Dk Mwinyi: Hii ni historia, haijawahi kutokea
Muktasari:
- Watu hao wamefutarishwa katika Uwanja wa Amani Complex Mkoa wa Mjini Magharibi na kuwahusisha watu tofauti bila kujali itikadi zao
Unguja. Wakati Zanzibar ikifutarisha watu zaidi ya 25,000 kwa wakati mmoja, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amesema tukio hilo ni la kihistoria kwani halijawahi kutokea.
Watu hao wamefutarishwa Machi 7, 2026 katika Uwanja wa Amani Complex Unguja Zanzibar.
Akizungumza katika futari hiyo, Rais Mwinyi ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema amefurahishwa kuona jambo hilo linafanyika katika hali hiyo.
"Tumezoea kufutarisha kila mkoa kwa wakati wake, lakini nilipoletewa taarifa hii nilisema lifanyike ni jambo jema sana kwani halijawahikufanyika na hii ni historia," amesema Dk Mwinyi
Amesema utaratibu huo ni vyema ukaendelezwa kwani unaunganisha watu wengi kwa wakati mmoja.
Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Mahmaoud Mahmoud amesema kufutarisha pamoja kunaongeza upendo, kuondosha chuki na kuongeza mshikamano na huruma miongoni mwa wanajamii.
"Hata kwenye maandiko vitabu vitakatifu inaelezwa wazi kufutarisha ni jambo la hekima anayefutarisha na anayefunga wote wapo sawasawa," amesema
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Akif amesema tukio hili linaonesha dunia dhahiri kwamba Zanzibar kuna amani, upendo na utulivu katika kuwaunganisha watu wote pamoja.
Amesema kamisheni wamekuwa wakiandaa matukio mengi katika kutangaza utalii lakini walikuwa hawajafikia katika hatua hii.
"Inaonesha wazi namna ambavyo tunaweza kupiga hatua kubwa, zaidi ya miaka 30 tumeshiriki katika matukio makubwa duniani lakini hili tulikuwa hatujafikia," amesema
Awali Mkurugenzi Mkuu wa ZBC Ramadhan Bukini amesema wamefurarisha takribani watu 25,000 kutoka maeneo yote ya Zanzibar bila kujali itikadi na dini za watu
"Hapa wamekuja watu wote hata wakristu wapo, hili ni jambo la kusifia na kuonesha mshikamano wetu katika kuendeleza umoja wa Wazanzibar," amesema