Soulja Boy amkingia kifua Jay Z

Muktasari:
- Soulja Boy amedai kuwa tuhuma za aina hiyo zinawalenga watu maarufu katika rap kwa kile alichoita ni wivu wa kuona wamefanikiwa kimaisha kwa kumiliki fedha nyingi kitu kinachowachukiza baadhi ya watu
Marekani. Rapa wa Marekani, Soulja Boy amemkingia kifua mwanamuziki mwenzake, Jay Z dhidi ya tuhuma za ubakaji kwa binti wa miaka 13, kosa analodaiwa kulifanya mwaka 2000 akiwa na Diddy ambaye yupo gerezani kwa tuhuma sawa na hizo.
Soulja Boy amedai kuwa tuhuma za aina hiyo zinawalenga watu maarufu katika rap kwa kile alichoita ni wivu wa kuona wamefanikiwa kimaisha kwa kumiliki fedha nyingi kitu kinachowachukiza baadhi ya watu.
Hivi karibuni kesi hiyo ambayo ilifunguliwa Oktoba 2024 ikimtaja Diddy kama mshtakiwa namba moja, imewasilishwa tena mbele ya mahakama na jina la Jay Z kujumuishwa ingawa rapa huyo na baba wa watoto watatu amekanusha madai hayo.
Msichana huyo mwenye umri wa miaka 37 kwa sasa, kupitia Wakili wake, Tony Buzbee anadai kuwa wasanii hao walimfanyia ukatili huo mara baada ya kumalizika hafla ya ugawaji wa tuzo za MTV VMAs 2000.
Akizungumza kupitia Instagram, Soulja Boy amekosoa kile anachoona kama jitihada za kuharibu alama iliyowekwa kwa umma na watu maarufu wa rap na kusema hayupo tayari kuona anarudishwa nyuma kwa mambo kama hayo.
"Ukiwa katika hii tasnia na kusimama kama biashara wataanza kuchafua jina lako, watajaribu kukushusha, hawataki kuona tunashinda na hawataki kuona tuna hizi fedha. Unapokuwa katika tasnia hii ya rap na kuwa mtu mashuhuri, utalengwa tu," alisema.
Soulja Boy sio rapa pekee ambaye hakubaliana na tuhuma dhidi ya Jay Z, kuna Meek Mill ambaye muda mfupi baada ya hati hiyo ya mashtaka kusambaa mtandaoni, alitumia ukurasa wake wa X kusema ni tuhuma zinazolenga kupotosha.
Meek Mill alidai habari hiyo ni ya uongo na kwamba vyombo vya habari vya Marekani sio vya kuviamini kabisa kwa jinsi vilivyoipa nafasi kubwa habari anayodai ina nia ovu ya kumchafua Jay Z, mshindi wa Grammy 24.
Kwa mujibu wa NBC News, Wakili Tony Buzbee aliwasilisha kesi hiyo mwishoni mwa wiki na kuongeza jina la Shawn Carter 'Jay Z' baada ya hapo awali jina lake kundolewa kwenye kesi na alitajwa tu kama John Doe.
Hata hivyo, Jay Z kupitia chapa yake ya Roc Nation alikanusha madai hayo na kusema yeye sio kama watu wengine maarufu, amekuwa akiwalinda watoto na kuyaita madai hayo ya kipuuzi na yenye lengo la kupata aina fulani ya faida kama fedha.
Utakumbuka Jay Z alifunga ndoa na staa wa Pop, Beyonce Knowles mwaka 2008 ingawa walikuwa pamoja kwenye uhusiano tangu mwishoni mwa miaka ya 1990, tetesi za kuwa pamoja zilianza katika kolabo yao ya kwanza, 03 Bonnie & Clyde (2002).
Miaka 16 ndani ya ndoa, Jay Z na Beyonce wamejaliwa watoto watatu, Blue Ivy Carter (2012) na pacha, Rumi na Sir Carter (2017), huku wakiwa wanandoa mastaa walioingiza fedha nyingi zaidi duniani, kwa pamoja utajiri wao unakadiriwa kuzidi Dola3 bilioni.