Tabora yapanda miti 570,000 kuelekea Siku ya Misitu Duniani
Baadhi ya maofisa wa uhifadhi kutoka wakala wa huduma za misitu nchini kanda ya Tabora wakiwa na wanafunzi wa shule ya Sekondari Fundikira katika zoezi la upandaji wa miti kuelekea Siku ya Misitu Duniani Machi 21.
Muktasari:
- Mkoa wa Tabora umepanda miti 570,000 katika msimu wa mvua 2025/2026, ikiwa ni jitihada za kuhifadhi mazingira kuelekea maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani, Machi 21.
Tabora. Mkoa wa Tabora umepanda miti 570,000 katika taasisi za serikali, binafsi na makazi ya wananchi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhifadhi misitu na kurejesha uoto wa asili kuelekea Siku ya Misitu Duniani huadhimishwa kila mwaka Machi 21.
Upandaji huo umefanyika katika msimu wa mvua wa mwaka 2025/2026, huku shughuli zikiendelea leo Machi 20, 2026 katika shule mbalimbali wilayani Tabora, kuelekea maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani yatakayofanyika kitaifa mkoani Lindi.
Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Ofisa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Aloyce Kilemwa, amesema miti hiyo inalenga kuongeza uoto wa asili na kurejesha maeneo yaliyoharibiwa.
Amesema miti iliyopandwa ni ya matunda, kivuli, mapambo na ile ya mbao, ambayo inaweza kupandwa mashambani na katika mipaka ya maeneo.
Hata hivyo, Kilemwa amesema changamoto kubwa iliyopo si upandaji wa miti bali ni utunzaji wake, akieleza kuwa baadhi hukanyagwa na mifugo au kukosa maji wakati wa ukame, hali inayosababisha kufa.
“Miti mingi inashindwa kukua kutokana na changamoto za kimazingira, ikiwemo kukanyagwa na mifugo au kukosa kumwagiliwa maji wakati wa ukame,” amesema.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, amesema hatua zimechukuliwa ikiwemo kuwagawia wanafunzi miti ili kila mmoja awe na jukumu la kuitunza hadi ikue.
Aidha, viongozi wa kisiasa, dini na mamlaka mbalimbali wamehusishwa kusimamia zoezi hilo ili kuhakikisha miti inapandwa na kukua kwa mafanikio.
“Tunashirikisha makundi mbalimbali kuhakikisha Tabora inakuwa ya kijani,” ameongeza.
Baadhi ya wakazi wa Tabora wameunga mkono juhudi hizo, wakisisitiza umuhimu wa kutunza miti ili kurejesha mazingira yaliyoharibika kutokana na ukataji holela.
Mkazi wa Tabora, Sauda Swaleh, amesema jamii ina wajibu wa kuhakikisha miti inatunzwa, akitoa mfano wa madhara yaliyotokea baada ya ukataji miti ovyo.
Amesema katika Shule ya Sekondari Fundikira, jengo moja liliezuliwa na upepo mkali kufuatia kukatwa kwa miti iliyokuwa ikizingira eneo hilo.
Kwa upande wake, Juma Mkanilo amesema matumaini ya uhifadhi yameongezeka baada ya wakulima wa tumbaku kuanza kutumia nishati mbadala katika ukaushaji, badala ya kuni.
Mkoa wa Tabora, ambao ni miongoni mwa mikoa mikubwa nchini yenye maeneo ya hifadhi, umekuwa ukikumbwa na changamoto ya ukataji miti kwa ajili ya mkaa, kuni na ukaushaji wa tumbaku.
Katika kudhibiti hali hiyo, Mkuu wa Mkoa, Paul Chacha, hivi karibuni alitangaza kufungia utoaji wa vibali vya uchomaji mkaa, hatua inayolenga kupunguza ukataji wa miti na kulinda mazingira.