Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Agrey Ndumbalo mpiga gitaa la ridhim wa Vijana Jazz Band

Muktasari:

  • Katika moja ya mifumo ya awali ya muziki wa dansi,  bendi zilikuwa  na mfumo wa kutumia magitaa ya aina tatu, gitaa la Solo,gitaa la ridhim na gitaa la Bass. Gitaa la solo lilikuwa na sauti ya juu, huku gitaa ridhim likiwa na sauti nzito kidogo ya kati, na mwisho gitaa la bass likiwa na sauti nzito kuliko magitaa mengine

Dar es Salaam, Muziki huu unaoitwa wa dansi umepitia mabadiliko mengi na hakika bado unaendelea kubadilika badilika kutokana na kuingia kwa wanamuziki wapya, teknolojia mpya na pia kupata vionjo vipya kutokana na muziki wa wanamuziki wengine duniani.

Katika moja ya mifumo ya awali ya muziki wa dansi,  bendi zilikuwa  na mfumo wa kutumia magitaa ya aina tatu, gitaa la Solo,gitaa la ridhim na gitaa la Bass. Gitaa la solo lilikuwa na sauti ya juu, huku gitaa ridhim likiwa na sauti nzito kidogo ya kati, na mwisho gitaa la bass likiwa na sauti nzito kuliko magitaa mengine.

Kimuundo gitaa la rythm na la solo hakuna tofauti. Yote yana nyuzi 6, lakini tofauti ilikuwa  katika upigaji na urekebishaji wa sauti kwenye amplifier. Gitaa la rythm hunyimwa treble (ukali) kiasi na kuongeza bass zaidi kuliko gitaa la solo ambalo huwa na treble zaidi ya magitaa mengine. 

Gitaa la bass awali lilikuwa na nyuzi mbili, likabadilika na kuwa na nyuzi nne na hiyo ni aina ya gitaa la bass ambalo wapiga gitaa hilo wengi hutumia japo siku hizi kuna magitaa ya bass yenye nyuzi tano, mengine nyuzi saba na hata yako yenye nyuzi nane. 

Mwanzoni mwa miaka ya 60 likaanza kutumika gitaa la nne lililojulikana kama ‘second solo’ au Wakongo waliliita ‘mi solo’. Inasemekana kaka yake mpiga solo maarufu wa Kongo wa enzi hizo Nicolaus Kasanda maarufu kwa jina la DR Nico, ndiye aliyeanzisha mtindo wa kuongeza gitaa hilo la nne. 

Baada ya mtindo huo kuwa maarufu, gitaa la ‘second solo’ lilikuwa likipigwa kwa mifumo mbalimbali katika bendi mbalimbali. Bendi nyingine zilitumia second solo kama gitaa lililokuwa linajibizana na solo, na bendi nyingine lilitumia gitaa hilo kuwa likijibizana na gitaa la ridhim na hata kulikuweko mfumo ambapo gitaa hilo aidha lilikuwa likipiga sauti ya pili ya chochote ambacho gitaa la solo au ya gitaa la ridhim lingepiga.

Bendi nyingine  mfano  Cuban Marimba Band iliyokuwa Morogoro, iliyokuwa chini ya Juma Kilaza, iliongeza ubunifu na kuongeza gitaa la 5 na kuliita ‘chord guitar’. Uamuzi wa aina ya mpangilio wa magitaa uliweza kuleta tofauti kubwa ya muziki kati ya bendi moja na nyingine.

Gitaa la ridhim bado linapigwa katika bendi nyingi lakini umuhimu wake umeshuka sana. Katika kipindi cha miaka ya 60 na 70, gitaa hili lilikuwa na umuhimu mkubwa na wapigaji wake waliweza kubuni staili zao wenyewe, na kujijengea sifa kubwa zinazodumu mpaka leo.

Kati ya wapiga rythm maarufu alikuweko Harrison Siwale aliyekuwa maarufu kwa jina la Satchmo, mwanamuziki huyu asili yake ilikuwa Zambia, wazazi wake walihamia Tanga wakati ule Tanga ikiwa kivutio kikubwa cha ajira kutokana na zao la mkonge.

Satchmo alipigia bendi kubwa za Tanga ikiwemo Atomic Jazz Band na hatimaye Jamhuri Jazz Band. Mwanamuziki huyu aligundua staili peke yake ya kupiga gitaa la rythm, wapigaji wengi walichukua mtindo wake na  kuongeza vionjo na kupata nao umaarufu mkubwa.

Upigaji wake wa gitaa la ulizifanya nyimbo za Jamhuri Jazz Band kuwa na utamu wa pekee kabisa. Ufundi wa Satchmo unaweza kusikika katika nyimbo kama Mganga no 1 na 2, Blandina au Siku Yetu la Leo.

Kule Tabora  marehemu Kasim Kaluwona alikuwa na staili tofauti ya upigaji wa gitaa la rythm uliyoifanya Tabora Jazz kuwa na staili yake peke yake, nyimbo kama Asha na Dada Lemmy ni kati ya nyimbo nyingi zilizoonyesha  ubora  wa Kasim Karuwona.

Charles Kasembe, kijana aliyetokea Masasi aliweza kuja na staili yake ambayo iliweza kuipaisha bendi ya Morogoro Jazz Band, ukisikiliza wimbo wa Wajomba Wamechacha, unaweza kuona ubora wa upigaji na jinsi ulivyokuwa tofauti na wapiga gitaa la rhythm wengine ambao nimewataja.

Wakati huohuo huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakati huo ikiitwa Zaire, kulikuwa na mipigo mbalimbali ya gitaa la ridhim, ila kitu kipya kikaanzishwa ambapo katika ufungaji wa nyuzi za gitaa hilo, badala ya kufunga nyuzi katika mfumo uliozoeleka wa uzi wa kwanza mpaka wa sita nyuzi hizi zikiwa na unene tofauti, kuanzia uzi wa kwanza ambao ulikuwa  mwembamba, hadi uzi wa sita uliokuwa mnene kuliko zote, wao wakaondoa uzi wanne na kuweka uzi wa kwanza, hivyo gitaa likawa na nyuzi za kwanza mbili.

Mpiga gitaa la ridhim wa bendi ya Lipua Lipua, Vata Mombasa alitumia sana staili hii na kuweza kuleta sauti mpya iliyoigwa Afrika nzima. Wakati huo bendi nyingine kutoka hukohuko Zaire, Orchestra Kiam, wakawa wanajivunia kupiga gitaa la rydhm kwa spidi kali sana,vibao kama Kamiki, Bomoto ni ushahidi wa kazi hizo. 

Utamu wa ufungaji wa nyuzi kwa staili hii uliweza kusikika vizuri katika gitaa la ridhim lililopigwa mwanzo kabisa wa wimbo Andoya wa Orchestra Le Kamale.
Umuhimu wa gitaa la ridhim ulikuwa ukionekana kwa bendi nyingi kuwa na mtindo wa ‘kuachia ridhim’, huo ulikuwa ni mpangilio ambapo gitaa la ridhim liliachwa lipige peke yake wakati magitaa mengine yakiwa kimya. 

Mtindo huu ulipendwa sana na wapenzi wa muziki. Utaratibu huu umerudi kwa njia ya ajabu sana, bendi nyingi za  taarab vimeanza ‘kuachia ridhim’ lakini kwa kuwa bendi hizo hazitumii tena gitaa, jukumu hili linafanywa na mpiga solo, tena vipande vingi vinavyopigwa ni vile vilivyopigwa na bendi za zamani!!  matokeo ni yaleyale, wapenzi wa muziki hupanda mzuka na kucheza sana wakati wa kipindi hicho.

Kwa ujumla siku hizi bendi nyingi za dansi hazitilii umuhimu tena gitaa la ridhim, kinanda kimechukua nafasi ya gitaa hili. Kuna bendi ambazo zinalo gitaa la rythm lakini kwa mfumo wa sasa wa muimbaji kuchukua nafasi kubwa ya wimbo gitaa hilo huwa hata halisikiki. Lakini hakika mwanamuziki atakayefanikiwa kubuni njia nyingine ya kutumia gitaa la ridhim anaweza akawateka wapenzi wapya wa muziki wa dansi.