Ahadi za Moza ndani ya siku 100 akiukwaa ubunge Kinondoni
Mgombea Ubunge wa Kinondoni kwa tiketi ya Chaumma, Moza Ally akinadi sera zake katika kampeni leo Septemba 29, 2025 eneo la Kigogo Mwisho, Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Mgombea ubunge wa Kinondoni kwa kupitia Chaumma, Moza Ally ameahidi ndani ya siku 100, atasimama mwenyewe kuhakikisha wanawake, wenye ulemavu na vijana wameunda vikundi kwa usawa bila upendeleo na wanapata mikopo kwa njia stahiki.
Dar es Salaam. Mgombea ubunge wa Kinondoni kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Moza Ally amesema iwapo atashinda nafasi hiyo, ndani ya siku 100 atahakikisha mikopo ya halmashauri inawafikia walengwa.
Kwa mujibu wa Moza, ndani ya siku hizo atasimama mwenyewe kuhakikisha wanawake, wenye ulemavu na vijana wameunda vikundi kwa usawa bila upendeleo na wanapata mikopo kwa njia stahiki.
Moza ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam leo, Jumatatu Septemba 29, 2025 alipozungumza katika mkutano wake wa kampeni, uliofanyika Uwanja Sumaye, Kata ya Kigogo wilayani Kinondoni.
Amesema kwa kuwa atakuwa mwakilishi wa wananchi wa Kinondoni, hataruhusu mikopo hiyo itolewe kwa upendeleo, huku akisisitiza vikundi vitakavyoundwa vitakuwa halisi na vya wazi.
“Tutapita nyumba kwa nyumba kuandika majina, mkituona msiogope, tunatafutiana mwanya wa kupata fedha ili wote tuwe na maisha mazuri,” amesema.
Ndani ya siku hizo, amesema katika ofisi yake atakuwepo mwanasheria ambaye jukumu lake ni kutoa usaidizi wa kisheria kwa vikundi vyote ili vikidhi uhalali wa kukopeshwa.
“Nitakuwa naleta mrejesho kila baada ya muda ili tukikutana kwenye mikutano kama hii, vikundi hivyo tuvione, watu waonekane ili tuseme kwa sasa tumefikia vikundi vimefikia kadhaa na unaona hali zao,” ameeleza.
Mgombea huyo, amesema wananchi hawatalazimika kuandaa fedha ili kuingia ofisini kwake na kumwona, bali watapata fursa hiyo kila pale watakapohitaji.
“Nitakuwa Mbunge wa watu, sitokuwa mbunge wa mfukoni. Nitahakikisha nawatumikia wananchi wa Jimbo la Kinondoni wakiwemo wa Kata ya Kigogo. Nipeni imani yenu,” amesema Moza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chaumma Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kileo amewataka wananchi wa Kinondoni kuhakikisha Oktoba 29, wanakwenda kupiga kura kwa wagombea wa chama hicho.
Amesema chama hicho kina dira inayolenga kutoa lishe bora kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili kuwajenga kiakili.
“Sisi tunataka watoto wetu wawe na afya bora kutokana na lishe bora. Ndiyo maana tumeweka sera ya kuhakikisha wanafunzi shule za msingi na sekondari wawe wanapata chakula shuleni,” amesema Kileo.