Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Filamu za Usawa na Uhuru wa Kujieleza kushiriki SZFF

Muktasari:

  • Tamasha hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Habari na Uchechemuzi Tanzania (Medea-Tanzania), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali litafanyika Oktoba 11 hadi 14 katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Dar es Salaam. Jumla ya filamu 250 kutoka Tanzania, Kenya, Nigeria na Afrika Kusini zinazohusu Usawa na Uhuru wa Kujieleza, zitashiriki katika Tamasha la Filamu la Sauti Zetu (SZFF) msimu wa pili.

Tamasha hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Habari na Uchechemuzi Tanzania (Medea-Tanzania), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali litafanyika Oktoba 11 hadi 14 katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Akizungumza na wanahabari leo Jumanne Septemba 24,2024, mratibu wa tamasha hilo, Sheila Kipuyo amesema litawaleta pamoja watengenezaji filamu, waigizaji na wapenzi wa filamu kutoka Afrika Mashariki na maeneo mengine Afrika.

“Tumepokea takribani filamu 250 kutoka Tanzania, Kenya, Nigeria na Afrika Kusini, zenye mada kuu zinazohusU usawa na uhuru wa kujieleza. Tamasha la mwaka huu, lina kauli mbiu ya ‘Beyond the Screen’,” amesema Kipuyo

Amesema tamasha hilo litaanza Oktoba 11 hadi 12 katika Ukumbi wa The Little Theater, Dar es Salaam na kutakuwa na uoneshaji wa filamu, warsha na mijadala. Wakati Oktoba 13 na 14 litafanyika Mwandenge na Kibaha mkoani Pwani.

“Wananchi watapata fursa ya kuangalia filamu na kushiriki mijadala yenye kuleta mabadiliko, lakini mwaka huu kutakuwa na mabadiliko, tofauti na mwaka jana na kumeongezwa programu maalumu, ikiwemo Sauti Zetu Storytellers Lab.

“Storytellers Lab itatoa mafunzo kwa watengenezaji wa filamu 15 kuhusu mbinu ya kupata rasilimali za kuwezesha uzalishaji wa filamu. Kutakuwa na uoneshaji wa filamu katika kibanda umiza tukisisitiza kuendeleza urithi wetu wa kitamaduni kupitia simulizi za kisasa,” amesema Kipuyo.

Aidha ameeleza katika tamasha hilo kutakuwa na mijadala ikigusia masuala muhimu ikiwemo uhuru wa kujieleza, usawa wa kijinsia na hali ya sasa ya tasnia ya filamu Afrika.

“Tuzo maalumu zitatolewa kwa watengenezaji wa filamu bora waliotoa mchango mkubwa katika sekta ya filamu barani Afrika. Washiriki mashuhuri wa mwaka huu ni pamoja na watengenezaji wa filamu, akiwemo Ayoub Kondo maarufu ‘The East African Black Jesus’, Juma Saada, na wengine kutoka Kenya,” amesema.

Kwa mujibu wa Kipuyo, filamu zilizochaguliwa kuingia katika tamasha hilo ni Kitovu cha Kifo, My Woman na Lost anad Found za Tanzania. Katika kipengele cha ‘ajenda yetu’ kutakuwa na filamu za Unasemaje (Tanzania), 1992 (Kenya), Beckma na Ifediche (Nigeria), Warm (Afrika Kusini) 

“Kipengele cha Community Baraza kutakuwa na filamu za zinazoibua mijadala katika jamii ambazo ni Mbozo (Tanzania) Last Super, The Caller na Kanairo (Kenya).”

Wakati kipengele cha The Reel Docs (Documentary) kutakuwa na filamu za Softie, No Simple Way Home, Shifting Power za (Kenya) While We Watched (India) na Esther and the Law (Nigeria and Netherlands,” amesema Kipuyo.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Filamu kutoka Bodi ya Filamu Tanzania (TFB), Emmanuel Ndumukwa amesema ni furaha kuona taasisi binafsi zikiandaa matamasha kama hayo.

“TFB tuna furahi tunapoona taasisi binafsi zinaandaa matamasha ya filamu ambayo yanachangia kuongeza ushindani, weledi na kutengeneza uhusiano na maeneo mengine,” amesema Ndumukwa.

Ndumukwa amesema TFB imefurahishwa na uwepo wa Storytellers Lab katika tamasha hilo, akisema kitendo cha Medea kuchagua watu 15 kupata mafunzo hayo ya kipengele hicho ikiwemo uandishi wa hadithi za filamu kutaongeza chachu katika filamu nchini.