P Diddy kizimbani madai ya kudhalilisha, kuwapiga wanawake

Sean "Diddy" Combs amefikishwa mahakamani leo Jumanne Septemba 17, 2024 kwa mashtaka yanayomkabili ambayo ni biashara ya ngono na ulaghai huku mengine yakiwa ni kuwapiga na kuwadhulumu wanawake baada ya kuwatumia kingono kwa zaidi ya muongo mmoja.
Rapa huyo mwenye umri wa miaka 54 na mtayarishaji nguli wa muziki alikamatwa huko Manhattan jana Jumatatu usiku na tayari leo hii amefikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi wa New York, Robyn Tarnofsky.
Combs anaweza kutumikia zaidi ya miaka 20 gerezani ikiwa atapatikana na hatia ya makosa matatu yanayomkabili: kula njama ya ulaghai, ulanguzi wa ngono, na usafirishaji wa makahaba ambapo mashtaka hayo yaliletwa na ofisi ya Mwanasheria wa Marekani Damian Williams wa Manhattan.
Mashtaka hayo yanaelezea madai ya mwaka 2008 kwamba aliwanyanyasa, kuwatishia na kuwalazimisha wanawake kwa miaka mingi ili kutimiza tamaa zake za ngono, kulinda sifa yake, na kuficha mwenendo wake kwa jamii huku pia anashutumiwa kwa kuwashawishi aliokuwa akiwafanyisha biashara ya ngono kuingia kwenye dawa za kulevya, na pia wakati mwingine kuwahusisha kwenye tamasha lake la maonyesho ya ngono ya siku nzima yanayoitwa "Freak Offs".
Katika mashitaka hayo ambayo yanarejesha shambulio la mpenzi wake wa zamani, mwimbaji wa R&B Cassie, ambalo lilinaswa kwenye video za hoteli waliyokuwa wakipumzika wawili hao na video hizo kusambaa miezi kadhaa hapo nyuma.
Combs alikamatwa jana Jumatatu huko Manhattan, jijini New York nchini Marekani ikiwa ni takribani miezi sita baada ya mamlaka za usalama kukamilisha uchunguzi wa biashara ya ngono kuvamia nyumba zake za kifahari huko Los Angeles na Miami.
Katika kipindi cha mwaka uliopita, Combs ameshtakiwa na watu mbalimbali hasa wanawake ambao wanaosema aliwafanyia unyanyasaji wa kimwili au kingono japo yeye mwenyewe amekana mengi ya madai hayo huku wakili wake, Marc Agnifilo, akisema nje ya mahakama leo Jumanne asubuhi kwamba Combs atakana tena madai hayo kwani hana hatia.
Combs anatuhumiwa katika mashtaka ya kugonga, kupiga ngumi na kuwaburuta wanawake mara nyingi, kurusha vitu na kuwapiga mateke huku akiwaandikisha wasaidizi wake wa kibinafsi, ulinzi na wafanyakazi wa ndani kusaidia kuficha yote.
Mashtaka yanamtaja Combs kama mkuu wa biashara ya jinai inayojihusisha au kujaribu kujihusisha na shughuli haramu mbalimbali ikiwa ni pamoja na biashara ya ngono, kazi ya kulazimishwa, usafirishaji haramu wa makahaba, makosa ya dawa za kulevya, utekaji nyara, uchomaji moto, hongo na kuzuia haki.
Combs, mwanzilishi wa Bad Boy Records, si mara ya kwanza anaingia kwenye matatizo ya kisheria kwani hapo awali Mnamo mwaka 2001, aliondolewa mashtaka yanayohusiana na ufuatiliaji risasi katika klabu ya usiku ya Manhattan huku miaka miwili nyuma alishiriki katika vurugu zilizohusisha matumizi ya bunduki ambayo ilijeruhi watu watatu na kupelekea mlinzi wake wa wakati huo, Shyne, kupatikana na hatia ya kushambulia na alitumikia kifungo cha miaka minane jela.