ADC yaishauri Serikali sakata kupaa bei ya mafuta
Muktasari:
- Imeelezwa kuwa tozo na kodi kwenye mafuta zikipunguzwa zitapunguza mzigo kwa mlaji wa mwisho ambaye ni mwananchi.
Dar es Salaam. Chama cha ADC kimeibuka na ushauri kwa Serikali kikisema bei ya mafuta isingepanda hadi pale akiba ya miezi mitatu iliyopo iishe kwanza.
Chama hicho kimesema Serikali uchukue hatua ya kupunguza tozo na kodi zilizopo kwenye mafuta ili kuwezesha upatikanaji na bei nafuu na kuepusha athari za kiuchumi kwa wananchi.
Ushauri huo unakuja ikiwa ni siku moja tangu Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya za mafuta ambazo zimepanda.
Hata hivyo, kupanda kwa bei hizo kwa mujibu wa Ewura kunatokana na mabadiliko ya soko la kimataifa, likiwemo ongezeko la bei ya mafuta ghafi na changamoto za usafirishaji.
Aidha, hali ya kisiasa na kiusalama duniani, hususan mvutano unaoendelea Mashariki ya Kati, imechangia kuvuruga upatikanaji na usambazaji wa mafuta katika masoko ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Ewura, gharama za uagizaji na usafirishaji zimeongezeka, zikichangiwa pia na kupanda kwa gharama za bima ya meli pamoja na ucheleweshaji wa mizigo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, leo Aprili 2, 2026 baada ya kikao cha Kamati Tendaji cha chama hicho kujadili hali hiyo sambamba na mwelekeo wa chama Mwenyekiti wake taifa, Shabani Itutu amesema kupanda kwa bei ya mafuta kunaleta hali ya hatari katika sekta za afya, kilimo, usafirishaji ambapo inagusa moja kwa moja maisha ya Watanzania.
Itutu, amesema ongezeko la bei ya mafuta limeathiri moja kwa moja gharama za usafiri pamoja na bei za bidhaa muhimu, hali inayowaumiza wananchi wa kipato cha chini.
Amesema kuna umuhimu kwa Serikali kuingilia kati kwa kupunguza baadhi ya tozo na kodi kwenye mafuta ili kurejesha unafuu wa bei na kulinda ustawi wa wananchi.
Amesisitiza hatua hiyo itasaidia kupunguza mfumuko wa bei na kuwezesha shughuli za kiuchumi kuendelea kwa ufanisi.
Katika kikao hicho, ADC imejadili masuala mbalimbali ya chama ikiwemo tathmini ya chaguzi ndogo zilizopita katika majimbo na kata mbalimbali.
Chama hicho kimeeleza kuwa kitaendelea kushauri Serikali juu ya masuala ya kiuchumi yanayogusa maisha ya wananchi, hususan katika kipindi hiki ambacho gharama za maisha zimekuwa zikiongezeka.