Intaneti inavyowainua wasanii kiuchumi
Muktasari:
- Hata hivyo, utamaduni wa kuuza kanda wapo walionufaika nao, mathalani kwa mujibu wa Ferooz albamu yake ya kwanza, Safari (2005) chini ya Bongo Records iliuza nakala 200,000 na kumpatia Sh150 milioni
Dar es Salaam. Miaka ya nyuma wasanii wa muziki na filamu walitegemea kuuza kanda kama njia ya kuingiza kipato, wanamuziki walikuwa na njia ya pili nayo ni kufanya matamasha ila sasa mambo yamebadilika baada ya kuimarika huduma ya intaneti na ujio wa mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, utamaduni wa kuuza kanda wapo walionufaika nao, mathalani kwa mujibu wa Ferooz albamu yake ya kwanza, Safari (2005) chini ya Bongo Records iliuza nakala 200,000 na kumpatia Sh150 milioni.
Nayo albamu ya TID, Sauti ya Dhahabu (2002) iliyotoka na nyimbo kali kama Zeze na Siamini, ilipoingia sokoni ilimpatia kitita cha Sh30 milioni, fedha hiyo ikagharamikia studio na video chache alizofanya, hivyo akabakiwa na Sh22 milioni.
Lakini kuimarika kwa huduma ya intaneti na kushika kwa kasi mitandao ya kijamii, utamaduni wa kuuza kanda ulitoweka na wasanii kuanza kuuza kazi zao mitandaoni katika majukwaa mbalimbali kama Spotify na YouTube.
“Mimi ni kati ya wasanii ambao hawapigi show sana ila nategemea fedha za mtandaoni, yaani huku napata fedha Spotify, YouTube, Boomplay, Audiomack, kwa hiyo mwisho wa mwezi unashangaa unapokea mshahara kama watu wengine walioajiriwa,” anasema Foby.
Dittomusic.com inakadiria wimbo unaposikilizwa (streams) zaidi ya mara milioni 1 katika mtandao wa Spotify na watu ambao wapo katika huduma ya malipo, basi msanii husika atapata Dola 4,370, huku Apple Music wakilipa Dola7,350 na YouTube Music Dola 690.
Mwishoni mwa 2023 Variety waliripoti kuwa staa wa Pop Marekani, Taylor Swift alipokea kitita cha Dola 104 milioni kutokana na mauzo ya muziki wake katika mtandao wa Spotify baada ya nyimbo zake kusikilizwa zaidi ya mara bilioni 26.1 kwa mwaka huo.
Ikumbukwe Taylor Swift ambaye ameuza rekodi zaidi ya milioni 200 duniani kote na kushinda tuzo 14 za Grammy, Oktoba mwaka huu alitangazwa na Forbes kufikia hadhi ya ubilionea akikadiriwa kuwa na utajiri wa Dola1.6 bilioni.
“Tunategemea intaneti kwa kutangaza na kuuza muziki na kuwasiliana na mashabiki wetu, kwa hiyo huduma hiyo inavvyozidi kuimarika maana yake sanaa inazidi kukua maana inakuwa rahisi kuwafikia wateja wetu ambao ndio mashabiki,” anasema Kala.
Mwimbaji wa Bongo fleva, Diamond Platnumz aliwahi kueleza kuwa wasanii wanapofurahia kupata namba kubwa YouTube au kuonyesha kushindani katika mtandao huo sio kutafuta sifa za bure bali kutokana na faida wanayoipata kiuchumi.
Mfano video ya wimbo wake, Waah! (2020) akimshirikisha Koffi Olomide kutoka DR Congo ilipotazamwa mara milioni 39.3 iliweza kumuingiza kiasi cha Euro 32,266, na sasa video hiyo imetazamwa zaidi ya mara milioni 167.4, hivyo ni wazi kapata fedha zaidi.
Hata hivyo, wasanii hawatumii tu mitandao kwa ajili ya kuuza kazi zao bali hata kukuza chapa zao kitu kinachopelekea kuwa na wafuasi wengi, na hapo inafunguka fursa nyingine ya kuwa mabalozi wa kutangaza huduma au bidhaa mbalimbali.
Ebitoke ni muigizaji ambaye anatumia ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 4 kuweka matangazo ya aina mbalimbali, anasema hiyo ni moja ya faida na sababu za kuendelea kuwa na ukurasa huo.
“Kwa tangazo moja kama ni la picha natoza Sh50,000 kama ni la video natoza Sh100,000, na hiyo ni kwa kuposti mara moja tu,” amesema Ebitoke.
Selena Gomez kutokea Marekani ambaye ndiye mwanamuziki mwenye wafuasi wengi Instagram duniani akiwa nao milioni 423, anatajwa na Influencer Marketing Hub kuwa hulipwa Dola 2.5 milioni ili kuchapisha tangazo moja katika ukurasa wake huo.
“Inavutia pale ambapo kampuni zinataka kufanya kazi na wewe ina maana sanaa yako ina ushawishi katika jamii. Kwa hiyo ni kitu kikubwa ambacho kimewapa mafanikio makubwa wasanii wengi na nina furahi kuwa miongoni mwao,” amesema Rosa Ree.