Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kanuni kuwabana wawekezaji kutoa CSR mbioni Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Hoteli ya Matemwe Attitude  ikiwa ni muendelezo wa Shamrashamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Muktasari:

  • Licha ya kutungwa sheria ya taaisisi kuwajibika kwa jamii ya mwaka 2023 haijaanza kutumika kutokana na kutokamilika kwa kanuni na miongozo.

Unguja. Wakati zikiandaliwa kanuni kuwabana  wawekezaji kuwajibika kwa jamii (CSR) katika maeneo wanayowekeza, Serikali imesema inatambua mchango wa sekta binafsi katika kukuza na kuendeleza uwekezaji, hivyo itahakikisha inaweka mazingira wezeshi kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema hayo leo  Januari Mosi, 2026 wakati wa uzinduzi wa mradi wa hoteli ya Matemwe Attitude iliyopo Kijini, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Uzinduzi huo ni mwendelezo wa shamrashamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema kuimarika kwa sekta ya uwekezaji ndiko kunakowavutia wawekezaji kuendelea kuwekeza Zanzibar, jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa ajira kwa wananchi wazawa na kukuza uchumi kwa jamii inayowazunguka.

Amesema jitihada hizo zimetoa matokeo chanya ikiwamo kuongezeka miradi ya uwekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo za utalii, ujenzi, nishati na kuzalisha fursa nyingi za ajira.

"Takwimu za Serikali zinaonyesha zaidi ya miradi ya uwekezaji 588 imesajiliwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ikiwa na thamani ya Dola bilioni 6.9 za Marekani na kuzalisha ajira 28,695 kwa wazawa," amesema.

Hemed amesema amefurahishwa na kauli ya mwekezaji wa hoteli hiyo kuahidi kuwa kipaumbele chake kitakuwa kuhakikisha wanaweka mazingira bora katika maeneo yanayowazunguka wananchi sambamba na kuigusa jamii moja kwa moja katika nyanja mbalimbali, lengo likiwa kuhakikisha ustawi bora wa wananchi wa Kijini na Mkoa wa Kaskazini kwa ujumla.

Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wawekezaji ili waendelee kuja kuwekeza Zanzibar.

Amewasisitiza wananchi kutoa ushirikiano kwa wawekezaji na kulinda mila na tamaduni za Kizanzibari.

Kiongozi huyo amewataka wananchi walioajiriwa hotelini hapo kufanya kazi kwa umakini, uadilifu, kufuata sheria za kazi na maelekezo ya waajiri wao.

Akizungunza kuhusu Mapinduzi, Hemed amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikano, kuyalinda, kuyadumisha na kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 ili kuendelea kupata maendeleo nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Kazi na Uwekezaji Zanzibar, Sharif Ali Sharif amesema wizara inaandaa kanuni ya ushirikiano na uwajibikaji katika jamii ambayo itawabana wawekezaji kujisogeza katika jamii wanayowekeza miradi mbalimbali ili nao waweze kunufaika na uwekezaji unaofanyika katika maeneo yao.

Amesema tayari kuna sheria ya mwaka 2023 ya CSR lakini bado haijatungiwa kanuni na miongozo ili kuanza kutekelezwa.

"Tunataka kutengeneza kanuni ili kuwabana wawekezaji kuwajibika kwa jamii katika huduma za shule, maji na nyinginezo, kanuni hizo zipo mbioni kukamilika," amesema.

Shariff amesema atahakikisha wafanyakazi wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa) wanafanya kazi kwa wakati na weledi mkubwa kwa viwango vinavyotakiwa ili kuhakikisha sekta ya uwekezaji inazidi kukua Zanzibar.

Mkurugenzi Mkuu wa Hoteli hiyo, Ravian Unthiah kutoka Mauritius, amesema wameamua kuwekeza Zanzibar kutokana na amani na utulivu uliopo.

Mazingira mazuri ya uwekezaji na wananchi kuwa tayari kutoa ushirikiano kwa wawekezaji ni sababu nyingine aliyosema imemvutia mwekezaji huyo, akiahidi kuisaidia jamii katika utunzaji wa mazingira na huduma muhimu za kijamii.

Amesema mradi huo utazalisha ajira zaidi ya 190 kwa wananchi wa Kijini na Mkoa wa Kaskazini kwa ujumla.

Wafanyakazi hao tayari wameshapatiwa mafunzo na ujuzi kulingana na kada wanazozifanyia kazi ili kutoa huduma bora kwa wageni na wazawa watakaofika hotelini hapo.

Amesema Matemwe Attitude Group ina zaidi ya hoteli tisa zenye madaraja tofauti.

Mkurugenzi wa Zipa, Saad Saleh Mohamed, amesema uwekezaji huo umegharimu Dola 22 milioni (zaidi ya Sh56 bilioni).