Kiredio alivyogeuza fursa tabia za wabongo kupenda umbea

Vicent Njau ndilo jina lake halisi ambalo alipewa na wazazi wake, lakini kutokana na kipaji chake cha kuongea kilichoshindwa kujificha tangu akiwa mtoto, alipofika darasa la tatu mwalimu wake alimpa jina la utani Kiredio, ambalo analitumia mpaka hivi sasa.
“Niliamua kuendelea kutumia jina la utani alilonipa mwalimu kwenye kazi zangu kwa sababu niliamini lina bahati ya kujulikana. Jina hili nilipewa nikiwa darasa tatu, lakini mpaka nafika la tano jina langu halisi likawa limepotea, ukiuliza Vicent Njau hunipati ila ukisema Kiredio utanipata,” anasema Kiredio, alipokuwa kwenye mahojiano na gazeti hili.
Anasema alianza kuigiza jukwaani mwaka 2019, jina lake lilifahamika zaidi mwaka 2023 na watu wengi wakapenda anachofanya, mbali ya kuigiza majukwaani amekuwa akifanya video fupi fupi au kontenti kama anavyoziita mwenyewe na kuziweka mtandaoni.
“Wazo la ‘kontenti’ ninazotengeneza zimekuja baada ya kugundua kuwa Watanzania wengi wanapenda umbea, kwa hiyo nikaona nafanya nini ili waweze kufuatilia kitu cha kimbea, nikajaribu kufanya na mtu anipe namba za mpenzi wake nimpigie alafu amtaje jina, nikafanya ya kwanza ikaenda ikapendwa basi nikasema nishikilie hapahapa,” anasema Kiredio.
Mchekeshaji huyo anasema kwa sasa amekuwa akipata ugumu wa kupata kontenti mpya, kwani watu wengi tayari wamemfahamu na wanajua anachofanya kutokana na kazi zake nyingi kwenda mjini. “Sasa hivi wengi wananijua nikimsimamisha mtu ananikataa, wanasema hawataki kuaibika, napata ‘kontenti’ kwa shida sana, hivyo naumiza kichwa nije na kitu gani,” anasema Kiredio.
Kitu asichokuja kukisahau
Pamoja na kufanya kazi nyingi ambazo zimependwa na watu, Kiredio anasema kuwa video ambayo aliifanya na muhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndiyo kazi yake pendwa ambayo hatokuja kuisahau.
“Kontenti ambayo sitaweza kuisahau kiukweli ni ya tukio ambalo limefanya nijulikane kwa Watanzania wengi, la msichana ambaye alikosa gari kwenye graduation ya UDSM 2023, baada ya kushindwa kutaja jina halisi la mpenzi wake ambaye amemnunulia gari.
Nimekutana na matukio mengi lakini lile lilinishangaza, na nikaanza kujilaumu ningejua angekosea mimi ningempanga amtaje mtu fulani, yaani mtu unashindwa vipi kumfahamu mpenzi wako ambaye anaweza kukununulia gari,” anasema.
Kuhusu madai kuwa huwa anawapanga watu kupata kontenti anasema,
“Sijawahi kumpanga mwanachuo yeyote kufanya na mimi ‘kontenti’, ila wanatamani kujua hali ya mahusiano yao, hivyo wananitafuta mwenyewe, nawapa miadi, kwa hiyo watu wakiona naenda kumpokea mtu wanajua nimempanga, lakini siyo kweli sijawahi kumpanga mtu,” anasema.
Anasema kazi hiyo imebadili maisha yake kwa kiasi fulani, ikiwamo kumsaidia mama yake mambo madogomadogo. “Hapo awali nilikuwa ninamtegemea mama kwa kila kitu. Kufutwa kwa akaunti yangu ya TikTok hakukunirudisha nyuma, zaidi pamenipiga teke nimesogea mbele, TikTok ukifanya kazi nzuri unaweza kupata watazamaji milioni moja kwa mwezi, kwa hiyo ‘akaunti’ yangu mpya ndani ya siku sita walinifuatilia zaidi ya watu 600,000, bado ninasonga mbele.
“Vijana tufanye kazi na tusikate tamaa, mimi nimeanza hii kazi mwaka 2019 nimekuja kuonekana na Watanzania 2023, kwa hiyo ukiangalia miaka minne nyuma nilikuwa sina pa kulala, nilikuwa nalala njaa, sina bando sina vocha lakini sikukata tamaa, pengine ningekata tamaa nisingefika hapa nilipo, kijana pambana hakuna kukata tamaa,” anasema Kiredio.