Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT-Wazalendo wataka mabadiliko Jeshi la Polisi

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman amjibu Kamishna wa Polisi Zanzibar.

Unguja. Chama cha ACT-Wazalendo kimemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai ya kubadilisha mfumo wa Jeshi la Polisi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Chama hicho kimetoa kauli hiyo kutokana na ilichodai kuendelea kuwapo matamshi kutoka kwa polisi dhidi ya demokrasia nchini.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari makao makuu ya ACT-Wazalendo eneo la Vuga, Zanzibar leo Alhamisi Agosti 22, 2024, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Othman Masoud amedai iwapo hatua za haraka zisipochukuliwa kuna maafa makubwa yatatokea.

Rais Samia aliunda Tume ya Haki Jinai iliyofanya kazi kupitia vyombo vya usalama na haki vikiwamo Polisi, Magereza na Mahakama chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Othman Chande.

Amesema miongoni mwa taarifa ya ripoti hiyo ilionyesha malalamiko makubwa chini ya mfumo mzima wa polisi na kupendekeza kufanyiwa marekebisho.

Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ametumia fursa hiyo kumjibu Kamishna wa Polisi Hamad Khami Hamad aliyoitoa hivi karibuni akiwataka wanasiasa kuchunga ndimi zao na kuacha kutumia kauli za kejeli, dharau na tuhuma kwa viongozi wakuu wa Serikali ili kudumisha amani.

Othman amesema kauli ya Kamishna Hamad inalenga upande mmoja, akisema hata kwenye mkutano wake na waandishi wa habari alitoa mfano wa moja ya mkutano wa chama hicho uliofanyika Pemba, huku akidai aliacha matusi ya hadharani yaliyotolewa na viongozi wakuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Yapo mengi yanayowahusu polisi wenyewe, lakini tatizo kubwa ni mifumo, kwa hiyo tunamuomba Rais Samia achukue hatua za haraka kutekeleza ripoti ya Tume ya Haki Jinai kubadilisha mfumo wa Jeshi la Polisi, lakini akiacha ukawa hivi mpaka uchaguzi huenda maafa yakawa makubwa katika uchaguzi wa mwaka 2025,” amesema.

Amesema kwa jinsi mfumo ulivyo sasa, baadhi ya polisi wanapokea maelezo kutoka kwa wanasiasa japo amesema wapo wanaofanya kazi kwa weledi.


Kauli ya Kamishna Hamad

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamad Khamis Hamad amevitaka vyama vya siasa nchini kutotumia majukwaa hayo kuvunjiana heshima na kutumia matamshi yenye kukuza chuki na kuchochea uvunjifu wa amani.

Bila kutaja chama kwenye taarifa yake, alitoa mfano wa moja ya mkutano wa ACT-Wazalendo uliofanyika Pemba alipoulizwa swali na mwandishi wa habari kueleza baadhi ya matukio yanayolenga kuhamasisha chuki.

"Uhuru wa kuzungumza ni haki muhimu katika kukuza demokrasia, hivyo lazima itekelezwe kwa uwajibikaji wa kuzingatia umuhimu wa kudumisha amani na utulivu na utawala wa sheria," amesema Kamishna Hamad.

Amesema Jeshi la Polisi linaheshimu haki za viongozi wa vyama vya siasa kuikosoa Serikali, kushawishi wafuasi wa vyama kujaribu kwa njia ya halali ya kuleta mageuzi kwa kuzingatia utaratibu wa sheria uliowekwa.

Amewataka makamanda wa polisi wa mikoa yote kuhakikisha wanafuatilia mikutano hiyo na kuwachukulia hatua watakaobainika kutaka kuvunja amani.

"Tumesikia baadhi ya viongozi wa vyama wakishabikia vitendo vya uvunjifu wa amani kwa kuhamasisha wafuasi wao kuchukua sheria mikononi mwao kama njia ya kujibu maneno ya uchochezi na kuingilia faragha za viongozi wao ila vitendo hivyo siyo tu kinyume cha sheria, badala yake vinadhoofisha mshikamano wa wa jamii," amesema Kamishna Hamad


Majibu ya ACT-Wazalendo

Othman amesema yapo matukio mengi yametokea lakini polisi haikuwahi kutok­­a hadharani au kuchukua hatua.

Amesema matukio ni mengi siyo tu kwa maneno lakini pia kwa uhalifu lakini hakuna aliyetoka kutoa tamko.

Amedai miongoni mwa matukio hayo ni kuuawa kikatili watu 21 wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, watu 18 walipigwa na kujeruhiwa wakiwemo viongozi wa chama hicho waandamizi ambao wengine wameachwa na ulemavu wa kudumu.

“Katika matukio haya yote hatukuwahi kuona kamishna anatoka hadharani kukemea au polisi kuchukua hatua dhidi ya watu waliofanya haya na ni mambo yapo wazi,” amedai Othman.

Amezungumzia matukio mengine aliyosema ni ya kuvunja amani akieleza yalitokea katika uchaguzi mdogo ulliofanyika Konde mwaka 2021 ambao ulifutwa.

Pia, amezungumzia baadhi ya wananchi kunyimwa vitambulisho vya Mzanzibari (Zan ID) akidai yote yanakaliwa kimyaa.

Kutokana na hayo, Othman ametahadharisha kwamba amani na utulivu ni dhamana ya watu wote, hivyo kila mtu akitimiza wajibu wake na kuwapo dhamira ya kweli itapatikana bila vitisho.

“Amani haiwezi kujengwa kwa maagizo, matumizi ya nguvu duniani hayajawahi kuleta amani,” amesema.

Othman amesema licha ya mambo yote hayo kufanyika, hakuna kilichobadilishwa katika sheria.

Hata hivyo, akizungumzia madai hayo, Kamishna Hamad amesema polisi wanatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria bila kupokea maagizo yoyote maana wao wana weledi wa kutambua viashiria vya uhalifu.


Kuhusu wakuu wa mikoa

Othman amesema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar wakuu wa mikoa siyo wanasiasa bali ni watendaji wakuu katika mikoa yao lakini wamekuwa wakitoa amri kwa polisi watekeleze wanachotaka wao.

“Polisi wanayo fursa ya kufanya kazi kwa weledi na maadili bila kuegemea upande wowote au kupewa maagizo kutoka kwa wanasiasa,” amesema. 

Kwa mujibu wa Othman jinai haina ukomo kwa hiyo kama kweli wanataka kutenda haki wachukue hatua za kushtaki waliotenda makosa hayo.

“Njia pekee ya kunisuru Zanzibar ni mambo kuendeshwa kwa haki bila kupedelea ukiwemo kuangalia mwenendo mzima wa mchakato wa uchaguzi,” amesema.

Hata hivyo, amesema chama hicho kitaendelea kuhubiri haki, amani na mustakabali wa Zanzibar, huku wakiwahimiza wananchi watambue haki zao pale zinapokiukwa.