Othman rasmi kumvaa Mwinyi Uchaguzi mkuu

Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud akipokea fomu ya kuwania Urais wa Zanzibar kutoka kwa Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya chama hicho, Mhene Said Rashid makao makuu ya chama hicho Vuga Unguja. Picha na Jesse Mikofu
Muktasari:
- Dk Hussein Mwinyi na Rais Samia Suluhu Hassan, walipitishwa katika mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika Januari 18 na 19 mwaka huu mjini Dodoma kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu.
Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud amechukua fomu ya kugombea Urais kupitia chama hicho katika uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Hatua ya Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kuchukua fomu hiyo, ni dhahiri anakwenda kuchuana na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ambaye chama chake cha Mapinduzi (CCM) tayari kimeshampitisha kuwania nafasi hiyo kwa awamu ya pili.
Dk Mwinyi na Rais Samia Suluhu Hassan, walipitishwa katika mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika Januari 18 na 19 mwaka huu mjini Dodoma kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu.
Katika uchaguzi huo pamoja na marais wa Tanzania Bara na visiwani, watachaguliwa wabunge, wawakilishi na madiwani.
Othman amechukua fomu hiyo leo Aprili 13, 2025 Makao Makuu ya ofisi za chama hicho Vuga Zanzibar, ambapo amekabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya chama hicho, Mhene Said Rashid na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho.
Pamoja na fomu hiyo, pia Othman amekabidhiwa Katiba ya Zanzibar na kanuni za chama ambavyo kwa mujibu wa Mhene, vitamwongoza kujaza fomu hiyo kwa usahihi.
“Nakukabidhi fomu hii, Katiba na kanuni za chama vitakuongoza kujaza fomu hii, na mwisho wa kurejesha fomu hii ni Aprili 17, 2025 saa 10:00 jioni, usije kusahau,” amesema Mhene.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu hiyo, Othman amesema hiyo ni nafasi muhimu katika nchi na chama chake cha ACT Wazalendo.
“Leo nimekuja kuchukua fomu kwasababu ni sehemu muhimu ya utaratibu wetu ndani ya chama, uchaguzi ni mchakato na kuna sehemu unaanzia, kabla hujaingia kwenye bahari kubwa ambayo ndio ile ya kitaifa, kwanza kuna mchakato wetu ndani ya chama,” amesema Othman.
Amepongeza chombo kinachosimamia mchakato huo ndani ya chama akisema maandalizi yameenda vizuri katika ngazi zingine za udiwani na uwakilishi kwa mikoa yote.
“Kwa hiyo niwashukuru sana kwa moyo wenu kushirikiana na mimi katika mchakato huu,” amesema kiongozi huyo.
Hata hivyo, amesema leo sio siku yake ya kuzungumza, bali ni ya kuchukua fomu, badala yake mazungumzo rasmi na vyombo vya habari atayafanya pindi atakaporejesha fomi hiyo Jumatano Aprili 16, 2025.
“Nawashukuru wanachama na viongozi wote mliojitokeza kunisindikisa kuchukua fomu ya kuwania nafasi hii muhimu sana kwa Taifa, “ amesema Othuman.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Omar Ali Shekha amesema katika nafasi hizo kila mtu yupo huru kugombea nafasi yoyote ambazo zinatangazwa Zanzibar na Tanzania bara.
“Kwahiyo kila mwanachama mwenye sifa aliyekamilisha yupo huru kugombea nafasi yoyote katika chama,” amesema.
Mhene amesema mchakato wa kuchukua fomu unaendelea vyema tangu pazia lake lifunguliwe Aprili mosi kwa ngazi ya ubunge, uwakilishi na udiwani na kukamilika Aprili 10, kuanzia Aprili 12 hadi 17 ni kwa ngazi ya Urais.
Akizungumzia gharama za uchukuaji wa fomu kwa ngazi ya ubunge na uwakilishi, Mhene amesema ni Sh100,000, udiwani Sh30,000 na kwa mgombea Urais ni Sh1 milioni.
Mbali na kuweka mgombea urais Zanzibar, Naibu katibu mkuu huyo amesema wanatarajia pia kusimamisha wagombea kwa nafasi zote kuanzia urais hadi udiwani kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo, amesema kwa upande wa Tanzania Bara kwa sasa wanaelekeza nguvu kwenye ajenda yao mabadiliko ya Katiba kisha mambo mengine yataendelea.
“Wengine watajiuliza mbona tumesaini kanuni, ndio tumesaini lakini sio kwamba tumekubaliana nazo, tumesaini kwa sababu utaratibu ndivyo ulivyo na hatua nyingine zitafuata za kupinga yale ambayo tunahisi sio sahihi, hatususii tunasaini na hatua nyingine zitafuata, kama ni kwenda mahakamani, sisi hatuachi fursa yoyote,” amesema kiongozi huyo.
Jana Aprili 12, 2025 vyama 18 vilisaini kanuni za uchaguzi huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimegomea kuzisaini na tayari Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeshatamka bayana kuwa hakitaweza kushiriki uchaguzi wowote kwa kipindi cha miaka mitano.
Wakati huo huo, Mhene amesema amefurahishwa na kishindo kikubwa cha wanawake ndani ya ACT Wazalendo ambao wameshaonesha nia ya kutaka kuingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi huo.
Hata hivyo, hakufafanua idadi ya waliojitokeza katika majimbo yote kwa ujumla akisema mchakato bado unaendelea hatua za ndani.
Kwa mujibu wa Mhene, baada ya kukamilisha urejeshaji wa fomu utaanza mchakato wa kura za maoni, vikao vya uteuzi na Julai watakuwa wamekamilisha hatua zote za kuwapata wapeperusha bendera ya chama chao katika uchaguzi mkuu.