Rais Mwinyi ayaonya mashirika ya umma ‘mzigo’
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akizungumza wakati akifungua jukwaa la Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi Unguja Zanzibar.
Muktasari:
- Imeelezwa kuwa, bado yapo mashirika ya umma yanayolipwa mishahara na kuendeshwa kwa fedha za Serikali jambo alilosema limepitwa na wakati.
Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali haitakuwa tayari kuendelea kubeba mashirika ya umma yanayoshindwa kujiendesha na kuendelea kutegemea ruzuku kutoka serikalini.
Amesema bado yapo mashirika ya umma yanayolipwa mishahara na kuendeshwa kwa fedha za Serikali jambo alilosema limepitwa na wakati, huku akizitaka taasisi hizo kujipanga na kujiendesha kwa tija na faida.
Dk Mwinyi amesema hayo jana Jumamosi, Mei 23, 2026 wakati akifungua Jukwaa la Wenyeviti na Maofisa Watendaji Wakuu Zanzibar lililoshirikisha viongozi waandamizi kutoka serikalini, taasisi za fedha, mashirika binafsi na taasisi za maendeleo kujadili ushirikiano wa kikanda, ukuaji wa uchumi na fursa za uwekezaji na kufunguliwa.
Amesema Serikali itatoa muda kwa mashirika hayo kufanya mageuzi ya kiutendaji na yale yatakayoshindwa kujiendesha Serikali haitakuwa tayari kuendelea nayo.
Aidha, amesisitiza kuendelea kwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 pamoja na miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo ujenzi na uimarishaji wa bandari, viwanja vya ndege, viwanja vya michezo na miundombinu ya barabara ili kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha uchumi wa kisasa na endelevu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Equity Group, Dk James Mwangi amesemaviongozi wa biashara barani Afrika wanatakiwa kuharakisha ukuaji endelevu wa uchumi kwa kuwekeza katika uongozi unaoleta mabadiliko, ubunifu, huduma jumuishi za kifedha na ushirikiano wa kimkakati.
Dk Mwangi amesema hayo wakati akiwasilisha mada mbili za ngazi ya juu zilizolenga kuonesha nafasi ya uongozi, teknolojia na ushirikiano katika kujenga taasisi imara na uchumi shindani.
Amesema Zanzibar ina nafasi ya kipekee ya kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji, biashara, nishati na uwekezaji, kinachoweza kuiunganisha Afrika na masoko makubwa yanayoibukia duniani kama India na China.
“Mfumo wa uchumi wa dunia unapitia mabadiliko makubwa, na maeneo yatakayojipanga kimkakati leo ndiyo yatakayoshiriki kwa nguvu katika kuunda uchumi wa kesho,” amesema Dk Mwangi.
Amesema uwezo wa nishati jadidifu, rasilimali za madini ya kimkakati na fursa zinazoendelea kujitokeza katika biashara, vinaipa Afrika nafasi muhimu katika uchumi wa dunia.
Amesisitiza Zanzibar ina uwezo wa kuwa kitovu cha usafirishaji, biashara, nishati na uwekezaji, sawa na nafasi ambayo Singapore imekuwa nayo katika kuunganisha mifumo ya biashara na usafirishaji Kusini Mashariki mwa Asia.
Katika mada yake kuu iliyobeba ujumbe wa: “Utekelezaji wa Mkakati kwa Kasi; Kuharakisha Ukuaji Endelevu Kupitia Uongozi wa Mageuzi na Ushirikiano wa Kimkakati,” Dk Mwangi amesema safari ya mageuzi ya Equity Group hadi kuwa moja ya taasisi kubwa za huduma jumuishi za kifedha barani Afrika, inahudumia wateja milioni 23 katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Amesisitiza ubunifu, ujumuishaji, uendelevu, teknolojia na ushirikiano wa kimkakati kuwa nguzo muhimu katika kujenga taasisi imara, zenye uwezo wa kuhimili mabadiliko na kuendelea kutoa thamani kwa jamii na uchumi kwa muda mrefu.
Dk Mwangi pia ameeleza namna Equity Group ilivyovunja vikwazo vya huduma za kibenki kwa kurahisisha masharti ya kufungua akaunti, kuondoa kima cha chini cha salio na kutumia teknolojia kupanua huduma za kifedha kwa jamii ambazo hapo awali hazikufikiwa kikamilifu na mfumo rasmi wa kifedha.
“Uongozi wa leo unahitaji ujasiri wa kubadili mifumo iliyozoeleka, kasi katika utekelezaji na dhamira ya kujenga ustawi wa pamoja,” amesema Dk Mwangi.
Dk Mwangi amesisitiza dhamira ya Equity Group katika kutekeleza mkakati wa triple bottom line, unaolenga kuunganisha faida ya kibiashara na matokeo chanya kwa jamii na mazingira.
Amesema mkakati huo unaendelea kuongoza uwekezaji na huduma za taasisi hiyo katika masoko yake mbalimbali barani Afrika.