Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sintofahamu daftari la wapigakura, ZEC yajibu

Maofisa ya uandikishaji katika tume ya uchaguzi Zanzibar ( ZEC ) wakiendelea kutoa huduma kwa wananchi wanaofika kujiandikisha katika wilaya ya chakechake. Picha na Muhammed Khamis

Muktasari:

  • Hatua ya ya uandikishaji wapiga kura wapya kwa awamu ya kwanza itaendelea tena katika Wilaya ya Mkoani mnamo Desemba 12 hadi 14, 2023 kwa Kisiwa cha Pemba.

Pemba. Baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzani wameilalamikia Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wakidai kukataliwa kuandikishwa upya katika daftari la wapigakura.

Malalamiko hayo yamekuja wakati ZEC ikiendelea na uandikishaji wapiga kura wapya kwa awamu ya kwanza na itaendelea tena katika Wilaya ya Mkoani Desemba 12 hadi 14, 2023 kwa Kisiwa cha Pemba.

Hata hivyo, akizungumzia changamoto hizo leo Desemba 9, Mkurugenzi wa ZEC Faina Idarous amesema hakuna mtu aliyepingwa kuandikishwa iwapo amekidhi matakwa yote ya kisheria.

Amesema uandikishaji huo wa kisasa unatumia mashine maalumu ambazo kuna wakati nazo huchoka na ndio maama hushindwa kusoma alama za vidole kwa muda.

Ameongeza kuwa, baadhi ya wananchi wanaokwenda kuandikisha wanakwenda wakiwa na jasho mikononi hivyo kushindwa kuonekana mpaka pale wanaposafishwa.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Desemba 9, Katibu wa Mkoa Chama cha ACT-Wazalendo, Saleh Nassor Juma amesema wanachama wao wengi wamekuwa wakikataliwa wanapokwenda kujiandikisha kwa visingizo vya ajabu.


"Kwa mfano katika maeneo mbalimbali ya Chakechake, masheha wanawakataa wanachama wetu wenye vitambulisho halali vilivyotolewa na Serikali wamekuwa wakiwapa majibu rahisi na kutowatambua," amesema.

Pia, katibu huyo amelalamikia mifumo ya usajili ya wapigakura wapya na kueleza kuwa haifai na inapaswa kutazamwa kwa umakini zaidi.

Amesema kwenye mashine hizo kwa mara kadhaa zimekuwa zikishindwa kusoma alama za vidole na hata kukataa kusoma taarifa za vitambulisho (ZAN ID) na mara inapotokea hivyo, wananchi hutakiwa kurudi na kuja siku nyingine.

Mwenyekiti wa Chama cha AFP, Said Soud amesema licha ya kuwa uandikishaji huo upo kwa matakwa ya kisheria lakini utaratibu unaotumika haufuati sheria.

Amesema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 wapigakura zaidi ya 80,000 walitolewa kwenye daftari na wanapokwenda kuandikisha awamu hii pia wanakataliwa tena licha ya kuwa na vitambulisho.

Majid Awadhi wa shehia ya Wara wilayani Chakechake, amesema yeye ni miongoni mwa waliokataliwa kuandikishwa.

Amesema licha ya kuwa na kitambulisho cha ZAN ID lakini sheha wa shehia yake amemkataa akidai kuwa yeye si mkazi halisi wa eneo hilo.