Majani aingilia kati ishu ya Paula kupewa jina la Kiislamu

Muktasari:
- Hayo ni baada ya mwanamuziki Marioo ambaye amezaa na binti wa Majani kuuliza kwenye mtandao wa Instagram jina gani la kiislamu litamfaa Paula ndipo Majani, akatoa mapendelezo yake.
Dar es Salaam. Mtayarishaji wa muziki nchini Paul Matthysse 'P Funk' amebariki binti yake Paula Paul kubadili dini na kuwa Muislamu huku akimchagulia jina la Sheila.
Hayo ni baada ya mwanamuziki Marioo ambaye amezaa na binti wa Majani kuuliza kwenye mtandao wa Instagram jina gani la kiislamu litamfaa Paula ndipo Majani, akatoa mapendelezo yake.

"Utapewa jina la marehemu bibi yako Sheila au Sheilah au tukupe jina la mama mkubwa wangu Pili?,"ameeleza Majani
Utakumbuka Paula na Marioo tayari wana mtoto mmoja aitwaye Amarah. Tetesi za uhusiano wao zilianzia Aprili 2023, baada ya mrembo huyo kuachana na Rayvanny, tangu wakati huo wamekuwa pamoja, ukiwa ni uhusiano wa kwanza wa Marioo kuuweka hadharani tangu kuhusishwa na Mimi Mars.

Tangu Marioo ametoka kimuziki na wimbo wake, Dar Kugumu (2018), Paula ndiye mrembo pekee ambaye ametokea katika video nyingi za nyimbo zake ambazo ni Lonely (2023), Tomorrow (2023) na Sing (2023).
Mbali na hayo Novemba 2024 Marioo alisema mipango ya kumuoa Paula tayari imefanyika hivyo siku yoyote atatangaza tarehe ya ndoa.

"Sisi tupo kama familia suala la ndoa ni dogo sana, ni kuamua na sheria tumeanza kufuata, mambo ya msingi tumeshafanya imebakia suala la kusema tarehe fulani tunataka kuoana, mpango huo upo kwa sababu nampenda, amenizalia mtoto mzuri kwa hiyo kama hitaji lake ni ndoa ni dogo sana barua tulishapeleka," amesema Marioo.