Mashine kupima nguvu ya lenzi ya jicho kwa watoto yatua Z’bar

Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui (katikati) akikabidhi mashine ya kupimia nguvu ya jicho wakati wa upasuaji wa kutolewa mtoto wa jicho Zanzibar
Muktasari:
- Mashine hiyo itatumika katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja.
Unguja. Wizara ya Afya Zanzibar imekabidhi mashine ya kufanyia uchunguzi na kupimia kiwango cha lenzi wakati wa kufanya upasuaji wa jicho kwa watoto, yenye thamani ya Sh75 milioni.
Mashine hiyo itatumika katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja.
Akikabidhi mashine hiyo kwa uongozi wa kitengo cha macho leo Jumapili, Machi 9, 2025 Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui amesema mashine hiyo itasaidia kujua uhalisia wa nguvu ya lenzi wakati wa upasuaji wa kutolewa mtoto wa jicho.
“Mashine hii itasaidia kujua uhalisia wa nguvu ya lensi, mtoto atawekewa wakati upasuaji wa kutolewa mtoto wa jicho," amesema Mazrui.
Pia, Mazrui amesema mashine hiyo inasaidia kutambua matatizo mengine ya macho kabla ya kufanyiwa upasuaji.
Mashine hiyo imeletwa ikiwa ni agizo la Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi alilolitoa hivi karibuni ili wananchi wapate huduma hizo bila usumbufu.
Mratibu wa huduma za Afya ya macho Zanzibar, Dk Fatma Juma Omar ameishukuru Serikali kwa kuwapatia mashine hiyo itakayosaidia katika kuimarisha huduma za afya ya macho hasa kwa watoto.
Amesema uwepo wa mashine hiyo utawasaidia kuondokana na upofu wa macho usiokuwa wa lazima.
Daktari Dhamana (mfawadhi/mkuu) wa Kitengo cha Huduma za Macho hospitalini hapo, Dk Ahmed Mohamed Muumin amesema kupatikana kwa kifaa hicho kutaimarisha huduma bora za macho katika hospitali hiyo.
"Uwepo wa mashine hii itasaidia kuwapatia huduma watoto wenye matatizo mbalimbali ya macho yakiwamo ya mtoto wa jicho," amesema Dk Muumin.
Katika hatua nyingine, Waziri Mazrui amefanya mazungumzo na taasisi ya JIPD ya nchini China inayoshughulikia maradhi yasiyopewa kipaumbele kikiwamo kichocho.
Waziri Mazrui amewashukuru kwa msaada mkubwa wanaosaidia katika sekta ya afya kisiwani Pemba.
Amesema jitihada kubwa zimeelekezwa kisiwani Pemba katika kukabiliana maradhi hayo kwa kufanya mambo mbalimbali ikiwamo kutoa elimu kwa jamii, kuwapima watoto shuleni pamoja na kuwapatia dawa za kichocho.