Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu Blackpassy kuigiza kama mwenye changamoto ya kusikia

Muktasari:

  • Blackpassy anasema alianza safari yake ya uigizaji mwaka 2017. Ambapo alijijenga hatua kwa hatua hadi kufikia umaarufu kupitia mitandao ya kijamii na maonesho mbalimbali ya vichekesho.

Dar es Salaam. Msanii wa vichekesho na uigizaji Pascalia Silanda (Blackpassy) ameendelea kuvutia mashabiki wengi kupitia mtindo wake wa kipekee wa uigizaji unaomfanya aigize kama mtu mwenye changamoto ya kusikia, licha ya kutokuwa na ulemavu huo katika uhalisia.

Blackpassy anasema alianza safari yake ya uigizaji mwaka 2017. Ambapo alijijenga hatua kwa hatua hadi kufikia umaarufu kupitia mitandao ya kijamii na maonesho mbalimbali ya vichekesho.

Akizungumza kuhusu mtindo wake huo, anasema wazo la kuigiza kama kiziwi lilitokana na kutafuta njia ya kujitofautisha katika tasnia ya burudani yenye ushindani mkubwa. Ambapo aliona hakuna msanii mwingine aliyekuwa akifanya aina hiyo ya uigizaji kwa kiwango chake.

Anabainisha kuwa hakufundishwa rasmi bali alijifunza mwenyewe kwa majaribio, na kubadili wazo hilo kuwa fursa ya kisanaa inayomsaidia kujenga chapa yake binafsi.

Hata hivyo, anakiri kuwa mara nyingine hukumbana na changamoto za kijamii, ambapo baadhi ya watu hushindwa kutofautisha kati ya uigizaji na uhalisia wake, na kudhani kuwa ana tatizo la kusikia.

Katika mafanikio yake, Blackpassy anasema mtindo wake umemsaidia kufikisha ujumbe kwa watazamaji kwa ufanisi mkubwa, jambo lililoongeza umaarufu wake siku hadi siku ndani na nje ya Tanzania.

Anasema pia amekuwa akijifunza kutoka kwa watu wenye tatizo la  kusikia ili kuboresha uhalisia wa uigizaji wake, jambo linalomsaidia kufikisha ujumbe wenye zaidi kwa watazamaji.

“Naishi na watu wenye changamoto ya kusikia, kupitia wao najifunza zaidi namna ya kuwasilisha hisia kwa uhalisia,” amesema.

Aidha, anakiri kuwa maigizo ya mapenzi ni miongoni mwa changamoto kwake, akisema wakati mwingine hupata ugumu wa kuonyesha hisia za kimahaba kwa uhalisia unaotakiwa.

“Katika kuigiza, lazima uvae uhusika. Ukishavaa inakuwa rahisi kufikisha ujumbe, lakini kuna jambo kuigiza mapenzi yananipa changamoto kidogo,” amesema.

Blackpassy anasisitiza kuwa siri ya mafanikio yake ni kujitumbukiza kikamilifu kwenye uhusika anaouvaa, jambo linalomsaidia kuwasilisha ujumbe bila kutumia maneno mengi.

Uigizaji wake umechangia pia kubadilisha mtazamo wa wanawake katika tasnia ya vichekesho, ambapo sasa wengi wameanza kujitokeza kutokana na kuhamasishwa na kazi za wasanii kama yeye.

"Kwa sasa wanawake wengi wameanza kuona kuwa inawezekana kufanya vichekesho bila kupoteza heshima yao na wengi wameingia kwenye tasnia hiyo kupitia mitandao ya kijamii", amesema Blackpassy

Kwa vijana wanaotamani kuingia kwenye sanaa, Blackpassy ametoa wito wa kutumia mitandao ya kijamii kama jukwaa la kujitangaza, badala ya kusubiri nafasi kutoka kwa watu.

“Chukua simu yako, jirekodi, weka mtandaoni. Watu wataona na watakuita,” amesema.