Miss Tanzania leo kusuka au kunyoa Miss World

Muktasari:
- Fainali za mashindano ya Miss World zinafikia tamati leo, huku macho na masikio ya Watanzania yakiwa kwa mwakilishi Juliana Rugumisa.
Dar es Salaam. Fainali za mashindano ya Miss World zinafikia tamati leo, huku macho na masikio ya Watanzania yakiwa kwa mwakilishi Juliana Rugumisa.
Fainali hizo zinafanyika leo saa 12:00 jioni nchini Puerto Rico, katika ukumbi wa José Miguel Agrelot Coliseum jijini San Juan.
Warembo 103 watapanda jukwaani kuchuana ambapo orodha ya walioingia 30 bora tayari imewekwa hadharani,huku Juliana akiwa hajachomoza popote.
Ikumbukwe Miss Tanzania alifika kambini siku 15 baada ya kuanza kwa kambi ya warembo wanaoshiriki mashindano hayo kukuta baadhi ya vipengele vinavyomuwezesha mshiriki kuingia nafasi za juu vimeshafanyika
Vipengele hivyo ni pamoja na Top Model, Miss mwenye kipaji, mwanamichezo bora na kile cha maswali ya papo kwa hapo kinachojulikana kama 'Head To Head' akishindwa kuwekwa kweyye ratiba kutokana na kuchelewa kufika katika mashindano hayo makubwa ya urembo duniani.
Wakati hali ikiwa hivyo, kwa wawakilishi wa nchi nyingine za Africa ikiwemo Cameroon na Botswana wameonekana kutakata baada ya kuingia kwenye 30 bora.
Kuingia kwao katika nafasi hii ni dalili tosha za mmoja wao kutwaa taji la Miss Africa.Tusubiri tu muda utaongea.
Tanzania kwa mara ya kwanza kung’aa katika mashindano hayo ni mwaka 2005 ambapo Miss Tanzania Nancy Sumari aliweka historia ya dunia kwa kunyakua taji la mrembo wa dunia, Kanda ya Afrika, linalijulikana kama ‘Miss World Africa’
Mwananchi linamtakia kila la kheri Juliana katika fainali hizo.