Suala la mafuta hatuna namna tufuate njia hii
Katika miezi ya karibuni, dunia imeendelea kushuhudia kupanda kwa bei ya mafuta kwa kasi inayotia wasiwasi. Sababu ni nyingi migogoro ya kisiasa, mabadiliko ya uzalishaji, pamoja na kuyumba kwa uchumi wa kimataifa.
Tanzania ambayo si mzalishaji wa mafuta, athari zake zimeanza kuonekana wazi: baada ya bei ya mafuta kupanda kwa karibu Sh1000 kwa lita moja ikilinganishwa na mwezi uliopita jambo ambalo linaweza kuibua kupanda kwa bei za bidhaa hivyo kuongeza mzigo mkubwa kwa wananchi wa kawaida.
Hali hii inapaswa kuwa kengele ya tahadhari. Ni wazi kuwa utegemezi wa mafuta ya petroli na dizeli ambayo hayazalishwi hapa nchini unaweka uchumi wetu katika hatari kubwa. Kadiri bei zinavyopanda, ndivyo tunavyozidi kupoteza fedha za kigeni na kuongeza presha kwa maisha ya kila siku ya Watanzania.
Suluhisho la kudumu halipo mbali. Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zilizobarikiwa kuwa na akiba kubwa ya gesi asilia, inayokadiriwa kufikia futi za ujazo trilioni 57. Hii ni rasilimali ambayo, ikiwa itatumika ipasavyo, inaweza kubadili kabisa mwelekeo wa nishati nchini hasa katika sekta ya usafiri.
Matumizi ya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) katika magari ni moja ya hatua muhimu zinazopaswa kupewa kipaumbele. CNG ni nafuu zaidi ikilinganishwa na petroli au dizeli, na pia ni rafiki kwa mazingira. Katika nchi nyingi, magari yanayotumia gesi yamekuwa mbadala halisi wa mafuta, yakipunguza gharama za uendeshaji na utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.
Hata hivyo, changamoto kubwa ipo katika gharama za awali za kubadilisha mifumo ya magari kutoka mafuta kwenda gesi. Hapa ndipo jukumu la Serikali linapokuwa muhimu zaidi.
Kuweka ruzuku au motisha maalum kwa wananchi na sekta binafsi kubadili mifumo ya magari yao kwenda CNG kutakuwa hatua ya kimkakati. Bila msaada huo, wananchi wengi wataendelea kushindwa kumudu gharama za awali, licha ya faida za muda mrefu.
Zaidi ya hapo, Serikali inapaswa kuharakisha uwekezaji katika miundombinu ya vituo vya kujaza gesi (CNG stations) ili kuhakikisha upatikanaji wake unakuwa rahisi na wa uhakika. Bila miundombinu ya kutosha, hata jitihada za kubadili magari zitakwama.
Lakini hoja ya nishati mbadala haiishii kwenye usafiri pekee. Sekta ya nishati ya kupikia nayo iko hatarini. Kupanda kwa bei ya mafuta duniani mara nyingi huathiri pia bei ya gesi ya kupikia (LPG), kwa kuwa nayo ni bidhaa ya mafuta na haizalishwi hapa isipokuwa huagizwa kutoka nje. Hali hii inaweza kurudisha nyuma juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi majumbani.
Nafahamu tunao mradi mkubwa LNG ambao umekuwa ukizungumzwa sana lakini nafikiri ni wakati sasa kuanza kutekeleza miradi midogo ya LNG wakati mkubwa ukisubiriwa. Miradi midogo ya kusindika na kujaza gesi kwenye mitungi inaweza kuongeza upatikanaji wa nishati ya kupikia kwa gharama nafuu zaidi na kupunguza utegemezi wa LPG ya kuagiza.
Hatua hii pia itachochea ajira, kukuza viwanda vidogo na vya kati, na kuongeza thamani ya rasilimali iliyopo nchini. Ni njia ya haraka na yenye matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi wa kawaida.
Kwa mtazamo mpana, matarajio ya kushuka kwa bei ya mafuta katika siku za karibuni si ya uhakika. Mwelekeo wa soko la dunia unaonyesha kuwa bei zinaweza kuendelea kuwa juu au hata kupanda zaidi, hasa kutokana na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi yanayoendelea.
Wachambuzi wanasema hata vita vya Israeli, Marekani na Iran vikikoma itachukua karibu miaka 5 kurejesha hali ya mafuta katika hali ya kawaida.
Mbaya zaidi, kuna hatari ya kuvurugika kwa minyororo ya usambazaji, hali ambayo inaweza kusababisha upungufu wa mafuta sokoni. Hapo ndipo changamoto itakapokuwa kubwa zaidi sio bei tu, bali upatikanaji wenyewe.
Hivyo Tanzania haina budi kuchukua hatua sasa. Kuendelea kutegemea mafuta ni kuendelea kujifunga kwenye mzunguko wa hatari. Uwekezaji katika gesi asilia, umeme na nishati nyingine mbadala si suala la uchaguzi tena, bali ni lazima kwa ustawi wa uchumi na ustahimilivu wa taifa.
Kwa wananchi, huu ni wakati wa kuanza kufikiria mabadiliko iwe ni kubadili magari, kuwekeza katika teknolojia mbadala au kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya mafuta. Kwa Serikali, huu ni wakati wa kuweka sera na motisha zitakazoharakisha mabadiliko hayo.
Kwa kufanya hivyo, Tanzania inaweza kupunguza utegemezi wa mafuta kutoka nje, kulinda uchumi wake, na wakati huo huo kujenga mustakabali wa nishati ulio salama, nafuu na endelevu.
Ephrahim Bahemu ni Mhariri wa uchumi na biashara gazeti la Mwananchi anapatikana kwa namba 0756939401