Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lindi wazindua mkakati kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula

Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na Uzalishaji), Mwinjuma Mkungu akizungumza leo Ijumaa, Desemba 12, 2025 katika kongamano la wataalamu wa kilimo na ushirika mkoani Lindi.

Lindi. Wakati mkoa wa Lindi ukifanya vizuri kwenye uzalishaji wa mazao ya biashara, bado unakabiliwa na uhaba wa chakula kutokana na wakulima wengi kujikita zaidi kwenye korosho na ufuta, hali inayosababisha uzalishaji mdogo wa mazao ya chakula.

Hali hiyo imeilazimu Serikali ya Mkoa wa Lindi kuja na mkakati maalumu wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula, hususan mazao ya kati kama mihogo, viazi lishe, mtama, alizeti, mbogamboga na matunda.

Akizungumza leo Ijumaa, Desemba 12, 2025 katika kongamano la wataalamu wa kilimo na ushirika, Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na Uzalishaji), Mwinjuma Mkungu, amesema wakulima wamekuwa wakilima zaidi mazao ya biashara na kuacha mazao ya chakula, jambo lililochangia mkoa kukabiliwa na uhaba wa vyakula mbalimbali.

Mkungu amesema mkoa umejipanga kushirikiana na maofisa kilimo waliopo vijijini na kata ili kuongeza uzalishaji kupitia mashamba darasa.

"Malengo yetu ni kushirikiana na maofisa kilimo kuanzisha mashamba darasa yatakayowawezesha wakulima kujifunza mbinu bora za kilimo. Hii itasaidia kufikia uwezo wa kujitegemea kwa chakula na kuongeza uchumi wa mkoa," amesema.

Amesema upatikanaji wa mbegu bora ni changamoto kubwa kwa wakulima wa Lindi, jambo linalosababisha uzalishaji mdogo, hivyo mipango ya kuhakikisha mbegu bora zinawafikia wakulima inaendelea kuimarishwa.

"Wakulima wengi hawatumii mbegu bora wala mbolea. Hii inasababisha mavuno duni. Kupatikana kwa mbegu bora kutaleta mabadiliko makubwa," amesema.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Zuwena Omary, amewataka maofisa kilimo kila mmoja kuwa na angalau ekari sita za mashamba darasa, huku wakulima wakitakiwa kuwa na ekari tatu kwa ajili ya kujifunzia mbinu bora za kilimo na matumizi ya mbolea.

Omary amesema matumizi ya mbolea katika mkoa wa Lindi bado ni madogo, hali inayosababisha mazao kutostawi ipasavyo.

"Maofisa kilimo hakikisheni mashamba darasa yanaanzishwa na mkasisitize matumizi ya mbolea ili kuongeza uzalishaji," amesema.

Ameongeza kuwa shule za msingi na sekondari zinapaswa kuwa na mashamba ya kuzalisha mazao ya chakula kama mtama, mihogo, mboga mboga na matunda ili ziwe na uhakika wa chakula shuleni.

Ofisa Kilimo wa Kata ya Mnolela, Haji Hassan, amesema kongamano hilo limeibua njia za kutatua uhaba wa chakula endapo mikakati iliyowekwa itatekelezwa ipasavyo.

"Tukitekeleza mikakati hii, tunaweza kuondokana na changamoto ya chakula na kujitegemea katika miaka ijayo," amesema Hassan.