soko la Buhongwa amesema wanalazimika kuuza bei hiyo kutokana na gharama za usafirishaji na ununuzi kutoka vijijini.

Baadhi ya wateja walioshindwa bei hiyo wamegeukia nyama, ambapo baadhi ya bucha imeshusha bei kutoka Sh10,000 hadi Sh9,000 kwa kilo moja.

"Nimeona kuku ghali sana, imebidi nije kununua nyama. Nina watoto sita... kuku mdogo tu wa kawaida anauzwa Sh25,000 hadi Sh30,000, nimeshindwa, bora ninunue nyama ambayo nina uhakika familia yangu itatosheka," amesema Aziza Idrissa.

Mbali na kuku, bei ya mchele nayo baadhi ya maeneo imepanda kutoka kati ya Sh2,000 hadi Sh2,500 siku tatu zilizopita na leo imefikia kati ya Sh2,400 hadi Sh2,700 kulingana na ubora.