Yanga yasaka rekodi kwa Stand United

Muktasari:
- Yanga itashuka dimbani leo ambapo itamkosa kiungo wake Pacome Zouzoua ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa siku 14 akiuguza maumivu ya enka.
Dar es Salaam. Yanga inasaka rekodi ya kutinga kwa mara ya 10 mfululizo hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho wakati itakapoikaribisha Stand United leo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni.
Tangu mashindano hayo yaliporudi msimu wa 2015/2016, Yanga imetinga nusu fainali tisa katika awamu tisa ambayo yamefanyika hadi sasa.
Kwa upande mwingine, nyavu za Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kuna uwezekano mkubwa zikatikiswa mara nyingi leo kama historia ya nyuma baina ya timu hizo na makali ya kufunga ambayo kila moja imeonyesha msimu huu.
Mechi baina ya Yanga na Stand United zimekuwa na historia ya kuzalisha idadi kubwa ya mabao ambapo katika mara kumi ambazo zimewahi kukutana hapo nyuma, ni mechi mbili tu ambazo mabao chini ya matatu yalifungwa na zote ziliisha kwa matokeo ya bao 1-0.
Lakini mechi nyingine nane, kila moja ilimalizika kwa kupatikana kwa mabao matatu au zaidi.
Mechi hizo 10 za nyuma baina ya Yanga na Stand United zilizalisha mabao 34 ikiwa ni wastani wa mabao 3.4 kwa mchezo na Yanga ina historia ya kufanya vizuri ambapo ilipata ushindi mara nane na kupoteza mbili.
Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana ilikuwa ni katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa Januari 19, 2019 ambao Stand United iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Ukiachana na historia hiyo, Yanga imekuwa na takwimu bora za kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu msimu huu kama ambavyo Stand United inayo kwenye Ligi ya Championship.
Katika mechi 25 za Ligi Kuu, Yanga imefunga mabao 54 ikiwa ni wastani wa mabao 2.16 kwa mchezo wakati kwenye Ligi ya Championship, Stand United imefunga mabao 42 katika mechi 26 ambayo yanaleta wastani wa bao 1.6 kwa mechi.
Katika mchezo wa leo, Yanga itamkosa kiungo wake Pacome Zouzoua ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa siku 14 akiuguza maumivu ya enka.
Wakati Yanga ikiwa nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu na pointi zake 67, Stand United inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ya Championsip ikiwa imekusanya pointi 55.
Mshindi wa mchezo baina ya Yanga na Stand United leo, atakutana na timu iliyoshinda mchezo wa jana baina ya JKT Tanzania na Pamba Jiji FC. Nahodha msaidizi wa Yanga, Dickson Job amesema kuwa mchezo huo utakuwa mgumu lakini wana imani watapata ushindi.
“Hakuna mechi ambayo Yanga inacheza inakuwa rahisi kwani kila timu inakuwa imejipanga sana kuhakikisha inapata matokeo mazuri dhidi yetu hivyo tunalitambua hilo na tutapambana kuhakikisha tunaingia nusu fainali na naamini Mungu atasaidia tutatimiza hilo,” alisema Job.
Kipa wa Stand United, John Mwenda amesema kuwa mchezo huo ni mgumu kwa upande wao lakini wamejiandaa kuucheza.
“Ni mechi ngumu ukizingatia Yanga ni timu kubwa na inayofanya vizuri pia itakuwa katika uwanja wake wa nyumbani hivyo kuna ugumu kwa upande wetu lakini tutajaribu kupambana nao kwa kadri ya uwezo wetu,” alisema Mwenda.