Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hati ya mashtaka 'dhidi ya Muungano’ ilivyomng’oa Rais Jumbe

Jana katika makala kuhusu Rais wa Awamu ya Pili wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Aboud Jumbe Mwinyi, tuliishia kwenye jitihada zake za kuimarisha Muungano kwa kuunganisha vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP) na kuzaliwa CCM.

Pia, tulieleza namna alivyofanikisha CCM izaliwe tarehe na mwezi sawa ilipoanzishwa ASP Februari 5, 1957 na alifanikisha kubakiza neno ‘Mapinduzi’ yaliyoleta uhuru wao Januari 12, 1964, liwe sehemu ya jina la chama kipya. Kwa maana ya Chama cha Mapinduzi bila kuwa na tafsiri yake kwa lugha ya Kiingereza.

Leo tunaendelea na maelezo ya namna Jumbe na watendaji wake ndani ya SMZ walivyopendekeza muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu kwa mambo 11 tu yaliyoainishwa katika Mkataba wa awali wa Muungano.

Mtazamo huo ndio aliouweka wazi Jumbe baadaye katika kitabu chake kiitwacho; The Partnership, yaani (Ubia kati ya Tanganyika na Zanzibar) kilichosambazwa mwaka 1984.

Kuthibitisha hilo, ananukuu ibara ya tano ya Mkataba wa Muungano inayosema kwamba kufuatia kuundwa kwa Serikali ya Muungano, "Sheria za Tanganyika zilizopo na zile za Zanzibar, zitaendelea kuwa na nguvu katika nchi hizo." (The Partnership, uk. 22).

Jumbe alielezwa hoja zake za kudai Serikali tatu kwa maelezo Zanzibar imemezwa na Bara hayakuhusisha Wazanzibari, bali yalikuwa ni maoni yake na alimtumia Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kuandaa madai yake.

Pia, Jumbe alifanya maandalizi yake kimyakimya tu, kwa kumtumia Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati huo, kuandaa rasimu ya mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kwa madhumuni hayo.

Maandalizi hayo ya siri yalipojulikana na ushahidi wa rasimu ya mabadiliko hayo ya Katiba kutolewa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM cha Februari, 1984, kiongozi huyo alilazimika kujiuzulu nyadhifa zake zote.

Ilielezwa katika kutimiza azma yake, Jumbe alilazimika kumwachisha kazi Mwanasheria Mkuu wake aliyepewa na Mwalimu Nyerere, Damian Lubuva na kumwajiri Bashir Ebassuah Kwaw Swanzy, raia wa Ghana, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na alimpa uraia wa kujiandikisha.

Kwaw Swanzy ndiye aliyeandaa 'hati ya mashtaka' dhidi ya Muungano iliyokamatwa na ndiyo iliyotumika kumsulubu kwenye kikao cha NEC ya CCM Dodoma, Januari 1984.

Jumbe aliandaa ‘hati ya mashtaka’ ya kuhoji muundo na uhalali wa Muungano kwenye Mahakama Maalumu ya Kikatiba ya Jamhuri ya Muungano, ambayo kwa mujibu wa Ibara ya 125 na 126 ya Katiba ya Muungano ya mwaka 1977, kazi yake pekee “ni kusikiliza shauri lililoletwa mbele yake na kutoa usuluhishi juu ya suala lolote linalohusika na tafsiri ya Katiba; iwapo tafsiri hiyo au utekelezaji wake unabishaniwa kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.”

Kabla ya hapo, akihutubia kwenye kilele cha Sherehe za Mapinduzi Zanzibar, Januari 12, 1984, Jumbe alionyesha kukerwa na jinsi Muungano ulivyokuwa ukiendeshwa na kuwataka Wazanzibari wavute subira wakati tatizo hilo likishughulikiwa, na kwamba bila ya mwafaka na maridhiano kati ya Zanzibar na Serikali ya Muungano juu ya muundo sahihi wa Muungano, Zanzibar ingekwenda mahakamani.

Kwa sababu ya upinzani huo, Jumbe aling'olewa madarakani pamoja na Waziri Kiongozi wake Ramadhani Haji Faki na Mwanasheria Mkuu Kwaw Swanzy alitangazwa ‘persona non grata’ na kufukuzwa nchini.


Katiba mpya ya Zanzibar

Jumbe ndiye aliyesaini Katiba mpya ya Zanzibar iliyoanzisha Baraza la Wawakilishi ambalo ni Bunge la Zanzibar na kuwapo Baraza la Mapinduzi na Baraza la Wawakilishi. Ndio maana Rais wa Zanzibar anaitwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Baraza la Mapinduzi pamoja na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar huunda Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Jukumu kuu la Baraza la Mapinduzi ni kumshauri Rais wa Zanzibar, ambaye ni mkuu wa Serikali.

Katiba hiyo mpya ndiyo iligawanya madaraka ya Baraza la Mapinduzi na yale ya Baraza la Wawakilishi, pia ndiyo ilianzisha mfumo wa uchaguzi unaowataka raia kupiga kura badala ya kazi hiyo kufanywa na Baraza la Mapinduzi.

kutoka Tanzania visiwani, ndio waliosimama mmoja baada ya mmoja kulalamika na kushambulia kule walikokuita 'kupenda kwangu na kunyima madaraka, kutosikiliza shauri wala maoni, kujifanyia nitakavyo, kutoipenda CCM na Azimio la Arusha na madai mengine kama hayo'…" ( uk 15)


KUJIUZULU

"….Siku ya Jumamosi, baada ya kumuachia Ramadhani Haji (aliyekuwa Waziri Kiongozi) kutoa maelezo yake, ndipo mimi nilipochambua tuhuma zilizotolewa. Nilipomaliza nikashauri niruhusiwe kuacha shughuli zote za chama na Serikali"


BAADA YA KIKAO

"….Nilipowasili nilikofikia, si muda walifika mabwana Kawawa (Rashid) na Sokoine (Edward) wakifuatiwa muda mfupi na Mwalimu Nyerere. Niliambiwa kwa vile niliacha madaraka kwa mdomo hakuna ushahidi, bora kufanya uthibitisho kwa maandishi.”

“Kwa kutotaka 'kuchafua hali ya hewa' niliandika kuacha madaraka ya Makamu Mwenyekiti wa chama na Makamu wa wa Rais wa Muungano, nikampa aliyekuwa mpiga taipu wangu achape. Mwalimu aliponiuliza kuhusu Zanzibar nilimwahidi kufanya hivyo nikifika Zanzibar"


HAIFAI KWENDA ZANZIBAR!

"...Hapo ndipo aliponiambia ingekuwa bora kwa 'sasa' kutokwenda Pemba (Nilikotaka kumpeleka kwao mke wangu niliyekuwa nimefuatana naye ) wala kwenda Unguja na kwa hiyo niandike na kuacha kwangu shughuli za Zanzibar. Kwa kuona wazi wasiwasi uliojidhihirisha, nilikubali yote."




ULINZI MKALI

"...Tulipofika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na kukuta ulinzi mkali wa Jeshi na Polisi, wakiwepo mkuu wa jeshi na mkuu wa jeshi la polisi, nilishindwa kabisa kuelewa sababu na maana ya yote hayo yalikuwa ni ya nini au kwa nini? Mpaka leo hakuna aliyenielimisha na bado niko ujingani" (uk 17)


SIMU IMEKATWA!

"....Nilipwerewa nilipofika nyumbani Mjimwema na kutaka kupiga simu Unguja. Niliona, kabla ya kutangazwa yaliyotokea, niwatulize wake zangu na wanangu Unguja angalau wajue tu nilikuwa salama Mjimwema. Niligundua simu hazifanyi kazi! Hapo nilimshukuru Mwenyezi Mungu nikamwachia yeye na kukaa kusubiri maajabu mengine huku nikiwaza 'Tunakwenda wapi'?"


SERIKALI TATU

"....Mfumo wa serikali tatu ndio umekuwa msimamo wangu na ndio mtizamo wangu uliopingwa vikali na chama..."


MAHUBIRI YA KUUVUNJA MUUNGANO!

"....Wenye kuhubiri kuuvunja muungano, watambue kuwa hawawezi kufanya hivyo kienyeji… Huu ni muungano wa Watanzania, si wa chama hiki au kile. Wote wenye umri wa miaka ishirini na tisa na chini ya hapo ambao naamini ndio wengi, hawajawahi kuwa chochote isipokuwa Watanzania.

Kabla ya kuwanyang’anya au kuwafutia Utanzania wao, wana haki ya kushirikishwa kuamua nasaba yao. Hii inamaana itapaswa kufanyika kura ya maoni ili Watanzania wenyewe ndio waamue kuvunja au kubadili mfumo wa Muungano.

Kisheria na kwa mujibu wa katiba, si jambo dogo au jepesi kuvunja Muungano, kama inavyoonekana baadhi ya viongozi kudhani. Lazima Watanzania kuangalia, kutafakari kwa makini na kujuana kwa yakini tunatoka wapi, kwa nini tuliungana, tumefika wapi na sasa tunataka au hatutaki nini, au tunataka kwenda wapi."


RAI YAKE

"....Katika zoezi hili (kuhusu Muungano), wanasiasa na Watanzania kwa ujumla wanapaswa wawe wakweli, wenye busara na zaidi kuliko yote ni uaminifu. Miaka 100 ijayo hapatakuwa, sio tu katika hili bali kote duniani, hata mmoja miongoni mwa walio duniani leo na hata akiwepo hatakuwa na lake. Bali, vizazi vyetu vitakuwepo. Mazao ya mbegu tunazoatika au kupanda leo itabidi kuvunwa na vizazi vyetu kesho"

Itaendelea kesho