Jidenna anavyobebwa na wimbo mmoja
Muktasari:
- Katika pitapita zangu mitandaoni nimeona mjadala kutoka kwa mashabiki, asilimia kubwa wakieleza kuwa wanamfahamu msanii huyo kupitia wimbo wake wa Bambi pekee na kuwa nyimbo zake nyingine hawazitambui kabisa.
Marekani. Kila msanii huwa na wimbo mmoja unaobaki kwenye kumbukumbu za mashabiki kwa muda mrefu. Kwa rapa Jidenna, wimbo wake wa ‘Bambi’ umekuwa ukidumu mioyoni mwa watu kwa takribani miaka tisa tangu uachiwe.
Katika pitapita zangu mitandaoni nimeona mjadala kutoka kwa mashabiki, asilimia kubwa wakieleza kuwa wanamfahamu msanii huyo kupitia wimbo wake wa Bambi pekee na kuwa nyimbo zake nyingine hawazitambui kabisa.
Mbali na Bambi, Jidenna amewahi kutoa nyimbo nyingine kadhaa zilizofanya vizuri zikiwemo Classic Man, Long Live the Chief, Chief Don't Run, Little Bit More, Tribe, Sufi Woman, Boomerang na Yoga aliyoimba pamoja na Janelle Monáe.
Jidenna jina halisi Jadenna Theodore Mobisson alizaliwa Septemba 4, 1985 huko Wisconsin, Marekani. Baba yake alikuwa profesa kutoka Nigeria na mama yake ni Mmarekani. Akiwa mtoto aliishi Marekani na Nigeria, hali iliyomfanya akue akiwa na mchanganyiko wa tamaduni za pande zote mbili.
Baada ya kumaliza masomo yake, alianza kujihusisha na muziki. Alikuwa akiandika nyimbo na kufanya maonyesho mitaani na kwenye sehemu za starehe, lakini baada ya muda msanii na mtayarishaji Janelle Monáe alimfanyia mpango wa kujiunga katika lebo ya Wondaland Records.
Baada ya hapo mwanga ukaanza kuonekana ambapo mwaka 2015 aliachia wimbo wa Classic Man uliogeuka kuwa moja ya nyimbo kubwa zaidi nchini Marekani. Wimbo huo ulimpa umaarufu mkubwa, na kuingia kwenye chati mbalimbali za muziki huku ukipata uteuzi katika tuzo za Grammy.
Mwaka 2017 Jidenna aliachia albamu yake ya kwanza iitwayo ‘The Chief’, ambayo ilibeba wimbo wa Bambi. Video ya wimbo huo ilivutia wengi kutokana na ubunifu wake na simulizi ya mapenzi iliyofanya nyimbo hiyo kupendwa katika nchi nyingi za Afrika huku wengi wakijua kuwa ndio ulikuwa wimbo wa kwanza wa Jidenna.
Baada ya mafanikio ya The Chief, aliachia albumu nyingine ya 85 to Africa mwaka 2019, kazi iliyobeba nyimbo nyingi zenye ladha ya Afrika. Mwaka 2023 aliachia albamu yake ya tatu ME YOU & GOD, akionyesha bado anaendelea kufanya muziki licha ya kutotokeza kwenye vichwa vya habari kama zamani.
Katika upande wa tuzo, mafanikio makubwa ya Jidenna yalitokana na wimbo wa Classic Man, ambao ulifanya aingie katika uteuzi wa tuzo za Grammy huku akishinda tuzo za Soul Train Music Awards. Ingawa Bambi haikushinda tuzo kubwa kama ilivyokuwa kwa Classic Man, ndiyo wimbo uliomfanya ajulikane zaidi katika sehemu nyingi za Afrika.
Kwa sasa Jidenna bado yupo kwenye muziki na amekuwa akitoa kazi mpya kwa vipindi tofauti huku akijihusisha pia na shughuli za uandishi, mitindo ya mavazi na miradi inayohusiana na utamaduni wa Afrika. Mpaka kufikia sasa wimbo wake wa Bambi umetazamwa zaidi ya mara milioni 44 katika mtandao wa YouTube.