Hili ndilo chimbuko la matabaka kwenye muziki wa Hip-hop

Muktasari:
- Kwa nchi kama Marekani muziki huo ndiyo umeshamiri, ukiongoza kwa zaidi ya asilimia 80 kusikilizwa kwenye mitandao ya kusambazia muziki kama vile Spotify, Apple Music, AudioMack na mingineyo
Dar es Salaam, Hip-hop ni muziki unaotajwa mara zote kuwa unazungumzia uhalisia wa maisha ya watu ukiakisi yale ambayo wamekuwa wakiyaishi
Kwa nchi kama Marekani muziki huo ndiyo umeshamiri, ukiongoza kwa zaidi ya asilimia 80 kusikilizwa kwenye mitandao ya kusambazia muziki kama vile Spotify, Apple Music, AudioMack na mingineyo.
Kwa takwimu hizo inaonesha dhahiri kuwa ni muziki ambao unateka hisia za watu wengi duniani na ndiyo maana umepewa kipaumbele na wasikilizaji wa rika zote.
Si ajabu kwenye baadhi ya matamasha yanahusisha watoto kuonesha vipaji kuona mmoja au wawili watajitokeza kwa ajili ya kuchana mashairi ya muziki huo.
Kwa Tanzania Hip-hop imekuwa ikibebwa tangu zamani na baadhi ya wasanii kama vile Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Joseph Haule ‘Profesa Jay’, Mwana FA, Fid Q, King Crazy GK, Chidi Benz, Saigon, Ngwair, AY na wengine wengi ambao kwa mashairi yao yaliyojaa umahiri waliweza kuteka nyoyo za mashabiki kuusikiliza muziki huo .
Mbali na wachanaji wa enzi za kina Sugu pia kuna kizazi kingine cha wachanaji kama Roma, Wakazi, One The Incredible, Marehemu Godzilla, Nay wa Mitego, Zaiid, P the Mc, Nash Mc na wengine kibao.
Kizazi hiki nacho kilitokea na kinaendelea kufanya yake katika kutoa burudani na sasa kuna kizazi cha kina Young Lunya, Rapcha na wengineo.
Ukisoma mtiririko huo utaona kwa kiasi gani kiwanda cha muziki wa Hip-hop kimekuwa na bahati ya kupata vichwa vikali.
Licha ya hayo kwenye kundi la watu ambao wanafanya jambo la kufanana hakukosekani utofauti wa kimawazo na kimitazamo, pamoja na matabaka ambayo wakati mwingine hupelekea watu kijitenga.
Hata kwenye muziki wa Hip-hop duniani iko hivyo kuna makundi mbalimbali ya wasanii ambayo wameamua kujitenga huku wengine wakidai wanachoimba kinagusa jamii moja kwa moja na wengine wakidai cha kwao kinagusa jamii na kuburudisha lakini wote wanafanya muziki wa aina moja.
Ikumbukwe kuwa muziki wa Hip-hop, unaojulikana pia kama rap na zamani disco rap, ni aina ya muziki maarufu ambao ulianzia mwanzoni mwa miaka ya 1970, kutoka kwa Wamarekani weusi na wahamiaji wa Afro-Caribbean huko Bronx, New York City.
Kwa miaka mingi Tanzania umekuwa ukitawala muziki wa aina moja, muziki wa kizazi kipya na kufanya aina nyingine za muziki kama wa Hip-hop kusikika kwa uchache. Jambo linalopelekea uhitaji wa akili kubwa kwenye kuandaa kazi za Hip-hop ili ziweze kufika mbali kama ambavyo wasanii wa kizazi kipya wanafanya.
Wiki moja baada ya Roma kuachia albamu yake ya kwanza inayoitwa Nipeni Maua Yangi, iliibuka mijadala mbalimbali kwenye mtandao wa ‘X’, ikihusisha baadhi ya watu kukosoa na wengine kusifia ubunifu alioufanya kwenye albamu hiyo.
Moja kati ya watu waliokosoa kazi hiyo ni pamoja na msanii wa Hip-hop anayefahamika kwa jina la Wakazi, ambaye alichambua albamu hiyo na kuanisha kasoro alizoziona.
Katika majibizano yao inaonekana kila mmoja anajiona mwamba dhidi ya mwenzie, maneno ya Wakazi kuhusu albamu ya Roma yalidai kuwa albamu ni mbaya huku akitoa sababu kuwa Roma ameongea pumba. Aidha katika maneno hayo Wakazi alimtaka Roma aache kujadili uandishi wake.
Migogoro kama hiyo ndiyo inaonesha matabaka kwenye muziki huo kwani wote wanafanya Hip-hop lakini kila mmoja anaamini anafanya muziki zaidi ya mwingine.
Luqman Maloto
Mbali na migogoro kuwa chanzo cha matabaka mkongwe kwenye upande wa uandishi habari na mfuatiliaji zaidi wa muziki nchini Luqman Maloto, amesema si vibaya kila mtu kufanya anachoweza kikubwa iwe biashara na apate wanunuaji huku akitolea mfano wa safari ya kimuziki ya msanii Darassa ilivyobadilika kutoka kuwa rapa anayeelimisha hadi kuwa rapa anayeburudisha.
“Ukishafanya kitu kuwa biashara hupaswi kumpangia mtu cha kufanya, hivyo inatakiwa shabiki mwenyewe achague nini anapenda, kama mtu anaimba vitu laini na anapata watu wa kumsikiliza huwezi kusema anakosea na kumwambia abadilike.
“Na kama mtu anaimba vitu vigumu na anapata mashabiki pia wanaomsikiliza huwezi kusema anakosea sababu tayari anafanya biashara,” alisema Maloto.
Soggy Doggy
Soggy ambaye ni mmoja kati ya wasanii na watangazaji wakongwe na mdau wa muda mrefu wa muziki wa Hip-hop alisema swala la matabaka si geni na linafanyika duniani kote halikuanzia Tanzania.
Alisema hayo huku akitolea mfano wa tofauti iliyokuwepo nchini Marekani ambapo upande wa The Notorious Big walikuwa wakiimbia starehe tu na upande wa kina 2pac walikuwa wakiimbia mambo ambayo yalikuwa yanaigusa jamii
“ Siyo jambo geni hilo jambo ni kawaida kwa utamaduni wa Hip-hop duniani kote vizazi na vizazi” alisema Soggy.