Quick Rocka kwenye maisha ya S2Kizzy

Muktasari:
- Kuanzia Komasava ya Diamond, Mapoz (Diamond), Ololufe Mi (Jux), Dah (Nandy), Ova(Mbosso), Kunguru (Mbosso) na nyingine nyingi. Hata hivyo ni ngumu kutaja mafanikio ya S2Kizzy katika kiwanda cha muziki Bongo, bila kuligusia jila la msanii Quick Rocka. Ilianza hivi.
Dar es Salaam. Zikitajwa nyimbo kumi za Bongo zenye mafanikio makubwa, lazima jina la mzalishaji muziki S2Kizzy litajwe. Hii ni kutokana na mkali huyo kuhusika kwenye kutengeneza nyimbo nyingi kali zilizopenya kimataifa.
Kuanzia Komasava ya Diamond, Mapoz (Diamond), Ololufe Mi (Jux), Dah (Nandy), Ova(Mbosso), Kunguru (Mbosso) na nyingine nyingi. Hata hivyo ni ngumu kutaja mafanikio ya S2Kizzy katika kiwanda cha muziki Bongo, bila kuligusia jila la msanii Quick Rocka. Ilianza hivi.

S2Kizzy alianza kutengeneza midundo mara baada ya kumaliza kidato cha nne huko Mbeya. Akawa anaenda internet cafe na kukaa kwenye kompyuta kisha anafanya mazoezi ya kuandaa muziki.
Baadaye alienda Morogoro kwa ajili ya kusoma kidato cha tano na sita. Hivyo kila akipata muda akawa anakuja Dar es Salaam kwenye studio mbalimbali ili kujifunza zaidi na mwisho wa siku akakutana na Country Boy.
S2Kizzy alipotengeneza tu mdundo wa wimbo wa Country Boy, Aah Wapi (2016) ndipo milango ikaanza kufunguka, DJ's waliupenda sana mdundo huo na wakaanza kuomba wautumie katika kazi zao na polepole jina la S2Kizzy likaanza kusambaa.
Punde akakutana na Quick Rocka ambaye alimpa nafasi katika studio yake ya Switch Records na hapo S2Kizzy akafahamiana na wasanii mbalimbali wakubwa wa Bongofleva kama Weusi, Mimi Mars, Vanessa Mdee, Rayvanny n.k na kuandaa kazi zao. Hii ndiyo sababu ya Quick Rocka kuingia kwenye maisha ya S2Kizzy.

Hata hivyo licha ya kuwa miongoni mwa watu waliomsindikiza S2Kizzy katika safari yake ya mafanikio, Quick Rocka anatajwa kama mmoja wa wasanii wenye mchango mkubwa kwenye muziki nchini.
Safari ya Quick Rocka kwenye muziki ilianza mwaka 2009, baada ya kuachia ngoma yake ya kwanza 'Bullet' iliyomtambulisha kwenye ramani ya muziki wa Afrika Mashariki. Wimbo huo uliojizolea umaarufu ulitayarishwa na Marco Chali chini ya studio za MJ Records. Ngoma hiyo ilipigwa sana kwenye vyombo vya habari wakati huo.
Kuachia kazi kali ilikuwa siyo kitu cha kubahatisha kwake kwani amefanikiwa kutoa ngoma kali za muda wote. Mwaka 2013 alidondosha ngoma ya 'My Baby' akiwa kamshirikisha Albert Mangwea 'Ngwair' mwaka huo huo Ngwair alifariki dunia, hawakufanikiwa hata kufanya video ya wimbo huo.
Mwaka uliofuata iliachiwa video ya wimbo huo na sehemu anayosikika Ngwair alifanya Twaah Kane, kijana anayeunda kundi la Mabantu kwa sasa.
My Baby ni moja kati ya nyimbo kali kwenye kiwanda cha muziki wa Bongo Fleva, na video yake ndiyo ilimtambulisha vizuri Hamisa Mobetto, ambaye alicheza kama Video Vixen.
Quick Rocka aliendelea kutoa ngoma kama 'Bishoo' (2017) alikiwa na Ngadu, Young Dee , Bembeleza (2019) akimshirikisha Joh Makini. Hata hivyo, licha ya sasa kuonekana akifanya vizuri kwenye upande wa filamu, bado juhudi zake kwenye muziki zinaendelea. 2021 aliachia Extended Playlist 'Ep' iliyoitwa 'Love Life' ikiwa na nyimbo nne ambazo ni Love Song, Teamo, Ukimya na Kabinti.
Mbali na hayo anamiliki studio yake ya muziki inayofahamika kama Switch Music, ambayo imetengeneza ngoma nyingi kwenye muziki wa Bongo Fleva.

Ukiachilia mbali Quick Rocka kufanya kazi kama msanii anayejitegemea, pia amewahi kusimamia kundi la muziki wa Hip-Hop 'OMG'. Lililokuwa linaundwa na Young Lunya, Salmin Swaggs, Conboi, na Luffa. kundi hilo lilifanikiwa kufanya vizuri kwenye muziki kabla ya kuvunjika na wasanii wa kundi hilo kuanza kujitegemea mwaka 2019.
Kundi la OMG, lilifanikiwa kutoa nyimbo nyingi likiwa chini ya Switch Music ya Quick Rocka. Baadhi ya ngoma walizoachia ni Solo, Uongo na Umbea, Wanangu na Wanao ft Rosa Ree na nyingine nyingi.