Joshua, Ngannou kuzichapa Machi 8

Muktasari:
- Ngannou aliushangaza ulimwengu katika pambano lake na Furry, huku wapenzi wengi wa mchezo huo wakimmwagia sifa kutokana na uwezo aliouonyesha katika pambano hilo.
Uingereza. Bondia wa uzani wa juu wa Uingereza, Anthony Joshua anatarajia kupanda ulingoni dhidi ya Francis Ngannou katika pambano la uzito wa juu Machi 8, 2024 nchini Saudi Arabia.
Kwa mujibu wa BBC, Ngannou (37) ambaye ni bingwa wa zamani wa UFC, alianza mchezo wake wa kwanza wa masumbwi Oktoba 2023 alipopambana na Tyson Fury katika pambano lilikuwa na upinzani mkali licha ya kupoteza.
Ngannou aliushangaza ulimwengu katika pambano lake na Furry, huku wapenzi wengi wa mchezo huo wakimmwagia sifa kutokana na uwezo aliouonyesha katika pambano hilo.
Furry (35) ambaye ni bingwa wa WBC atapigana na Oleksandr Usyk (36) wa Ukraine anayeshikilia mikanda ya WBA, WBO na IBF Februari 17, 2024.
Waandaaji wa pambano la Joshua na Ngannou walikuwa na nia ya kuandaa pambano kati ya Joshua na Deontay Wilder Machi 2024, lakini uamuzi huo ulibadilishwa kutokana na Wilder kupoteza pambano lake la hivi karibuni dhidi ya Joseph Parker wa New Zealand.
Inaelezwa kuwa wiki chache zilizopita Joshua alikuwa akipuuza uwezekano wa kupigana na Ngannou, lakini kupoteza mapambano kwa Wilder na Parker kulimfanya kufikiria upya maamuzi yake na hatimaye kukubali.