Mradi wa “Mlinde Mama” wachochea afya bora kwa wajawazito mkoani Geita

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dk Omari Sukari (aliyeshika kishikwambi) pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la PHIT na Kamati ya Afya ya Mkoa (RHMT) wakati wa upokeaji vishikwambi vilivyotolewa na mradi wa Mlinde Mama.
Prime Health Initiative Tanzania (PHIT) ni Shirika la Tanzania lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam lililoundwa ili kuchangia katika kuboresha afya nchini Tanzania.
PHIT inalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za afya ikijikita zaidi katika afua za afya ya uzazi, mtoto na vijana (RMNCAH), UKIMWI, maradhi yasiyo ya kuambukiza (NCDs), mabadiliko ya tabia katika jamii (SBC) na matumizi ya teknolojia kuboresha huduma za afya.
Mwaka 2022, PHIT ilipokea ufadhili kutoka mfuko wa Bill and Melinda Gates Foundation (BMGF) ili kutekeleza mradi wa “Mlinde Mama” mkoani Geita.
PHIT kwa kushirikiana na Wizara ya afya, Wizara ya Ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) walitekeleza mradi wa Mlinde Mama katika vituo sita vya kutolea huduma katika halmashauri za wilaya Chato na Geita na kufanikiwa kuleta mafanikio mbalimbali ambayo yalileta matokeo chanya katika kuboresha afya kwa akina mama wajawazito.
Mradi huu ulikuwa na afua mbili ambazo ni utafiti wa utekelezwaji wa huduma jumuishi za wajawazito kwa njia ya makundi (Group Antenatal Care) na mfumo wa afya wa kidigitali unaoweza kutumia akili mnemba (AI) katika kutambua matokeo mabaya yanayoweza kutokea wakati wa ujazuzito na hivyo kusaidia watoa huduma wa afya kuchukua hatua stahiki mapema.

Mtoa huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Geita (kulia) akiwasimamia wajawazito kupimana uzito wakati wa huduma kwa njia ya makundi.
Lengo kuu la afua zote mbili ni kumjengea mama mjamzito uwezo binafasi wa kufuatilia maendeleo ya ujauzito wake kupitia wamama wajawazito wenzake, na pia kuwezesha utambuzi wa hali ya hatari kwa haraka wakati wa ujauzito na kuwezesha watoa huduma kufanya maamuzi sahihi ya kuwasaidia wajawazito mapema. Haya ni baadhi ya mafanikio ambayo yameweza kufikiwa ndani ya miaka miwili ya utekelezaji wa mradi huu.
Mradi ulifanikiwa kuwashirikisha wadau mbalimbali na wataalamu wa mifumo ya kompyuta na teknolojia na hatimaye kutengeneza mfumo wa akili mnemba. Mfumo huu una uwezo wa kutabiri hali ya shinikizo la damu au kifafa cha mimba wakati wa ujauzito.
Shirika liko katika hatua za kutafuta wadau mbalimbali ili kuweza kuufanyia majaribio zaidi na mwendelezo wa mfumo huu hili uweze kuwa sehemu ya mifumo ya sasa ya Serikali ya kukusanya taarifa za afya.
Pia, mradi ulifanikiwa kutekeleza afua ya utoaji wa huduma za wajazito kwa njia ya vikundi kama ilivyotarajiwa. Katika afua hii, Mlinde Mama iliwezesha kuundwa kwa vikundi 521 vyenye wajawazito zaidi ya 5,900.
Afua hii ilikuwa ya kipekee kwani ilikuwa ya kwanza kutekelezwa katika nchi yetu huku ikitumia tafiti nyingine za kisayansi ambazo ziliwahi kutekelezwa katika nchi nyingine.
“Katika afua hii, wajawazito walikuwa na uwezo wa kujihudumia wenyewe kwa kutumia vifaa vya kidijitali ambavyo vilitolewa na Shirika letu (PHIT) hivyo kuwafanya akina mama kushirikishwa kikamilifu katika huduma za afya.
“Pia wajawazito waliweza kupewa vitabu vyenye ujumbe wa afya ya mama na mtoto ambapo jumbe hizi ziliweza kushirikishwa kwa wenza wao na jamii inayo wazunguka.
Kutokana na ubunifu wa afua hii, tulishuhudia ongezeko la wajazito wanaojifungulia katika vituo vya afya kutoka asilimia 34 mwaka 2022 kabla ya kuanzishwa kwa mradi na kufikia asilimia 95 baada ya utekelezwaji wa mradi,” anaeleza Mkurugenzi wa Shirika la PHIT, Dk Augustino Hellar.
Aidha, kulikuwa na ongezeko la wajawazito wanaopata dawa za kuzuia malaria kama inavyoshauriwa kutoka asilimia 43 hadi kufikia asilimia 76 baada ya utelekezwaji wa mradi.
Pia mradi ulishuhudia ongezeko la wajazito wanaojifungualia katika vituo vya afya kufikia asilimia 96, upimaji wa shinikizo la damu (100%), upimaji wa kipimo cha pili cha HIV (81%), malaria (84%), na ongezeko kubwa la akina mama wanaopata dawa za kuzuia minyoo na kuongeza damu.
Kwa namna ya pekee wadau mbalimbali ambao walionufaika na utekelezwaji wa mradi huu walitoa maoni yao, wakisisitiza uendelezwaji wa kazi za Mlinde Mama kupitia Serikali na wadau wengine katika sekta ya afya.
Mfano, mjamzito kutoka kituo cha Katoro alisisitiza namna utoaji wa huduma kwa njia ya vikundi inavyosaidia kuwaweka karibu na watoa huduma.
“Kwenye ujauzito wangu wa mwanzo nikuwa naogopa kumuuliza muuguzi maswali, lakini katika kundi tunajadili kila kitu kwa uwazi, na nahisi niko tayari zaidi kwa ajili ya kujifungua.” Pia baadhi ya watoa huduma walitoa maoni yao juu ya utekelezwaji wa mradi wa Mlinde Mama hasa katika afua ya kidijitali.
“Kabla ya mfumo wa kidijitali ambao tunaweka taarifa katika vishikwambi (UCS), tulilazimika kupitia rejesta nyingi kutafuta historia ya mgonjwa. Sasa, kwa kubofya kidogo tu, tunaweza kupata taarifa za kliniki za awali na historia ya ujauzito ya mwanamke yeyote kwa haraka,” anaeleza mtoa huduma Kituo cha Afya cha Katoro.
Kwa upande wa wajumbe wa kamati ya afya ya wilaya walisisitiza juu ya faida zilizopatikana kutokana na ubunifu wa mradi huu.
“Huduma kwa njia ya vikundi imesaidia vituo vyetu kuongeza viwango bora vya viashiria mbalimbali kwa wajawazito. Wanawake hufurahia kuhudhuria kliniki kwa sababu wanapata huduma na kujifunza kutoka kwa wenzao wakisaidiwa na mtoa huduma.
“Bado tuna changamoto ya vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga, lakini bado tuna changamoto ya mahudhurio ya wajawazito kwenye kliniki zetu, na hii iko wazi wengine wanakuja wameishachelewa, lakini pia changamoto ya udhurio la kwanza chini ya wiki 12 na hii ni kiashiria muhimu ambacho tunapimwa kitaifa na kimataifa. Lakini tuna imani kupitia hiki ambacho mmekifanya (PHIT) kitatupa mwelekeo na picha sahihi,” anaeleza Dk Sukari.
Shirika linapenda kuwashukuru wadau wote ambao wamefanikisha mradi huu hususan Serikali ya awamu ya sita ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Afya, TAMISEMI, Kamati ya Afya Mkoa ikiongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dk Omari Sukari na Kamati za afya za wilaya ya Chato na Geita, viongozi wa vituo vya afya, bila kuwasahau wanufaika wetu mama wajawazito ambao walipokea mradi wetu kwa mikono miwili.
Kwa taarifa zaidi: Tembelea tovuti https://phit.or.tz