Hemed awahimiza vijana Zanzibar kugeukia kilimo
Mkulima wa mbogamboga Rashid Khamis akiomuonesha Makamu wa Pili shamba lake la pilipili hoho Kitule Paje Mkoa wa Kusini Unguja. Picha na Jesse Mikofu
Muktasari:
- Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla amesema hakuna sababu ya vijana kulia ajira badala yake ni kubadili mitazamo na kujikita kwenye kilimo
Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema wakati Wazanzibar wakilalamika kwamba vijana hawana ajira, kuna fursa kubwa katika sekta ya kilimo ambayo haijatumika ipasavyo.
Hivyo, ameitaka Wizara ya Kilimo, Umwagilia, Maliasili na Mifugo na watendaji wengine kutoa elimu na kufanya kazi ya kubadilisha mitazamo ya vijana na wananchi ili wajikite kwenye kilimo.
Hemed ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Julai 6, 2027 katika shamba la kilimo Mtule Paje, Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea mashamba ya mpunga, kilimo cha mbogamboga na ufugaji.
"Tunalalamika vijana hawana ajira lakini kuna fursa kubwa sana kwenye kilimo, tunapaswa kutoa elimu na kubadilisha mtazamo kwamba wanaokwenda kwenye kilimo ni watu wa chini," amesema.
Amesema kwa sasa kuna hoteli nyingi ambazo zinahitaji mbogamboga lakini bado kinachopatikana hakijatosheleza kutokana na uzalishaji kuwa mdogo.
"Kuna fursa nyingi kwenye sekta ya kilimo, leo hapa tunaambiwa kuna oda nyingi za bidhaa hizi lakini hazipatikani," amesema,
Ameitaka wizara husika kujikita kutoa elimu kwa wananchi wabadilishe mitazamo hasi kuhusu kilimo wajikite huko badala ya kutegemea ajira serikalini kwani Serikali haiwezi kuajiri watu wote.
Amesema: "hata zile ajira 300,000 ziliozoahidiwa kwenye ilani, hatuwezi kuzipata zote serikalini lakini ni kupitia sekta hizi, kwa hiyo ni wajibu sasa kuweka mazingira, kuwapa utaalamu na kuwawezesha wakulima."
Hivi karibuni, iliibuka hoja kuhusu ajira za vijana wa Zanzibar kuchukuliwa na wageni, jambo lililoibua mjadala ndani na nje ya Baraza la Wawakilishi.
Mjadala huo uliibuka baada ya Naibu Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Hafidh Hassan Khamis kueleza ndani ya Baraza kwamba ajira nyingi katika sekta ya hoteli, Wazanzibari ni wachache ikilinganishwa na wageni, hivyo akasema wanakwenda kufanya mapinduzi.
Hoja hiyo ilichukuliwa kwa mitazamo tofauti na kuibua mijadala ya ubaguzi ndani ya baraza na na kwenye mitandao ya kijamii
Akiwa katika mashamba ya mapunga Cheju, Hemed amesema Zanzibar kuna eneo kubwa ambalo bado halijafanyiwa kazi ipasavyo katika kilimo, jambo ambalo linasababisha iendelee kuagiza mchele kutoka nje ya nchi.
"Sisi bado tunalima kizamani, na tunalima mara moja kwa mwaka, wakati wenzetu Tanzania Bara wanalima mara tatu kwa mwaka, lazime tubadilike katika kilimo cha namna hiyo," amesema.
Ameiagiza wizara hiyo kuhakikisha maeneo yote yanayofaa kulimwa yatengenezewe mifumo ya kisasa na umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji na kujiepusha na kuagiza mchele na bidhaa zingine za kilimo nje ya nchi.
"Bado tunaagiza chakula kingi nje ya nchi, karibu asilimia 80 tunaagiza kutoka nje ya nchi, sasa tunapaswa kutoka huko na tunaweza tukifanya vizuri kwenye kilimo itatupa mwanga mzuri," amesema.
Amesema ipo haja kutoka kwenye kilimo cha mazoea na kufanya kilimo cha biashara.
Naye, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Suleiman Masoud Makame amesema eneo la Cheju limeanza kubadilika baada ya kuweka miundombinu ya umwagiliji na kulima kisasa.
Amesema awali wakulima walikuwa wakilima robo ekari wanapata magunia 10 ya mpunga lakini kwa sasa wanapata magunia 22 kwa robo ekari.
"Tumeanza kuona mabadiliko baada ya kuanza kilimo cha kisasa kwasasa hata mavuno yanaongezeka," amesema waziri huyo.
Naye, mkulima wa mbogamboga Kitule, Rashid Khamis amesema kuna soko kubwa la mbogamboga Zanzibar kwani hoteli nyingi zinahitaji na hawajaweza kukidhi mahitaji.