Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hili ndilo Baraza Kivuli la ACT-Wazalendo Zanzibar


Muktasari:

  • Weteule waeleza mikakati yao katika usimamizi wa sera

Unguja. Chama cha ACT-Wazalendo kimetangaza baraza la wasemaji wa kisekta Zanzibar likiwa na jukumu la kufuatilia utendaji wa Serikali kisera, uchumi na ustawi wa jamii.

Majukumu mengine ni kuona jinsi gani sera, sheria, maamuzi na usimamizi wa shughuli za Serikali unaathiri maendeleo na mustakabali wa nchi wa usalama wa raia, utengamano wa kijamii, haki, amani na utulivu.

Hatua hiyo imekuja baada ya kupata uzoefu wa baraza kama hilo kwa upande wa Tanzania Bara.

Baraza hilo lenye sekta 16 lililoundwa na Kiongozi wa Chama hicho, Dorothy Semu, baada ya kushauriana na viongozi wenzake, limetangazwa leo Septemba 6, 2024 na Mwenyekiti wa chama hicho, Othman Masoud.

Akitangaza baraza hilo Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema muundo wake umezingatia sekta zilizopo Zanzibar bila kujali majina na muundo wa wizara zilizopo Zanzibar kwa sasa.

“Imezingatiwa zaidi mtazamo wa chama chetu juu usimamizi wa sekta hizo kwa ufanisi. Hivyo, baraza hilo litakuwa na muundo wa wizara za kisekta 16 kwa ujumla wake,” amesema.

Baraza hilo litaongozwa na Mkuu na Kiongozi wa Baraza ambalo chini ya Ofisi yake atakuwepo msemaji wa kisekta na naibu wake. Pia, Katibu Kiongozi wa Baraza atakuwa chini ya ofisi hiyo.

Kwa mujibu wa Othman, jukumu kubwa la baraza la wasemaji wa kisekta ni kufuatilia utendaji wa Serikali kisera, kisheria na kiutendaji na kuona jinsi gani sera, sheria, maamuzi na usimamizi wa shughuli za Serikali unaathiri maendeleo na mustakabali wa nchi na wananchi, uchumi, ustawi wa jamii, usalama wa raia, utengamano wa kijamii, haki, amani na utulivu wa nchi.

Pia, litafuatilia mambo hayo kwa kuzingatia masilahi ya wananchi hasa katika matumizi ya madaraka, rasilimali na fursa za nchi ili kuona kwamba malengo muhimu yaliyoelezwa na Katiba ya Zanzibar na Katiba ya chama hicho yanatimizwa kwa ukamilifu.

Amesema miongoni mwa mambo yatakayopewa kipaumbele maalumu katika kazi za baraza ni ubora wa sera za kiuchumi na fedha, ufanisi katika huduma za kijamii ikiwemo afya na elimu, haki za raia katika ardhi na upatikanaji wa haki zao katika vyombo vya umma na vya kutoa haki.

Nyingine ni mapambano dhidi ya ufisadi na utengamano wa kijamii, amani na utulivu. 

“Hapa nitanabahishe kuwa kuundwa kwa baraza hili hakutaondoa utaratibu wa chama wa mikutano ya hadhara, baraza litakuwa tu ziada ya juhudi za chama kuwa sauti ya wananchi,” amesema.

Othman amesema uundaji wa baraza hilo la kisekta umetokana na Katiba ya Zanzibar kifungu cha 9(2)(a) ambacho kinatamka bayana kwamba mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe ambayo nguvu na uwezo wote wa Serikali kufuatana na Katiba utatokana na wananchi. 


Pia, kifungu cha 10 cha Katiba kimeweka bayana malengo muhimu ya kisiasa ya nchi, miongoni mwa hayo, kama yalivyoelezwa katika kifungu cha 10(b) ni kuondosha kabisa vitendo vya rushwa na utumiaji mbaya wa cheo dhidi ya umma kwa wale wote walio na madaraka.

Wakati huohuo ibara ya 7 ya Katiba ya Chama cha ACT-Wazalendo inaeleza malengo na madhumuni ya chama ambayo inakiamuru chama kupigania takribani malengo yote yaliyoainishwa katika Katiba ya Zanzibar katika kazi yake ya kuwa ni sauti ya watu.


Walioteliwa

Mkuu wa wasemaji wa kisekta na baraza ni Ismail Jussa, Katibu akiwa Seif Hamad Suleiman.

Katika ofisi ya mkuu wa kisekta (mawaziri wa nchi) msemaji ni Hamad Mussa Yussuf na naibu msemaji ni Mohamed Bussara.

Sekta ya Fedha, Uchumi, na Dira ya Maendeleo msemaji ni Profesa Omar Fakih Hamad na naibu wake ni Miza Bakari Haji.

Utumishi wa Umma na Maadili ya Uongozi msemaji ni Hassan Jani Masoud, naibu msemaji ni Halima Abbas.

Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Mipango Miji, msemaji ni Jabir Idrisa, huku naibu msemaji akiwa Nahoda Khamis.

Biashara, Uwekezaji na Uwezeshaji Kiuchumi msemaji wake ni Mahmoud Shineni, naibu akiwa Salma Mbarouk Abdalla

Katiba na Sheria, msemaji ni Khalfan Amour Mohamed na naibu ni Biole Mohamed Omar.

Kilimo, Ufugaji na Uvuvi msemaji ni Abdilahi Jihad Hassan, naibu ni Makiye Juma Ali.

Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati msemaji ni Rashid Ali Abdalla; naibu ni Salma Mohamed Ali.

Mafuta na Gesi Asilia msemaji ni Said Ali Mbarouk, huku naibu ni Rashid Habib Ali.

Mawasiliano na Usafirishaji msemaji ni Seif Khamis Mohamed, na naibu wake ni Nassor Marhoun.

Utalii na Urithi wa Taifa msemaji ni Dk Haji Ali Haji Mbarouk, huku naibu ni Jina Suleiman Hassan.

Elimu, Ubunifu na Stadi za Ufundi msemaji ni Dk Mohamed Ali Suleiman na naibu wake ni Suleiman Ali Seif.

Kwa upande wa Afya, msemaji ni Dk Suleiman Maulid, naibu ni Janeth Fussi.

Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, msemaji ni Ally Saleh, huku naibu msemaji ni Humoud Ahmed Said.

Maendeleo ya Wanawake, Watoto na Makundi Maalumu ni msemaji ni Halima Ibrahim Mohamed na naibu msemaji ni Hidaya Yussuf Ali.

Vijana na Ajira, msemaji ni Abdalla Haji Shaame na naibu ni Shaaban Khamis Abdalla (Chonja).


Vipaumbele vya wateule

Wakizungumza kuhusu uteuzi huo, baadhi ya wateule wamesema watahakikisha wanasimamia majukumu hayo kwa weledi ili kufikia malengo na matamanio ya wananchi, huku wakiomba ushirikiano wa kila mmoja.

Msemaji sekta ya Fedha, Uchumi na Dira ya Maendeleo, Profesa Omar Fakih Hamad amesema anajiandaa kwani wameona upungufu mkubwa katika utekelezaji wa mipango ya Serikali.

Amesema atahakikisha wanaunganisha kati ya ilani wanayoitekeleza kwa pamoja ya CCM na kuangalia mazuri yaliyopo kwenye ACT-Wazalendo na kuangalia ahadi zilizotolewa lakini hazijatekelezwa.

“Kumekuwa na kero kubwa sera za kodi, kuna kodi nyingi zimeingizwa tunaamini wananchi zinawakera kwa hiyo tutakwenda kuanza na haya,” amesema Profesa Omar ambaye ni mwakilishi katika Baraza la Wawakilishi.

Naibu msemaji wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, Makiye Juma Ali amesema, “tunakwenda kusimamia CCM na ilani zao lakini kero za wananchi kwenye sekta hiyo na namna ya kuwasaidia.”

Idrisa Jabir, aliyeteuliwa kuwa msemaji wa sekta ya Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Mipango Miji amesema sekta hiyo haina uwazi kwa hiyo anakwenda kuyasimamia hayo.

“Ukifanya mambo yanayohusu wananchi lakini hawapati taarifa huku ni kukengeuka kwa hiyo tunaomba ushirikiano na sisi tutafanya kazi kwa mujibu wa utaratibu uliopo,” amesema.