Prime
Bado hakijaeleweka ongezeko la gharama mizigo ya meli

Muktasari:
Serikali imekiri kuwepo kwa ongezeko la bei za usafirishaji wa mizigo kwa meli zinazotoka nje ya nchi, ikisema imeweka mikakati ya kupunguza bei hiyo kwa mlaji wa mwisho ikiwa pamoja na kuzungumza na TRA katika utozaji wa mizigo inayoingia nchini.
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiahidi kulitafutia ufumbuzi ongezeko la gharama za usafirishaji wa mizigo kutoka nchi za Ulaya na Asia kwa njia ya meli, baadhi ya kampuni za usafirishaji zimesema bado hawajapata mwafaka.
Ongezeko hilo la gharama za usafirishaji limetajwa kusababishwa na hali ya usalama katika eneo la Suez Canal ambako kunatajwa kuwa na uharamia, hivyo meli kutoka Asia zimekuwa zikichukua safari ndefu kupitia Afrika Kusini na hivyo kuongeza gharama za usafirishaji.
Pia kuna uhaba wa meli, kwani meli nyingi sasa zinapeleka mizigo Ulaya, badala ya kwenda Afrika, huku pia kukiwa na uhaba wa makontena ya kubebea mizigo.
Kutokana na ongezeko hilo, Watanzania wanatarajiwa kupata maumivu ya kuongezeka kwa bei za bidhaa zikiwamo za mavazi kama nguo za aina tofauti, mabegi, pochi na viatu.
Pia kuna vipuri vya magari kama matairi, vifaa vya ujenzi vikiwamo vigae, makufuli, vitasa na aluminiamu na bidhaa za kiofisi yakiwamo makaratasi.
Kutokana na hofu hiyo, jana Jumanne, Mei 21, 2024 akizungumza na kituo cha habari cha Clouds TV jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara amesema wamekubaliana na wadau wa usafirishaji na taasisi za Serikali mambo ya kufanya kwa muda mfupi ili kutafuta suluhu.
“Moja wapo ni kuhakikisha kwamba tunatumia fursa tulizonazo kwa mfano kampuni zinazoweza kusaidia meli zitakazounganisha ile mizigo na kuja upande wa Tanzania.
“Niwatoe wasiwasi Watanzania, kwamba ni kweli bei zimeongezeka, lakini tutahakikisha kwamba haziathiri bei za mlaji. Tulikuwa na wenzetu wa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), tutaangalia namna kodi zinazokadiriwa zisije zikafuata bei inayoongezeka kwa haraka,” amesema.
Amesema pia wameweka mkakati wa kuongeza kasi ya kuondoa mizigo bandarini, ili kupunguza gharama za uendeshaji.
“Tatu ni kuhakikisha tunaongeza miundombinu ya kutoa mizigo bandarini kwenda huko inakokwenda, walikuwepo wawekezaji waliotuonyesha vifaa vingi vinavyofungwa hivi sasa bandarini, ambapo ndani ya wiki ijayo baadhi vitaanza kutumika ambavyo vina uwezo mkubwa wa kutoa mizigo kwenye meli,” alisema.
Mambo bado
Wakati Serikali ikisema hayo, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo (JWK), Martin Mbwana akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, amesema bado suluhisho halijapatikana licha ya vikao walivyofanya na Serikali.
“Bado hawajatoa mwarobaini wa tatizo, kwa sababu kilichosababisha kupanda kwa bei ya kasha moja ni gharama na uhaba wa makontena na uhaba wa meli.
“Kwa hiyo pomoja na kwamba TRA wanaangalia ile bei isiwe kubwa, lakini lazima tujue kwamba mizigo imekwama China na meli zimekuwa chache,” amesema.
Amesema walitegemea wangepata ufumbuzi wa kudumu kama wangeunganisha nguvu na Kenya kubeba mizigo kwa pamoja.
“Ikiwa Serikali ya Kenya ikiweka nguvu kwenye kupakia, biashara itahamia kwao. Kampuni za meli kama Maersk, TIL, Costal ni kampuni binafsi, hivyo tuangalie tutaunganisha meli kubeba mizigo ya Afrika Mashariki.
“Meli kubwa inatoka kule inakuja kushusha Singapore ingawa kwenye meli ndogo ndogo kama Durban, Mombasa, Dar es Salaam na kwingineko. Kwa hiyo tutafute meli yetu tubebe mizigo yetu, hapo itakuwa angalau tumepata suluhisho la muda fulani,” amesema.
Kwa upande mwingine kampuni ya Mo Cargo iliyotangaza ongezeko la bei wiki iliyopita kwa wateja wake wanaosafirisha mizigo kutoka China na Dubai kuja Dar es Salaam, imesema mambo bado hayajaeleweka.
Mwakilishi wa kampuni hiyo aliyezungumza na Mwananchi, Mayasa Mpangala amesema chanzo ongezeko la bei ni kuongezeka kwa gharama za usafirishaji hasa kwa nchi za Asia na Ulaya, ambako gharama zimeongezeka karibu asilimia 50.
Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo ya Serikali, Mayasa amesema bado hawajapata maelekezo yoyote ya Serikali kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa.
“Mpaka sasa (leo jioni) hakuna maelekezo yoyote kuhusu suala la bei, kwa sababu tunachokilipa ni muda ambao makontena yametoka nje kuja huku na ndio muda ambao freight (gharama za usafirishaji) zinatakiwa zilipwe. Mpaka sasa hakuna mwafaka wowote, wala mabadiliko yoyote,” amesema.
Kuhusu kodi amesema haiwezi kupungua ghafla, akisema hata kampuni za usafirishaji bado hazijapata bei kamili za kutoza wateja wao.
“Tunajaribu tu kuwapa bei ambazo tunakokotoa kuangalia mteja anahusika vipi na kampuni inanufaika vipi kwa makisio yaliyopo ambayo ni kati ya dola za Marekani 8,000 (Sh20.7 milioni) hadi 10,000 (Sh25.9 milioni) kutoka dola 2,500 (Sh6.4 milioni).
Kampuni nyingine iliyotangaza ongezeko ni Silent Ocean, ikisema bei za usafirishaji mizigo zimebadilika kidogo kuanzia Mei 18, 2024 ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Mwakilishi wa kampuni hiyo aliyezungumza na Mwananchi, Witness Rogasian, amesema bado wanasubiri uongozi wa kampuni hiyo utoe mwelekeo wa bei.
“Bado tunasubiria viongozi wetu watupe gharama ambayo itakuwa nafuu kwa wateja na kwetu sisi. Tukisafirisha mizigo ni lazima tuwe na gharama kamili, ndio maana tunawaomba wateja wetu waendelee kusubiria, tukipata gharama kamili itakuwa rahisi kutambua gharama itakayokuwa rafiki,” amesema na kuongeza:
“Tunasafirisha mizigo kama kawaida, kwa mteja ambaye ana haraka huwa tunamwambia awasiliane na kule mzigo unakotoka moja kwa moja,” amesema.
Mkakati wa TPA
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, amesema msongamano wa meli katika Bandari ya Dar es Salaam hausababishi moja kwa moja gharama hizo, kwani umekuwepo kwa muda mrefu.
“Kitu cha kujua ni kwamba nchi yetu kumekuwa na ongezeko kubwa la biashara ya bandari, kwa sababu kuna shughuli nyingi za kiuchumi zinafanyika na vilevile nchi zinazotuzunguka zimeongeza uzalishaji wa malighafi kama madini na ujue pia tumekuwa na gati zilezile 12 kwa miaka yote,” amesema.
Akifafanua zaidi, Mkurugenzi wa TPA, Plasduce Mbossa amesema kutokana na chagamoto za usalama katika njia ya Suez Canal, hivyo meli nyingi zimeaamua kupitia rasi ya Cape of Good Hope nchini Afrika Kusini.
“Wakati wanapitia Suez Canal walikuwa wanatumia siku 30 kwenda kurudi China kwenda kuchukua mzigo. Sasa muda umeongezeka kwa siku 18 zaidi, kwa hiyo unajua uzalishaji mkubwa wa bidhaa unafanyika zaidi China, Japan na Korea ndio wanasafirisha vitu kwenye maeneo mengine. Sasa kama meli zingekuwa zinakuja kila baada ya mwezi, maana yake anayepokea mzigo anategemea kila mwezi, lakini meli zimeongeza siku 18 zaidi
“Kwa hiyo kilichofanyika sasa, meli zilizokuwa zikileta mzigo kwetu Afrika zinachukuliwa kwenda kubeba mzigo wa Ulaya au Marekani kwa sababu kuna faida zaidi kuliko kubeba mzigo wetu,” alisema.
Amesema wako katika hatua za kuhakikisha wanaongeza idadi ya gati kwa Dar es Salaam na ujenzi wa bandari ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
“Tumeshatangaza zabuni na pia tuko kwenye hatua za juu kabisa za kuongea na wawekezaji, kuna kampuni zimeonyesha nia ya kujenga. Bandari ya Dar es Salaam tunategemea kujenga gati 10 tukianza na mbili, baadaye mbili baadaye sita kulingana na majadiliano tuliyonayo,” amesema.
Pia amesema kuna kazi za operesheni, akiitaja kampuni ya DP World kuwa miongoni mwa mikakati ya kuharakisha upakuaji wa mizigo.
“Kwa hiyo pale ameongeza vifaa, muda si mrefu tunategemea tutawasha mashine zile mbili za kisasa za kushusha makontena ambapo tutapunguza sana muda wa meli kusubiri.”
Mkakati mwingine amesema: “Tumeongea na baadhi ya kampuni za meli ambazo tumesema kama wataleta mzigo kwa bei rahisi watakuwa hawajipangi kwenye foleni kusubiri, zitakuwa zinaingia moja kwa moja, zinashusha mzigo na kuondoka.”
Juhudi za kuwapata viongozi wa TRA hazikufanikiwa baada ya simu ya Kamishna Mkuu, Alphayo Kidata kuita bila kupokelewa.