Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mgombea urais Makini aahidi soko, viwanda vya mazao Rungwe

Mgombea Urais wa chama Makini, Coaster Kibonde akimnadi mgombea ubunge wa Rungwe kupitia chama hicho, Gabriel Kibonde (kulia) wakati wa mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika eneo la KK wilayani humo mkoani Mbeya.

Muktasari:

  • Amesema iwapo atapewa ridhaa ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atajenga viwanda vitakavyokuwa mwarobaini wa kuzalisha malighafi na kutafuta soko ndani na nje ya nchi.

Mbeya. Mgombea urais wa chama cha Demokrasia Makini (Makini), Coaster Kibonde ameahidi kuwajengea viwanda maalumu wakulima wa mazao ya kahawa, parachichi na chai katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya ili wanufaike na kilimo wanachokifanya.

Akizungumza leo Septemba 29, 2025 Mtaa wa K-K katika mwendelezo wa kampeni zake mkoani Mbeya, Kibonde amesema anashangazwa kuona mazao ya chai, parachichi na kahawa zikikosa soko na kufanya wakulima kutonufaika na kilimo chao.

Amesema iwapo atapewa ridhaa ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atajenga viwanda ambavyo vitakuwa mwarobaini wa kuzalisha malighafi na kutafuta soko ndani na nje ya nchi.

"Nitafufua kiwanda cha chai, lakini kutakuwa na viwanda vya mazao ya parachichi na kahawa ambapo serikali yangu itatafuta soko la ndani na nje," amesema Kibonde.

Amesema suala la katiba litafanyiwa pia kazi ambapo atateua baraza la mawaziri akiwapa nafasi viongozi wote wa vyama katika nafasi mbalimbali akiwaomba wananchi kudumisha amani na utulivu wa nchi.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa chama hicho, Jimbo la Rungwe, Gabriel Kibonde amesema akipata ridhaa ataanza na miundombinu ya barabara, daraja na kujenga machinjio ya kisasa.

"Nitapita nyumba kwa nyumba, Kata na Kijiji kuhakikisha kila mmoja anafanya shughuli zake kwa ufanisi, lile daraja katika machinjio yetu naenda kuijenga kisasa, barabara zote zitapitika," amesema Kibonde.

Awali, katibu wa chama hicho Mkoa wa Mbeya, Leonard Mwaikambo amesema siasa siyo chuki wala uhasama kwani nia ya kila mmoja ni kuliongoza Taifa.

"Leo ni mkutano wa tatu mkoani hapa, nimpongeze na kumshukuru mwenyekiti wa Mtaa huu kuhudhuria kampeni yetu, hii inaonesha umoja wetu kama Watanzania," amesema Mwaikambo.

Naye Naibu Katibu Mwenezi wa chama hicho, Ramadan Mbombo amesema siasa ni uti wa mgongo akieleza kuwa yeyote anayepatikana katika nafasi ni kupitia siasa.

"Kuanzia ngazi ya mtaa hadi Taifa wote tunawachagua sisi kupitia siasa, tumekuja wana Rungwe kuwaomba mtupe kura ili Makini tuliongoze Taifa.

"Vyama vyote vinayo haki ya kuiongoza nchi ikiwamo Makini, tunazo sera zinazogusa maisha ya wananchi na matarajio yetu ni kuona Rungwe inampa kura mgombea wetu wa urais, Kibonde," amesema Mbombo.

Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Grace Ngonyani amewaomba wanawake na vijana kuwa msitari wa mbele kufanya maamuzi sahihi kukichagua Chama Makini kutokana na kuguswa zaidi katika sera.

Amesema wananchi wasikate tamaa katika kupiga kura kwani kufanya hivyo ni kuwapa nafasi wengine kuchagua wanaowapenda kwa masilahi yao binafsi.