Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watanzania watakiwa kuvitembelea vivutio vya utalii

Muktasari:

  • Licha ya uwepo wa vivutio vingi vya utalii nchini bado idadi ya Watanzaninia wanaofanya utalii kwenye vivutio hivyo ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya watalii wanaotoka nje ya nchi

Musoma. Watanzania wametakiwa kufurahia uwepo wa vivutio vya kitalii nchini vinavyotambulika kimataifa  ambapo pamoja na mambo mengine wametakiwa kuwa na mwamko wa kuongeza kasi ya kuvitembelea vivutio hivyo ili kuwavutia zaidi watalii kutoka nje ya nchi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Rorya Juma Chikoka kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara ,Evans Mtambi leo Agosti 19,20,2024 alipokuwa akizungumza na washiriki wa shindano la kumtafuta mrembo wa kanda ya ziwa atakayewakilisha kanda hiyo kwenye mashindano ya taifa yatakayofanyika baadaye mwaka huu.

                     

Baadhi ya washiriki wa shindano la kumtafuta mrembo wa Tanzania kanda ya ziwa  wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Rorya  Juma Chikoka (hayupo pichani) walipofanya ziara mkoani Mara. Picha na Beldina Nyakeke

Chikoka amesema licha ya uwepo wa vivutio hivyo bado idadi ya Watanzania wanaofanya utalii kwenye vivutio hivyo ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya watalii  wanaotoka nje ya nchi hivyo ni vema Watanzania wakaona umuhimu wa uwepo wa vivutio hivyo na kuvitembelea ili kuvutia zaidi watalii kutoka nje.

"Ingawa sina namba kamili kwasasa lakini takwimu zinaonyesha kuwa Watanzania wanaotembelea vivutio vyetu ni ndogo sana, watalii wengi wanatoka nje ya nchi hebu tuhamasike kutembelea vivutio vyetu na kwa kufanya hivyo mbali na kuongeza pato la taifa lakini pia tutakuwa mabalozi wazuri wa kutangaza vivutio hivyo na kuweza kuwavutia wageni zaidi," amesema.

Ametolea mfano wa hifadhi ya taifa ya Serengeti ambayo kwa miaka zaidi ya mitatu mfululizo imekuwa hifadhi bora Afrika jambo ambalo linapaswa kutumiwa na Watanzania kwa kuongeza kasi ya kutembelea hifadhi hiyo ili kushuhudia uzuri wake na maajabu yaliyomo.

"Mkuu wa Mkoa ameamua kuwaalika washiriki hawa kuja kutembelea vivutio vya mkoa wetu ikiwemo hifadhi ya Serengeti ambayo asilimia 75 iko mkoani Mara niwaombe washiriki hawa kuwa mabalozi wazuri, tuwatangazie Watanzania mambo mazuri kama haya ili waje wajionee wenyewe,"ameongeza. 

Amesema mbali na kuongeza idadi ya watalii, lakini hali hiyo pia itasaidia kuwavutia wawekezaji wengi kutoka ndani na nje ya mkoa kuja kuwekeza mkoani humo kwa maelezo kuwa mkoa unazo fursa nyingi katika sekta za utalii, kilimo, madini, uvuvi na mifugo.

Muandaaji wa mashindano ya urembo Kanda ya Ziwa, Rosemary Range amesema lengo la washiriki hao kufanya ziara mkoani Mara kupitia mwaliko wa mkuu wa mkoa huo ni kutaka kuungana na Rais Samia  Suluhu katika kuutangaza utalii wa Tanzania.

"Tunataka kutumia mashindano hayo kutangaza utalii wetu kama ambavyo alianza Rais wetu na kama mnavyojua kanda ya ziwa imebarikiwa kuwa na vivutio vingi na baada tu ya kupokea mwaliko wa mkuu wa mkoa huu hatukusita tulikubali mara moja kwani tunalo jukumu katika hili," amesema

Baadhi ya washiriki wa mashindano hayo wamesema mkoa wa Mara una fursa nyingi za kiuchumi katika sekta za utalii, madini, uvuvi, mifugo na nyingine nyingi hivyo ni vema fursa hizo zikatumika vema kukuza uchumi wa wakazi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla. 

"Tumeambiwa Watanzania wengi bado hawajawa na utamaduni wa kutembelea hifadhi zetu hasa ya Serengeti licha ya hifadhi hii kuwa bora duniani, nadhani inatokana na kutokuwa na taarifa zaidi niombe kila mmoja kwa nafasi yake atoe elimu kwa wananchi hii itasaidia kuongeza mwamko wa Watanzania kufanya utalii kwenye hifadhi zetu," amesema Veronica Patrick.