Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vikumbo vya mastaa Bongo Fleva tuzo TMA

Muktasari:

  • Misimu mitatu tangu kurejea tena kwa TMA imekuwa ya neema na mafanikio kwa wasanii pamoja na tasnia kwa ujumla lakini bado kuna changamoto ambazo zinahitajika kufanyiwa kazi na waandaaji.

Dar es Salaam. Baada ya kusimama tangu mwaka 2015, hatimaye Tuzo za Muziki Tanzania zilirejea tena 2022 na kuanza kuwatunza wasanii waliofanya vizuri 2021, huku hadi sasa Zuchu akiwa ndiye msanii aliyefanya vizuri zaidi akibeba tuzo saba.

                       

Misimu mitatu tangu kurejea tena kwa TMA imekuwa ya neema na mafanikio kwa wasanii pamoja na tasnia kwa ujumla lakini bado kuna changamoto ambazo zinahitajika kufanyiwa kazi na waandaaji.

Tuzo hizi zilianzishwa mwaka 1999 na Baraza la Sanaa Taifa (Basata) chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, 2003 zilipata mdhamini na kujulikana kama Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) hadi ziliposimama 2015.

Kufuatia kukosekana kwa miaka saba, serikali ikaamua kubeba jukumu hilo huku kila msimu kukiwa na mabadiliko katika uandaaji, uwasilishaji na hata muonekano wa tuzo zenyewe. Je, mambo yapo vipi hasa?.


1. Waliofaya Vizuri 2021 - 2023

Katika misimu hii mitatu ya TMA kuna wasanii waliofanya vizuri zaidi, wapo wenye rekodi ya kushinda tuzo nyingi kwa msimu mmoja kama ambavyo imeonyeshwa katika kipengele A, B, C, huku kipengele D kikigusia wale wenye jumla ya tuzo nyingi kwa misimu yote.


A. Alikiba - Tuzo Sita

Staa wa Bongo fleva, Alikiba ndiye msanii aliyeng'aa zaidi msimu wa 2021 akishinda tuzo tano sawa na mwaka 2015, ushindi huo ulikuja baada ya kufanya vizuri na albamu yake ya tatu, Only One King (2021) iliyotoka na nyimbo 16.
Alikiba kutokea Kings Music alishinda kama Mtunzi Bora wa Melodi, Albamu Bora (Only One King), Msanii Bora wa Kiume Chaguo la Watu Kidijitali, Msanii Bora Afrika Mashariki na Video Bora ya Mwaka (Salute).

Msimu uliofuatia hakushinda na msimu uliopita wa 2023 ambao ulifanyika Oktoba 19 mwaka huu, alishinda tuzo moja ya Wimbo Bora wa Bongo fleva (Mahaba), hivyo kufikisha tuzo sita za TMA katika misimu hii mitatu ila kwa ujumla hiyo ni tuzo ya 18.


B. Zuchu - Tuzo Saba


Mwimbaji huyu wa WCB Wasafi msimu wa 2021 hakushiriki kutokana na msimamo wa lebo yake ila 2022 alijitosa na kushinda tuzo tano sawa na Alikiba mwaka 2021 na hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Zuchu kuwania TMA na kushinda.

Zuchu alishinda TMA 2022 kama Msanii Bora wa Kike wa Mwaka, Video Bora ya Mwaka (Mwambieni), Msanii Bora wa Kike Bongofleva, Wimbo Bora wa Bongo fleva (Kwikwi) na Mwanamuziki Bora wa Kike Chaguo la Watu Kidijitali.

Msimu uliopita alishinda tuzo mbili katika vipengele vya Mwimbaji Bora wa Kike Bongofleva na Mtumbuizaji Bora wa Kike, hivyo kufikisha tuzo saba akiwa ndiye msanii mwenye rekodi ya kushinda mara nyingi zaidi tangu kurejea kwa TMA 2021.


C. Diamond - Tuzo Tano

Naye Diamond Platnumz, Mkurugenzi Mtendaji wa WCB Wasafi, msimu wa 2021 hakushiriki, 2022 akashinda kipengele cha Msanii Bora wa Kiume Chaguo la Watu Kidijitali licha ya kusema hakuwasilisha kazi zake ili kupata uteuzi.

Msimu wa 2023 Diamond akashinda tuzo nne ambazo ni Mtumbuizaji Bora wa Mwaka, Video Bora ya Mwaka (Achii ft. Koffi Olomide), Wimbo Bora wa Dansi (Achii ft. Koffi Olomide) na Msanii Bora wa Kiume wa Mwaka.

Hivyo kufikisha tuzo tano kwa misimu hii miwili aliyoshiriki ila kwa ujumla Diamond ameshinda tuzo 22 za TMA akiwa ndiye msanii aliyeshinda mara nyingi zaidi kwa muda wote akifuatiwa na mshindani wake wa miaka mingi, Alikiba mwenye tuzo 18.


D. Harmonize (6), Nandy (4), Phina (4), Young Lunya (4) & Marioo (4)

Staa wa Konde Music Worldwide, Harmonize msimu wa 2021 alishinda tuzo tatu, msimu wa 2022 tuzo moja na msimu wa 2023 tuzo mbili, jumla ana tuzo sita sawa na Alikiba na juu ya Diamond ila yeye ameshindwa kufikisha walau tuzo nne kwa msimu mmoja.

Kwa upande wake Nandy msimu wa 2021 alishinda tuzo tatu, msimu wa 2022 akakosa na msimu wa 2023 akashinda moja na kumfanya kufikisha tuzo nne sawa na Phina aliyeshinda mbili 2021 na mbili nyingine 2022 ila 2023 hakuambulia kitu.

Naye Young Lunya alishinda tuzo mbili 2021 sawa na Marioo ila msimu uliofuatia wote walikosa, walikuja kuibuka tena msimu wa 2023 na kila mmoja kushinda tuzo mbili, hivyo nao kufikisha nne sawa na Nandy na Phina, mshindi wa BSS 2018.


2. Ushindi wa Kwanza

Miaka saba ya kutofanyika TMA kuna wasanii, watayarishaji na waongozaji video walioibuka katika kipindi hicho na hawakuwahi kuonja ladha ya tuzo kama wale waliokuwepo tangu 2015 kushuka chini, ila 2021 walikuwepo na kushinda kwa mara ya kwanza.


                        

Baadhi ya hao ni Zuchu, Harmonize, Nandy, Phina, Marioo, Young Lunya, Rapcha, Mbosso, Rayvanny, Gachi, Rosa Ree, Chino Kidd, Baddest 47, Jay Melody, Billnass, Appy, Dipper Rato, Kontawa, Abbah, S2kizzy, Mr. T Touch, Ringle Beat, Fole X n.k.

"Binafsi najivunia na imenipa nguvu ya kuendelea kupambana zaidi. Nimegundua unapofanya kazi kwa kabidi unaweza kupata vitu ambavyo vinakufanya ufurahie kazi yako," anasema Kontawa, mshindi wa TMA 2022 kama Msanii Bora wa Kiume Chipukizi.

Ikumbukwe hadi 2015 kuna vipengele havikuwepo TMA ila 2021 vikaanzishwa, mathalani muziki wa Singeli ambao umetoa washindi kama Sholo Mwamba, Mimah, Snura, Dulla Makabila na Kenny Touch kama Mtayarishaji Bora.

Vipengele vingine vipya kwa wasanii wa ndani na baadhi ya washidi wake ni Meneja Bora (D Fighter), Dansa Bora (Baby Drama, Angel Nyigu, Chino Kidd), Muigizaji Bora wa Video za Muziki (Fevushka, Seleman Masenga), DJ Bora (Ally B, DJ Mammy) n.k.


3. Changamoto, Pongezi na Maoni

Kama ambavyo kuna baadhi ya vipengele vimeongezwa katika TMA, pia kuna ambavyo vimeondolewa, mfano kile cha Kundi Bora la Mwaka ambacho kilikuwepo hapo awali na kutoa washindi kama Jambo Squad (2013), Weusi (2014) na Yamoto Band (2015).

                      

Kundi la Mabantu ambalo limefanya vizuri miaka ya hivi karibuni lakini hawajapata nafasi ya kushinda TMA, limesema kuondolewa kwa kipengele hicho sio kwamba ni makundi ni machache ila yanayosikika kwa sasa ndio machache, hivyo yapewe nafasi.  

"Kama tunataka kuwa na makundi mengi inabidi hamasa iwepo kama kukirudisha hicho kipengele cha Kundi Bora katika tuzo ilimradi kuyapa motisha makundi mengine kama kweli tunayahitaji makundi katika hii tasnia," wamesema Mabantu.

Naye Angel Nyigu, dansa aliyefanya kazi na wasanii kama Vanessa Mdee, Harmonize, Rayvanny, Mimi Mars, Rosa Ree, Diamond, Zuchu n.k, amepongeza TMA kuweka kipengele chao kwa misimu ya miwili mfululizo ingawa wa 2023 hakikuwepo!.

"Binafsi kila nikishinda tuzo naona kabisa siku hizi dansi inaheshimika na ndio sababu tunawekwa kwenye tuzo kubwa kama TMA, hii inayonyesha ni jinsi gani wanaheshimu kile tunachofanya," anasema Angel, mshindi wa TMA 2022 kama Dansa Bora wa Kike.

Mtayarishaji muziki kutoka MJ Records, Master J amesema dijitali pia inapaswa kupewa nafasi katika kutoa maamuzi ya kuwapata washindi katika vipengele ambavyo havihitaji utaalamu.

"Lazima tuiangalie dijitali kwa sababu ya mauzo ya streams, huwezi kununua streams, tena dijitali ndio inaturahisishia kama kuna vipengele unaweza kwenda huko, mfano Wimbo Bora wa Mwaka, Msanii Bora wa Mwaka, ukiangalia streams ni rahisi kujua kuliko kusikiliza" amesema.  

Ikumbukwe msimu uliopita Jux alilalamika kuwa wimbo wake, Enjoy (2023) akimshirikisha Diamond alistahili kupata nafasi nyingi katika TMA 2023 kutokana na mafaniko yake ikiwemo video yake kutazamwa (views) YouTube zaidi ya mara milioni 100.

                       

Ila wimbo huo uliambulia kipengele kimoja cha Wimbo Bora wa Kushirikiana na kushinda, lakini Jux alisema ulistahili kuwania Video Bora, Wimbo Bora wa Bongo fleva, Msanii Bora wa Bongo fleva, Msanii Bora wa Kiume, Mtunzi Bora na Mtumbuizaji Bora.

Hata hivyo, 2 Percent mwenye rekodi ya kushinda tuzo tano za TMA kwa usiku mmoja, amesema tuzo ni kwa ajili ya wasanii wote na sio wa wanaofanya vizuri mtandaoni kwani hata wanaofuatilia muziki sio wote wapo mitandaoni.

"Wanajua kabisa wao sio wanamuziki kwenye jamii bali ni wa mtandaoni kutokana wanaishi kwa matukio ya huko, nachoweza kusema hizo tuzo zinawahusu wanamuziki wa Tanzania ambao muziki wao upo kwenye jamii au una mchango kwenye jamii," amesema.

Utakumbuka 20 Percent aliyetoka kimuziki na wimbo wake, Money Money (2005) uliobeba jina la albamu yake ya kwanza, mwaka 2011 alishinda tuzo tano za TMA kwa mpigo sawa na Alikiba 2015, 2021 na Zuchu 2022, huku Diamond akiondoka na saba 2014.