Usafirishaji kwa njia ya meli, reli utasisimua uchumi wa wengi

Ngollo John
Muktasari:
- Hii ni baada ya miaka kumi kupita tangu huduma hiyo ilipositishwa Agosti 21, mwaka 2009 kutokana na sababu kadhaa, ikiwemo ya kipande cha kilometa tisa cha reli kati ya eneo la Port Bell-Kampala nchini Uganda kuharibika.
Huduma ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli na meli kutoka Dar es Salaam kwenda nchini Uganda imerejea kuanzia Juni 24, mwaka huu baada ya nchi hizo mbili kufanya marekebisho ya miundombinu iliyokuwa imelala muda mrefu.
Hii ni baada ya miaka kumi kupita tangu huduma hiyo ilipositishwa Agosti 21, mwaka 2009 kutokana na sababu kadhaa, ikiwemo ya kipande cha kilometa tisa cha reli kati ya eneo la Port Bell-Kampala nchini Uganda kuharibika.
Hatua ya kurejesha usafiri huo ilifikiwa baada ya marais John Magufuli na Yoweri Mseveni wa Uganda kukubaliana kuondoa vikwazo vinavyokwamisha ukuaji wa uchumi katika nchi hizo mbili, walipokutana na kufanya mazungumzo Novemba 10, mwaka jana huko Uganda.
Marais hao waliwaagiza mawaziri wanaoshughulikia sekta hizo kukaa pamoja na kuondoa vikwazo vya biashara.
Shehena ya kwanza ya mizigo kutoka Dar es Salaam kwa treni hadi Mwanza na baadaye kwa meli ya MV Umoja hadi nchini Uganda ilianza kusafirishwa Juni 24 mwaka huu katika bandari ya Mwanza kusini. Meli ya Mv Umoja ina uwezo wa kubeba mabehewa 19 sawa na tani 1,200 za mizigo.
Akizungumza katika uzinduzi wa safari hizo, Kaimu Meneja wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) Eric Hamissi anasema makubaliano ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ni kuwa na mkakati wa pamoja ambao utamwezesha mfanyabiashara kufanya biashara kwa tija.
Anasema mizigo inayosafirishwa kutoka Tanzania kufika nchini Uganda wamepanga kutumia siku tano na kuwa siku moja itatumika ndani ya maji na kufika bandarini inatumia siku nne.
Hatua hiyo imefungua fursa za biashara kwa wafanyabiashara wa hapa nchini na nchi jirani kwa kutumia bandari hiyo ambayo ilionekana kusuasua kwa muda mrefu.
Anasema usafirishaji wa majini na reli ndio wenye gharama nafuu ikilinganishwa na usafiri mwingine wowote, hivyo ni wakati sasa kutumia usafiri huo.
Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa anasema tayari kuna tani 12 za mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam zinazosubiriwa kusafirishwa kwa njia ya reli kwenda Uganda huku nyingine 11 zikisubiriwa kuwasili wakati wowote bandarini hapo.
Alisema wakati wakiendelea na matengenezo ya reli mpya ya kati, pia wataiboresha iliyopo iwe inafanya kazi kwa ufanisi lengo ni kutaka kila kitu kirudi na kufanya kazi kama ilivyokuwa awali.
Anasema wanataka kuondoa malalamiko yaliyokuwapo kipindi cha nyuma ya kuchelewesha mizigo bandarini na watahakikisha wanaboresha zaidi utendaji wa shirika hilo.
Anawataka wafanyabiashara kufanya utafiti wa fursa za biashara zinazotakiwa kusafirishwa kwa njia hiyo.
Huduma hiyo si tu itarahisisha usafirishaji bali pia itapunguza gharama na hivyo kuzimua uchumi nchini.
Ni rai yangu kuwa wafanyabiashara wote nchini, hasa wale wanaotumia njia mbalimbali za usafirishaji wakiwamo wa Kanda ya Ziwa kujipanga na kutumia vema fursa hii.
Kwa kutambua umuhimu huo, Mwenyekiti wa wafanyabiashara mkoani Mwanza, Christopher Gachuma anapongeza Serikali kwa kufufua safari na usafishaji wa mizigo kwa njia ya reli akisema utapunguza gharama ya kufanya biashara na hatimaye bei ya bidhaa kwa walaji itakuwa chini.
Pongezi pekee hazitoshi, bali anawataka wafanyabiashara hao sasa watumie kikamilifu fursa hiyo kukuza biashara zao na uchumi wa Taifa.
Kupanuka kwa biashara siyo tu kutaongeza kipato na kukuza uchumi, bali pia kutaongeza fursa za ajira rasmi na zisizo rasmi kwa vijana kupitia shughuli mbalimbali za huduma, biashara na uwekezaji wa kati na mdogo.
Uongozi wa mkoa wa Mwanza nao utekeleze kwa kasi mchakato wa kujengwa kwa bandari kavu ya kuhifadhi mizigo katika eneo la zaidi ekari 1,500 lililotengwa katika Kijiji cha Fela wilayani Misungwi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, kazi hiyo inatarajiwa kuanza mara moja baada ya wananchi ambao maeneo yao yanaingizwa kwenye mradi huo kulipwa fidia.
Ili kwenda na kasi ya maendeleo na kukua kwa biashara, ni vema ulipaji wa fidia uharakishwe kuruhusu mradi kuanza.
0757 708 277