Watoto wanaotumikishwa Zanzibar kutoka Bara waanza kusakwa

Muktasari:
- Katika ukaguzi uliofanyika kwa siku nne, jumla ya watoto 40 wamekamatwa wakiingia kisiwani humo kwa ajili ya kufanya kazi.
Unguja. Katika kukabiliana na tatizo la usafirishaji wa watoto kutoka Bara kwenda Zanzibar kwa ajili ya ajira za utotoni, Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama imeanza kufanya ukaguzi kwenye meli zinapowasili katika Bandari ya Malindi ili kubaini uwapo wa watoto hao.
Katika operesheni iliyofanyika kwa siku nne kuanzia Aprili 18 hadi 21 mwaka huu, jumla ya watoto 40 wamebainika kusafirishwa kwa ajili ya kwenda kufanya kazi mbalimbali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff ameeleza hayo Aprili 23, 2024 wakati akieleza mpango huo ambao unalenga kuzuia wimbi la uingiaji wa watoto kutoka Bara wanaokwenda visiwani humo kutumikishwa.
"Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kufanya jitihada za kupinga ajira za watoto ambapo imekuwa kikwazo katika kukuza maendeleo yao na Taifa kwa ujumla," amesema.
Kwa mujibu wa waziri huyo, miongoni mwa kazi ambazo zimebainika kufanywa na watoto hao ni pamoja na kutumikishwa kingono, kazi za nyumbani, kukuza bidhaa mbalimbali mitaani kama vile karanga, mayai na nyinginezo.
Amesema kutokana na hali hiyo, kwa sasa wanataka kuanzishwa dawati la kupinga ajira za watoto bandarini ambalo litajumuisha maofisa kazi, ustawi, Jeshi la Polisi, uhamiaji ili kuzuia watoto hao kuingia nchini.
"Kuwepo kwa dawati la kupinga ajira za watoto litakalokuwa na upande wa Dar es Salaam ambao litazuia kuingia huku au kama wakiingia kwa bahati mbaya basi warudishwe kwa kupokelewa na dawati hilo, ili kuhakikisha wanarudishwa maeneo waliyotoka," amesema.
Amesema kitendo cha kuwatumikisha watoto hakikubaliki kisheria kwani kinasababisha kuwakosesha haki zao za msingi za kibinaadamu ikiwemo elimu pamoja na kudhoofisha nguvu kazi ya Taifa la baadaye.
Waziri Shariff amesema takwimu za mwaka 2020/2021 zinaonesha kuwa asilimia 62.2 ya watoto wa kiume ndio wanaoathirika zaidi na ajira hizo.
Bila kutaja idadi kamili ya takwimu hizo, amesema maeneo yanayoongoza ni Mkoa wa Kusini Unguja asilimia 12.2, Kusini Pemba asilimia sita na Mkoa wa Mjini Magharibi asilimia 2.4.
Ofisi imeweka sheria na sera madhubuti zinazopinga ajira za watoto na kuendelea kuimarisha mifumo ya kusimamia na kutekeleza sheria hizo, ikiwemo sheria ya ajira namba 11 ya mwaka 2005 ambayo inakataza ajira za kuwatumikisha watoto.
Naye Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi na Uwezeshaji, Halima Maulid Salum amezitaka taasisi mbalimbali kushirikiana kwa pamoja katika kuliondoa tatizo la ajira za watoto, zinazorudisha nyuma maendeleo yao.
"Tumejipanga kuhakikisha wanaowatumikisha watoto wanachukuliwa hatua na wale ambao wanatakiwa kwenda shule watarejeshwa," amesema.
Khadija Khamis ni mwanaharakati wa masuala ya haki za watoto Zanzibar, amesema wanaowafanyisha kazi watoto wanapaswa kuchukuliwa hatua kali, lakini tatizo hilo linaendelea kwa sababu hakuna hatua zinazochukuliwa.
"Iwapo wakionekana watu wamechukuliwa hatua inaweza ikasaidia na watu wakashtuka kuona kwamba hili jambo lipo kweli," amesema.