Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hata mikoani kuna wasanii

Muktasari:

  • Mashindano yaliweka hadharani umahiri wa wanamuziki kutoka kambi mbalimbali za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na kambi za Jeshi la Kujenga Taifa

Dar es Salaam, Vikundi washiriki wa Mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi yaliyomalizika mwishoni mwa mwezi wa nane, yameonyesha ukweli ambao umekuwa umefichika miaka mingi ya karibuni kuwa hata mikoani kuna wasaniii wenye weledi wa hali ya juu. 

Mashindano yaliweka hadharani umahiri wa wanamuziki kutoka kambi mbalimbali za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na kambi za Jeshi la Kujenga Taifa . 

Vikundi vya ngoma na bendi vilitoka  Mlale JKT ya Songea, Mpwapwa JKT, Makutopora JKT, TMA Jazz Band ya Arusha ambayo zamani ilikjulikana kama Les Mwenge, Nyuki Jazz Band ya Zanzibar, na vyote vilionyesha umahiri wa hali ya juu.

Kwa muda mrefu wanamuziki wote maarufu ilikuwa kama ni  lazima watoke Dar es Salaam au wahamie Dar es Salaam ili kwanza wapate umaarufu. 

Hili ni jambo la kushangaza kwa kuwa katika zama hizi vyombo vya utangazaji viko karibu kila wilaya mkoa kuna kituo cha redio, pia kuna mtandao wa intanet ambao unatoa fursa ya kujitangaza toka popote duniani.  Hebu turudi nyuma  miaka 50 iliyopita.  

Tanzania ilikuwa na kituo kimoja kikubwa cha redio nacho ni Radio Tanzania Dar es Salaam, pia kulikuwa na  redio moja nyingine maarufu kwa muziki injili, ilikuwa inaitwa Radio Sauti ya Injili.

Magazeti yalikuwa machache kama vile The Standard, Nationalist, Uhuru na Mzalendo  yalikuwa ndio magazeti makubwa nchini, ni watu wachache sana walioweza kupata nakala za magazeti haya nchini kutokana na miundombinu wakati ule, pamoja na hali hiyo wanamuziki kutoka kila kona ya nchi waliweza kupata umaarufu hata kama hawakuwahi kugusa jiji la Dar es Salaam. 

Hebu tuangalie baadhi ya bendi zilizokuwa na maskani nje ya Dar es Salaam ambazo ziliweza kuweka alama  sio tu nchini, bali zilifikia hata kujulikana nje ya mipaka ya nchi hii, tuanze na mkoa wa Morogoro. Mkoa huu ulikuwa na bendi maarufu karibu kila wilaya.

Cuban Marimba na Morogoro Jazz Band za mjini Morogoro,  bendi ambazo zilikuwa na sifa hasa za kuitwa kongwe mkoani hapa, maana zote mbili ziliundwa kati ya mwaka 1942 mpaka 1946, bendi hizi ziliendelea kutamba mpaka miaka ya 70. 

Mkoa wa Morogoro ulikuwa pia na bendi kama Kilosa Jazz Band, Sukari Jazz Band,  Mahenge Jazz Band, Kilombelo Jazz Band, Njohole Jazz band na hata bendi maarufu ya shule ya sekondari ya Kwiro iliyoitwa Kwiro Jazz Band, kuna hadithi kuwa hata mitindo maarufu ya Morogoro Jazz Band kama vile Likembe  ulianzishwa na bendi hii ya shule. 

Mji wa Tanga nao ulitoa mchango mkubwa sana katika muziki wa Afrika Mashariki kwa ujumla. Kulikuwa na bendi nyingi maarufu, zikiwemo bendi mbili ambazo nazo zilianza miaka ya hamsini. Jamhuri Jazz Band ambayo ilianza kama Young Nyamwezi Jazz Band, kwenye mwaka 1955 na washindani  wao Atomic Jazz Band. 

Kwa miaka mingi bendi hizi zilikuwa na wapenzi kutoka  kila kona ya Afrika ya mashariki.  Mchango mkubwa zaidi wa Jamhuri Jazz Band katika muziki wa Afrika Mashariki, ni kuwa mbegu iliyoanzisha bendi ya Simba wa Nyika, bendi ambayo ilikuwa chini ya ndugu wawili Wilson Peter na George Peter.

Na kutokana na bendi hii kukaja kupatikana bendi nyingi sana zikiwemo Les Wanyika, Orchestra Jobiso, Orchestra Les les na nyingine nyingi zilizokuja kutawala anga ya muziki Afrika Mashariki kwa kipindi kirefu. 

Tanga pia kulikuwa na vile vikundi maarufu vya muziki wa Taarab, Lucky Star na Black Star. Sifa kubwa ya vikundi hivi ni kuwa haswa ndivyo vyaweza kupata sifa ya kuanzisha ‘modern taarab’, kwani wao ndiyo walianza kutumia vyombo kama magitaa ya umeme katika muziki wa taarab. Mwanamuziki maarufu wa Mombasa Juma Bhallo alianza muziki wa taarab kwao baada ya kupitia makundi haya. 

Kule Tabora kulikuwa na bendi nyingi maarufu kama vile Tabora Jazz Band, Kiko Kids, Nyanyembe Jazz Band, ambazo nazo kwa miaka mingi si tu kuwa ziliwaburudisha wakazi wa Tabora lakini pia kujulikana na kupendwa nchi jirani. 

Rafiki yangu mmoja mwanamuziki maarufu kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo aliwahi kunambia kisa cha kuja kutafuta kazi ya muziki Tanzania ni baada ya kuwa akisikia muziki wa Tabora Jazz Band na ndoto yake ilikuwa kuja kufanya kazi kwenye nchi yenye bendi nzuri kama ile.  

Mwanza palikuwa na bendi maarufu ya Super Veya ambayo iliundwa na wanamuziki wengi kutoka Kongo, na ni bendi ambayo ilimlea mwanamuziki maarufu Zahir Ally Zorro, na pia kulikuweko na bendi ya Kimbo Twist Band ambayo ilitoa wanamuziki wawili waliochangia sana muziki wa dansi, marehemu Rashid Hanzuruni na marehemu Kassim Mponda. 

 Kule Geita kulikuwa na bendi ya GEDECO Jazz Band, bendi iliyokuwa mali ya shirika la Geita Development Corporation, bendi ambayo ilikuwa mwanamuziki kutoka Nigeria.
 Musoma Jazz Band na Mara Jazz Band zinajieleza maskani yake kutokana na majina yao. Nyimbo kama Kitenge cha Sikukuu ziliifanya Mara Jazz kuwa maarufu nchi nzima. 
   
Kule Kigoma kulikuwa na Lake Tanganyika Jazz Band au maarufu kama Lake Jazz.bendi ambayo alianzia marehemu Shem Karenga. Iringa kulikuwa na bendi kadhaa kama Born Jazz band, Habanero Jazz Band na kadhalika lakini iliyokuwa na umaarufu zaidi ni Highland Stars Jazz Band, kiongozi wa bendi hiyo ndiye baba mzazi wa mpiga solo na mpiga kinanda maarufu wa Msondo Ridhwani Pangamawe. 

Iringa pia kulikuwa na bendi ya wanafunzi iliyowahi kuwa maarufu iliyoitwa Orchestra Mkwawa, na hakika huwezi kuacha kutaja Tancut Almasi Orchestra, bendi ambayo mwandishi aliwahi kuipigia kati ya mwaka 1986 na 1989 na nyingine nyingi.

 Mashindano ya Utamaduni ya Mkuu wa Majeshi yana kila dalili za kufufua hali ile ya kuweko na bendi maarufu kila kona ya nchi. Nawashauri viongozi wa vyombo vya habari vya kila wilaya waanze uzalendo na kuwaangalia kwa upendeleo wasanii waliomo katika wilaya zao.