Imechukua miaka miwili Diamond kuingia Billboard

Muktasari:
- Hatua hiyo inakuja wiki mbili tangu Diamond kutoa remix ya wimbo huo akimshirikisha Jason Derulo wa Marekani akiungana na Khalil Harisson na Chley wa Afrika Kusini waliosikika katika toleo la kwanza ambalo ndilo limeingia Billboard.
Dar es Salaam, Hatimaye baada ya miaka miwili Bongo Fleva imefanikiwa kupata nafasi kwa mara ya kwanza katika chati ya Billboard U.S Afrobeats Songs kupitia wimbo wa Diamond Platnumz, Komasava (2024) uliotengenezwa na S2kizzy.
Hatua hiyo inakuja wiki mbili tangu Diamond kutoa remix ya wimbo huo akimshirikisha Jason Derulo wa Marekani akiungana na Khalil Harisson na Chley wa Afrika Kusini waliosikika katika toleo la kwanza ambalo ndilo limeingia Billboard.
Ikumbukwe mnamo Machi 29, 2022 ndipo chati ya kwanza ya Billboard U.S Afrobeats Songs, ilitoka ambapo msanii wa Nigeria, Ckay alishika namba moja kupitia wimbo wake, Love Nwantiti (2020).
Nafasi ya pili ilienda kwa Fireboy DML kupitia wimbo, Peru (2021), nafasi ya tatu akachukua Wizkid, Essence (2021). Kwa ujumla nafasi ya kwanza hadi ya 10, wasanii wa Nigeria ndiyo walishika wakiwa wameshirikia na wenzao wa Uingereza, Marekani .
Billboard ambao kwa miongo mingi wanasimamia chati kubwa za muziki duniani kama Billboard Hot 100, Billboard 200, Billboard Global 200, Billboard Holiday Hot 100 n.k, walianzisha Billboard U.S Afrobeats Songs kwa kushirikiana na tamasha la Afronation.
Chati ya Billboard U.S Afrobeats Songs inatoa orodha ya nyimbo 50 za Afrobeats kutoka Afrika ambazo ni maarufu nchini Marekani na inapangwa kwa jinsi wimbo husika unafanya vizuri upande wa kusikilizwa na mauzo kwenye majukwaa makubwa ya mtandaoni.
Sasa Komasava ya Diamond imeingia moja kwa moja hadi nafasi ya 39 kati ya nyimbo 50, huku wimbo wa mshindi wa Grammy 2024 kutoka Afrika Kusini, Tyla, Water (2023) ukishika nafasi ya kwanza ambapo umekaa hapo kwa wiki 43.
“Afrobeats imekua kwa kiasi fulani kama mahadhi nchini Marekani, na tunajivunia kuonesha nyimbo zinazofanya vizuri na wasanii katika chati hizi mpya za kila wiki.” alisema Makamu Mkuu wa Rais wa Chati na Maendeleo Billboard, Silvio Pietroluongo.
Ikiwa Komasava itaendelea kufanya vizuri, ni wazi itapanda juu zaidi ndani ya Billboard U.S Afrobeats Songs, hivyo kuchochea remix yake aliyoshirikiana na Jason Derulo wa Marekani kuingia Billboard Hot 100, chati kwa ajili ya nyimbo zinazofanya vizuri duniani kote.
Utakumbuka Wizkid kutoka Nigeria aliingia kwa mara ya kwanza Billboard Hot 100 kupitia wimbo, One Dance (2016) ambao ameshirikishwa na Drake kutokea Marekani, huu ulifanya vizuri hadi kushika nafasi ya kwanza.
Agosti 2019 alirejea tena Billboard Hot 100 baada ya kushirikishwa na Beyonce wa Marekani katika wimbo, Brown Skin Girl (2019), kisha baadaye akaingia rasmi na wimbo wake, Essence (2020) akimshirikisha Tems ukiwa ni wimbo wa kwanza Nigeria kufanya hivyo.
Akizungumzia mafanikio hayo ya Diamond, Babu Tale, Meneja wa WCB Wasafi na Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, amempongeza msanii huyo na kusema hayo ni matokeo ya kujitoa zaidi kwa kile anachokiamini.
“Kile ambacho tunakiona kwa Diamond leo hii, ni sehemu au matunda ya jitihada za yeye na timu yake ambazo wamezionesha, kuwa kwenye Billboard ina maana na sisi Swahili Nation tunaenda kugusa hizo sehemu.” alisema Babu Tale.
Baada ya kuingia Billboard U.S Afrobeats Songs, Diamond anaendelea kuandika rekodi kama msanii wa kwanza Tanzania na Afrika katika mambo mengi upande wa sanaa na biashara kitu kinachomtofautisha na wenzake wengi.
Akiwa ndiye msanii aliyeshinda tuzo nyingi zaidi za muziki Tanzania (TMA) kwa muda wote, 18, pia Diamond ni msanii wa kwanza Tanzania kumiliki redio na TV akiwa wa pili Afrika baada ya Youssou N’Dour, mshindi wa Grammy 2005 kutoka Senegal.
Ndiye msanii mwenye wafuasi wengi katika mitandao ya kijamii Afrika Mashariki wa kwanza Afrika kufikisha ‘views’ bilioni 2 YouTube.
Anashikilia rekodi kama msanii wa kwanza Afrika kushinda tuzo mbili za MTV Europe Music Awards (MTV EMA) kwa usiku mmoja. Diamond alishinda 2015 katika vipengele vya ‘Best African Act’ na ‘Best Worldwide Act/ India’ ambacho Miss World 2000 na Staa wa filamu India, Priyanka Chopra naye alikuwa anawania.