Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Doria, uhifadhi wa bahari vyachochea uzalishaji wa samaki kuongezeka

Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu, Hamad Bakar Hamad akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari katika ofisi za Idara ya Habari Maelezo Zanzibar

Muktasari:

  • Uzalishaji wa samaki umeongezeka kutoka tani 38,000 hadi 88,000 kutoka mwaka 2020 hadi mwaka 2024.

Unguja. Mpango wa kuhifadhi bahari na kufanya doria za mara kwa mara umetajwa kupunguza uvuvi haramu na kuongeza uzalishaji wa samaki kisiwani Zanzibar kwa kipindi cha miaka minne.

Pia, uhifadhi huo unatajwa kuchochea sekta ya utalii na kuendelea kuvutia watalii wengi kutembelea kisiwa hicho kutokana na fukwe zake kuwa safi, ambazo ni moja ya vivutio vikubwa vya utalii.

Kwa mujibu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu, uzalishaji wa samaki umeongezeka kwa asilimia 107 kutoka tani 38,108 hadi tani 88,000 mwaka 2020/24, ambapo zimefanyika zaidi ya doria 1,500.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Idara ya Habari (Maelezo), Mkurugenzi wa Idara ya Uhifadhi wa Bahari katika Wizara ya Uchumi wa Buluu, Dk Makame Omar Makame, amesema kuwa doria zinazofanywa na wizara hiyo zimeanza kuzaa matunda kwa kuleta matokeo chanya katika jitihada za uhifadhi wa mazingira ya baharini.

“Tija inaonekana, kwa sasa kuna watalii wanafurahia kutembelea maeneo yetu ya fukwe, na tunapoona kuna ongezeko kubwa la uzalishaji wa samaki, jua inachangiwa na uhifadhi. Uvuvi haramu unaharibu mazalia, unaua samaki wachanga,” amesema na kuongeza:

“Mvuvi mmoja katika uvuvi haramu anaua samaki wengi akivua samaki wanaojaza janvi moja, samaki hao hao wanaweza kujaza carry mbili (gari ya tani moja) wakiwa wakubwa. Sasa utaona kiasi gani wanavyoharibu samaki,” amesema.

“Huu ni matokeo ya kushindwa kufanyia kazi taka za manispaa, hazihifadhiwi vizuri, kwa hiyo zinakwenda baharini. Hii ni jambo kubwa, lakini linahitaji wadau wengi wakiwemo manispaa,” amesema.

Amesema plastiki zikibaki baharini kwa muda mrefu, samaki wakizila taka hizo, zinahatarisha afya ya binadamu.

Hata hivyo, amesema kuna jitihada mbalimbali za kutekeleza mradi kupitia Jumuiya ya Ulaya (EU) kuona namna ya kutatua changamoto ya plastiki baharini.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo na Uratibu wa Uchumi wa Buluu, Mondy Muhando, amesema kuna mpango wa matumizi ya bahari (Marine Spatial Planning), ambao katika sampuli ya awali umeonyesha mafanikio makubwa.

Kupitia mpango huo wamepanga matumizi ya bahari, hususan katika maeneo yenye migogoro zaidi.

“Utekelezaji wake unalenga zaidi maeneo maalumu kulingana na changamoto zilizopo za migogoro kwa kushirikiana na taasisi ambazo zipo katika sekta hizo,” amesema.

Akifafanua kuhusu kuongezeka kwa bei ya samaki licha ya kwamba uzalishaji wake umeongezeka, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Hamad Bakar Hamad, amesema bei inaongezeka kulingana na mahitaji kwani bidhaa hiyo imekuwa ikiongezeka mahitaji yake.

“Bidhaa ikiwa inahitajika kwa kiasi kikubwa, hata bei yake lazima iwe juu. Kwa hiyo, mahitaji na upatikanaji wa samaki vina mahitaji mengi. Hakitoshi, halafu uzingatie nchi ambayo ni kitovu cha utalii kama Zanzibar, hilo litakuwa linaendelea.”

Amesema bei ya samaki mwaka 2000 hadi kufikia mwaka 2024 imeongezeka kwa asilimia 201. Hii fedha inaenda kwenye mfuko wa wavuvi na mnyororo wao unaongezeka. Mlaji ni hasara, lakini kwa mvuvi ni faida.

Muhando amesema kinachotakiwa ni angalau kufanya uwiano kwa sababu ukilazimisha samaki wavuliwe mpaka bei ishuke, maana yake kuna kitu kinaitwa sustainability kitakuwa hakipo.

Amesema kwa sasa mwelekeo wa Serikali ni kuwa na ufugaji wa samaki wa kibiashara, ambao walijaribu mwaka 2020 lakini haukufanikiwa kwa sababu hawakuwa na vifaranga, walikosa wataalamu na uelewa mdogo wa watu kuhusu ufugaji wa samaki.

“Katika hili lazima tuwe wakweli, hatukufanikiwa, lakini kwa sasa tumeshajipanga kuhakikisha tunakwenda kufuga kibiashara,” amesema.

Amesema kwa sasa Serikali imeshaelekeza fedha za kujenga bandari mbili kuu za uvuvi wa bahari kuu.