Samia: Tanga kaeni mkao wa kula
Muktasari:
- Aeleza mkakati wa kuiunganisha bandari ya Tanga na reli kutoka Tanga hadi Musoma yenye urefu wa kilomita 1,108.
Tanga. Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema endapo atapewa ridhaa ya kuongoza nchi kwa kipindi kingine cha miaka mitano, Mkoa wa Tanga utanufaika na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo itakayoufungua kiuchumi na kuongeza ajira.
Akizungumza leo Jumatatu, Septemba 29, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Usagara, Tanga Mjini, Samia alieleza mikakati ya kimkakati inayolenga kuinua uchumi wa mkoa huo, ikiwemo uendelezaji wa bandari ya Tanga.
Amesema bandari hiyo, ambayo imepangwa kuwa bohari ya mafuta na gesi, itazalisha ajira mpya 2,100.
Aidha, ametaja mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga ambao umekamilika kwa asilimia 84, ukielezwa tayari kunufaisha wananchi wengi.
“Kwa mfano, eneo la Chokeleani pekee limeajiri watu 1,300, huku wilayani Tanga watu 2,000 wakiwa tayari wamepata ajira kupitia mradi huo,” amesema Samia.
Ameongeza kuwa Serikali yake ikipata ridhaa, itatekeleza mradi wa reli ya kilomita 1,108 kutoka bandari ya Tanga kuelekea Arusha hadi Musoma, hatua itakayochochea shughuli za viwanda na madini.
Reli hiyo imepangwa kuunganishwa na barabara ya Handeni–Singida kwa ushirikiano kati ya Mamlaka ya Bandari (TPA) na Tanroads (Wakala wa Taifa wa Barabara Tanzania).
Kadhalika, ameahidi upanuzi na ukarabati wa barabara ya Dar es Salaam–Chalinze–Segera hadi Arusha, yenye urefu wa kilomita 646 ili kupunguza msongamano wa magari.
“Mwelekeo wetu ni kuirudisha Tanga ya viwanda, sambamba na kuanzisha na kuendeleza kongani za viwanda katika kila wilaya. Tutaendelea pia kufufua viwanda vilivyobinafsishwa lakini havijaendelezwa, ikiwemo kiwanda cha chai Korogwe,” amesema.
Samia ametaja pia maendeleo mengine yaliyopangwa kwa Tanga kuwa ni kuanzishwa kwa kiwanda kipya cha kuunganisha magari ya wagonjwa na kuvutia wawekezaji wapya, sambamba na kuweka maeneo wazi kwa ajili ya uwekezaji.
Katika sekta ya madini, amesema Serikali itabaini maeneo mapya yenye rasilimali hizo ili vijana wapate fursa za ajira na kujiajiri. Upande wa kilimo, ameeleza kuwa maeneo maalum yametengwa nchini, yakiwemo Tanga, kwa ajili ya mashamba ya vijana.
Pia ameahidi kukamilisha ujenzi wa soko la kisasa la wamachinga lenye uwezo wa kuhifadhi wafanyabiashara 1,400 na kujenga soko la samaki la kimataifa wilayani Pangani, huku wavuvi wakiboreshewa nyenzo na miundombinu ya kisasa.
Akizungumzia sekta ya afya, Samia ameahidi kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda vya dawa na vifaa tiba ili kupunguza gharama za matibabu.
Aidha, amesema atatekeleza mpango wa bima ya afya kwa wote ndani ya siku 100 za kwanza za utawala wake, hatua itakayokomesha changamoto za kushikiliwa kwa maiti hospitalini kutokana na kushindwa kulipia gharama za matibabu.
“Mambo ya kuzuia maiti kwa sababu haijalipiwa gharama za matibabu hayatatokea tena. Kila Mtanzania akiwa na bima ya afya, gharama zitalipwa iwe amepona au amefariki,” amesema mgombea urais huyo.
CCM Tanga yamuahidi
kura za kishindo
Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdulrahman amesema mkoa huo umejipanga kumpa Samia ushindi mkubwa wa kura pamoja na wagombea wa ubunge na udiwani kupitia chama hicho.
“Tuna kila sababu ya kukupa kura nyingi sana. Tunashukuru hali ya amani na utulivu uliodumu nchini na hapa Tanga chini ya uongozi wako. Tumeendelea kuwa wamoja na wenye mshikamano,” amesema Abdulrahman.
Ujumbe wa Kihongosi kwa vijana
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenan Kihongosi amewataka vijana nchini kutokubali kurubuniwa na watu wasiolitakia mema Taifa, akisema wapo wanaochochea vurugu kwa manufaa yao binafsi huku familia zao zikiwa nje ya nchi.
“Tuna wajibu wa kulinda amani na utulivu wa Taifa letu, tusishawishike kushiriki vurugu yoyote. Wanaotaka kututumia kama daraja tuwakatae kwa sababu familia zao haziko nchini, wao wakileta machafuko wana sehemu za kwenda, sisi hatuna. Kwa hiyo tuwakatae na kuwaambia wazi amani kwanza,” amesema Kihongosi.
Kwa upande wake, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kupiga kura na kutokubali kupotoshwa na maneno ya watu kupitia mitandao ya kijamii.
“Wakati tunapitisha jina la mgombea wetu tulijiridhisha kwamba ni mtu sahihi. Niwaambie Watanzania, huyu mama ni mashine kweli kweli, ana utu na uzalendo wa hali ya juu. Wanaopiga kelele mitandaoni siyo wajumbe wa vikao, hawa hapa ndiyo wapiga kura. Mama wanaokupenda ni wengi kuliko wanaokuchukia, hivyo kaza buti twende mbele,” amesema Nape.
Wabunge waomba kura
Mgombea ubunge wa viti maalumu kupitia kundi la wafanyakazi, Mariam Mungula amesema katika kipindi cha miaka minne, Serikali imelipa malimbikizo ya mishahara ya Sh226 milioni kwa wafanyakazi na kuwapandisha madaraja, hatua iliyosaidia kuongeza ari ya utumishi.
Amesema mbali na hatua hiyo, Serikali imeboresha maslahi ya wafanyakazi na kufungua ajira mpya, ambapo zaidi ya watu 150,000 wameajiriwa.
“Niwaambie wafanyakazi tushukuru kwa hili, hivyo ifikapo Oktoba 29, 2025 tujitokeze kuwachagua viongozi wa CCM ili waendelee kutuletea maendeleo,” amesema Mariam.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Tanga, Kassim Mbaraka amesema uwekezaji uliofanyika katika bandari ya Tanga ndani ya miaka minne umekuwa na mchango mkubwa katika kubadilisha uchumi wa mkoa huo.
“Mama kuna mambo umeyafanya Tanga ambayo hayakuwahi kufanyika tangu uhuru. Uwekezaji uliofanyika bandari ya Tanga umewezesha idadi ya meli kuongezeka kutoka 118 mwaka 2020 hadi zaidi ya meli 400 kwa sasa. Bandari hii sasa inashusha tani 1.3 milioni za mizigo, ajira rasmi zilizozalishwa ni 457 na vibarua 17,871,” amesema.
Kutokana na ongezeko hilo la shughuli za bandari, Mbaraka aliomba Serikali kuipanua barabara ya Muheza–Tanga kutokana na msongamano mkubwa wa magari.
Naye mgombea ubunge wa Jimbo la Handeni, Charles Sungura alitumia mkutano huo kuwaomba wananchi wa jimbo hilo kuipigia kura CCM, huku akiahidi kusimamia upatikanaji wa zahanati katika vijiji 26 ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.